Hii Ndiyo Sababu Kuu Ya Kushindwa Kwako.


Categories :

Neno kushindwa sio zuri masikioni mwa watu wengi. Wengi hutamani maisha yao kwenda kama wanavyotarajia. Lakini mambo huwa tofauti, ni mara chache mambo hutokea kama yalivyotarajiwa. Kiwango cha kushindwa kinatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Kwa ajili ya kushindwa wengi hufa moyo na kuacha kuendelea kuchukua hatua. Ka ajili ya kushindwa, kuna watu huingiwa na hofu ya kuchukua hatua mpya kwa ajili ya kumbukumbu walizokuwa nazo awali.

Kuna sababu nyingi ambazo zimesababisha watu kushindwa, lakini leo nakushirikisha sababu moja kuu inayochangia wewe kushindwa mara nyingi katika maisha yako. Ukichunguza nyakati mbalimbali ambazo umeshindwa, utatambua kuwa sababu hiyo imechangia kwa asilimia kubwa. Sababu hiyo ni kukosa mipango. Kutokuwa na mpango wa namna gani unaenda kufanya jambo ni kuanza kutengeneza mapema mazingira ya kushindwa.

Mipango hutokana na malengo uliyo nayo. Unapokuwa na lengo la kupata kitu fulani, ni lazima uweke mipango ya namna ambavyo utaenda kufanya ili uweze kupata matokeo hayo. Watu wengi wamekosa mipango ya kufanya vitu. Wanafika na kulivamia jambo bila kupanga ni nini watakifanya na njia gani. Ufanisi huwa mdogo sana pale unafanya jambo bila maandalizi yoyote.

Peter Drucker alisema “Action without planning is the reason for every failure.” Ikimaanisha kuwa kuchukua kitendo chochote kile bila mipango ni sababu ya kushindwa. Je huwa unaweka mipango kabla ya kufanya jambo lolote? Una mipango gani juu ya lengo la kupata utajiri? Una mipango gani juu ya lengo la kuimarisha afya yako? Je una mipango gani juu ya kutimiza lengo la kuimarisha mahusiano yako. Kuwa na malengo bila kuweka mipango ya kuchukua hatua ni sababu kuu ya kushindwa kupata mafanikio.

Hata  Benjamin Franklin alisema “If you fail to plan, you are planning to fail!” Akiwa na maana kuwa kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa. Kumbe unapoamua kufanya vitu bila kuvipangilia unakuwa unafanya maandalizi ya kushindwa. Kumbe maandalizi ya kushindwa umekuwa ukiyafanya wewe mwenyewe kila siku kwa kutopanga namna ya kupata matokeo.

Kutumia muda vyema. Moja faida ya kupangilia kazi zako ni kutunza muda. Ukipanga nini unaenda kukifanya katika muda fulani hutababaika tena kujua ni kitu gani inabidi ukifanye kwenye muda fulani. Kujiuliza unafanya nini na kawa namna gani hupoteza muda.

Huongeza ufanisi. Faida nyingine ya kuweka mipango ni kuongeza ufanisi. Unapoweka mipango, akili yako inajiandaa kufanya jambo hilo hata kabla ya muda kufika. Akili kutambua nini unaenda kufanya husaidia kuanza kufanya maandalizi ndani ambako ndiyo chimbuko la ufanisi wa utendaji wako. Pia kwa kuweka mipango utatambua changamoto unazoweza kukutana nazo na kuzitafutia uvumbuzi hata kabla ya kuanza kufanya jambo. Hii itakupa nafasi kubwa ya kufanikiwa kwenye yale unayoyafanya.

Ndugu kufanya mambo bila kuweka mipango ni sawa na kuyaishi malengo au ndoto zako bila mwelekeo. Hii itakusababishia kupata ajali unapoendelea kusafiri kwenye barabara ya  mafanikio yako. Angalia malengo uliyojiwekea kuyatimiza mwaka huu, je umeyawekea mipango na je unaifuata? Natambua una hamu ya kupata mafanikio kwa kuepuka kushindwa mara nyingi. Utayapata mafanikio hayo kwa kuanza kuweka mipango kwenye kila jambo unalotaka kulifanya, usilivamie tu na kuanza kufanya. Pata muda na andika mpango wa kila lengo ulilonalo ili kuwa kwenye njia sahihi ya kutimiza malengo yako.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *