Hii Ndiyo Siri Ya Kutengeneza Ndoto Kubwa.
Kuna wakati umeona mafanikio ya mtu, ukatamani na wewe kuwa na mafanikio kama hayo. Kuna wakati imekuja picha akilini mwako ukitamani uwe mtu wa namna fulani. Lakini mawazo na picha hizo zikawa zina katishwa na kumbukumbu nyingine zilizopo ndani yako kuwa huwezi kuwa mtu kama huyo kwa sababu mbalimbali kama historia ya maisha yako, kabila lako, elimu uliyo nayo nk.
Kwa sababu ya ukubwa wa picha ulizoziona, umefikiri kuwa watu fulani ndiyo wanaostahili kupata utajiri, fahari, furaha na vingine vizuri na vikubwa na sio wewe. Hii imeenda mbali zaidi kwa kuona kuwa wewe huwezi kutengeneza ndoto kubwa kwani hizo zinawafaa watu wengine. Ndiyo maana licha ya kuupata ujumbe huu ndani yako, umekuwa ukiupuuza ukifikiri huo unakuja kwako kwa kukosea.
Wale uliowaona wamepata mafanikio makubwa maishani mwao hawakuwa na kila kitu ambacho kingewawezesha kutimiza mipango ya ndoto kubwa walizokuwa nazo. Bali walikuwa na kitu kimoja ambacho kimewasaidia kupata vitu walivyo navyo na wewe unaweza kupata vitu hivyo. Kuna siri moja muhimu ambayo wanayo, na wewe unaweza kuitumia na kutengeneza ndoto kubwa kisha kuitimiza na kupata chochote unachotaka. Siri hiyo ni kuwa na kanuni ya kutoa mipaka ya fikra kwa kufikria kwamba kama kungekuwa hakuna kikwazo chochote ungetaka uwe nani au upate nini?
Bila kufuata kanuni hii ni vigumu sana kutengeneza ndoto kubwa kwani kila utakapokuwa unafikiria kutengeneza akili yako itakupa vikwazo. Kwa mfano utakapoanza kufikiri kuwa na ndoto ya kuwa huru kifedha, akili yako itakuletea taswira ya umasikini wa familia yako, kuwa wewe huwezi kufika safari hii kwa sababu huna mwanzo mzuri. Utakapofikiria kuanzisha kampuni fulani , akili yako itakukumbusha na kukuaminisha kuwa kuanzisha kampuni unahitaji uwe na elimu, hivyo wewe huwezi kuwa na ndoto kama hiyo.
Kumbe ili utengeneze ndoto yako kubwa lazima uanze na kanuni hii ya kufikiri na kujiachia kana kwamba hakuna kikwazo chochote. Jiulize swali hili, kama kila kitu kingekuwepo, mazingira yangeruhusu, watu wangekuwa upande wako kana kwamba hakuna kikwazo chochote maisha gani ungetamani uyaishi? Mtu wa namna gani ungetamani uwe? Wapi ungetamani ufike?
Huu ndiyo mwanzo mzuri wa kupata chochote katika maeneo yote ya maisha yako. Katika hatua hii huhitaji kushikilia tena vikwazo, huhitaji kujiuliza tena udhaifu wako wala vikwazo ulivyo navyo, bali unasikiliza matamanio ya maisha yako ya uhuru. Wengi wameishia kuishi ndoto ndogo na maisha ya kawaida kwa sababu ya kuacha akili zao zishikilie vikwazo badala ya kuziacha ziwe huru na kutengeneza maisha wanayoyataka.
Marilyn Monroe alisema ‘’The sky is not the limit. Your mind is’’ akimaanisha kuwa anga sio kizuizi lakini akili yako ndiyo kizuizi. Huu ni ujumbe mzito sana ukiutafakari kwa kina. Kiasi cha mafanikio unachokipata ni kile ambacho akili yako inakipanga. Kama ni kidogo, cha kawaida na hukifurahii tambua kuwa ni kwa sababu ya akili yako kujipangia kiasi kidogo kwa kujiwekea vizuizi.
Ndugu! Umetambua kuwa akili yako inaweza ikatengeneza chochote isipojiwekea mipaka. Hii ni nafasi yako ya kutathmini ndoto ulizonazo sasa, je ulizitengeneza ukifikiri kuwa huna kikwazo chochote? Tumia sasa siri hii ya kuondoa mipaka kwenye fikira wa kutumia siri hii, fikiri kuwa hakuna kikwazo na ona ni kitu gani unakitaka na kwa kiwango gani kwenye kila eneo la maisha yako kisha baada ya kutambua hivyo anza kuweka mipango ya kuvipata. Usijinyime, unaweza kupata chochote kile ambacho akili yako itakipokea na kukiamini.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz