Kwa Nini Unamuiga Chura? Ondoka Kwenye Hatari Hii!


Categories :

Ukimchukua chura hai na kumweka kwenye maji ya moto, ataruka na kutoka kwenye maji hayo na hivyo lengo la kumpika kutotimia. Lakini kuna njia nyingine ambayo unaweza kumpika chura bila usumbufu wowote. Mchukue chura wako kisha mweke kwenye maji ya baridi, naye ataendelea kuogelea humo na kufurahia. Kisha weka chombo hicho kwenye moto. Kadri muda unavyoenda , joto la maji hayo litakuwa linaongezeka na chura atakuwa anaongeza joto la mwili wake ili liendane na joto la maji linavyozidi kuongezeka.

Kitendo hicho atakachokuwa anafanya chura kinatumia nguvu, hivyo maji yatakavyokuwa yanakaribia kuchemka, chura huyo atakuwa tayari amechoka na hivyo kushindwa kuongeza joto lake. Hapo ndipo atakapoanza kuhisi kuungua na kuamua kuruka nje ya maji hayo. Lakini zoezi hilo halitafanikiwa kwani atakuwa hana nguvu za kufanya hivyo kwani nguvu zote alitumia kuongeza joto wakati maji yakiendelea kushika moto. Hiki kitakuwa ndiyo kifo cha chura.

Unaweza ukawa miongoni mwa watu wanaomdharau chura kwa ujinga ambao anaufanya na labda kuhitimisha kuwa anafanya hivyo kwa sababu hana utashi na akili nyingi. Lakini kwa bahati mbaya na wewe pia inawezekana ni miongoni mwa chura ambao wapo kwenye maji yanayoendelea kushika moto huku ukipambana na kuongeza joto la mwili wako ili kuendana na joto maji. Ndugu! Unapoteza muda toka kwenye maji hayo kabla nguvu zako hazijaisha na kufia humo. Hivi ndivyo ulivyomuiga chura na kutaka kufa kijinga;

Umeendelea kuahirisha mambo na kusema utafanya kesho. Unajua ni nini inabidi ufanye ili utoke kwenye hali ngumu unayopitia, iwe ni afya au uchumi lakini muda wa kufanya ukifika hufanyi. Kwa kuendelea kusema utafanya kesho, ni sawa na chura anayeendelea kukaa kwenye maji ya moto akiamini ataendelea kupambana na kadri joto litakavyokuwa linaendelea. Wakati wa kuweka kazi nia sasa, usiahirishe, kila siku kuna kesho.

Kwa kuridhika na kile unachokipata sasa. Inawezekana upo kwenye ajira au mahali pengine ambapo una uhakika wa kupata chochote kila baada ya muda fulani. Kwa uhakika huo umejisahau na kuona unaweza kutoboa maisha yako kwa stahili hii. Kama unachokipata sasa hakikui ujue hicho kiasi kinakufa taratibu bila ya wewe kugundua, unahitaji kukipa uhai kipato unachokipata sasa kwa kuwekeza na kukizalisha zaidi. Muda mzuri wa kufanya hivyo ni sasa, usisubiri mpaka kipindi unakaribia kustaafu ndipo uanze kuwekeza, litakuwa jambo gumu sana kwako kwani nguvu zako zitakuwa tayari zimepungua.

Kung’ang’ania mahusiano yenye shida. Mahusiano yasiyo na uaminifu huonyesha dalili mapema, japo mwanzoni huhitaji umakini mkubwa kuziona dalili hizo. Chukulia mahusiano yako kipindi cha uchumba , kwa sababu ya upya na udanganyifu wa mahusiano ya kipindi hicho wengi hawaweki nguvu kuchunguza kama kuna udhaifu wowote kwenye mahusiano hayo. Hiki ni kipindi muhimu sana kabla ya kuchukua uamuzi wa kuoana na kuwa vigumu zaidi kuachana na muhusika hayo kama utakuwa hujaridhika nayo. Kabla hujafika mbali kwenye mahusiano ya biashara, jiridhishe kama watu ulioungana nao ni sahihi.

Kuchelewa kufanya maamuzi. Chochote unachofanikiwa kukifanya ni kwa sababu ya maamuzi unayoyafanya. Kwa hiyo ukiona hupati matokeo fulani basi ujue hukufikia maamuzi. Kwa kuendelea kubaki bila kufanya maamuzi au kwa kuchelewa kufanya maamuzi, unazidi kuchelewa kupiga hatua. Hata kama maamuzi unayofanya hayakupi matokeo mazuri, ni bora kuliko kutofanya maamuzi kabisa. Kama umekuwa ukiendelea kuchelewa kufanya maamuzi, basi wewe ni sawa na chura anayeendelea kukakaa kwenye maji yanaoendelea kupashika na kuamini atayashinda.

Chunguza mahali ulipo sasa na yale unayoendelea kuyafanya, inawezekana ulikuwa unaendelea kupoteza muda na nguvu bila kujua. Wewe kuwa mwerevu kuliko chura, fanya maamuzi ya kutoka haraka kwenye hatari hizo hapo juu ili uepuke kifo cha maisha yako ya mafanikio.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *