Huu Ndiyo Uhuru Wako Pekee Ambao Unapaswa Kuulinda Usichukuliwe Na Yoyote.
Moja ya kitu kinachotafutwa na binadamu yoyote ni uhuru. Mahangaiko mengi ambayo mwanadamu anayafanya ni kwa nia ya kutafuta uhuru. Uhuru ni hali ya kuwa na uwezo wa kuamua mambo yako mwenyewe bila kuathiriwa na mtu au hali nyingine. Katika hali kama hii kunakuwa hakuna kikwazo chochote kinachoweza kusimama ili usiweze kupata, kujisikia au kwenda popote.
Kinyume cha uhuru ni utumwa. Hii ni hali ya kuwa katika himaya ya mtu au hali fulani. Tunakumbuka kipindi cha ukoloni ambapo watu walikuwa chini ya utumwa. Katika kipindi hicho mtu alikuwa hana uhuru wa maisha yake zaidi kupangiwa cha kufanya. Sasa Nchi nyingi zimepata uhuru na wanana uwezo wa kuamua mambo yao wenyewe. Lakini bado kuna utumwa ambao watu wengi bado wanao. Licha ya uhuru wa nchi ambao tunao bado kuna uwezekanao wa mtu kuendelea kuwa mtumwa wa maisha yake mwenyewe.
Kuna utumwa mwingi ambao binadamu wa leo bado anaendelea kupata, mojawapo ni utumwa wa kiuchumi na wa kifikra. Utumwa wa fikra hutokea pale mtu anapolazimishwa nini akifikiri, namna gani ajisikie na nini akiamue kwenye matukio mbalimbali. Kuna matukio mbalimbali huwa yanatokea katika maisha ya mwanadamu ya kila siku. Matukio hayo ndiyo huwa yaonyesha kama mtu anaweza kulinda uhuru wake au la.
Licha ya utumwa ambao unaweza ukamzunguka na kumtesa mwanadamu, lakini ni katika eneo hili kati ya matukio na maamuzi ndipo mtu anaweza kuwa huru. Uhuru huo ni kuwa uwezo wa kuamua matokeo ya matukio. Je matukio yanayotokea huwa yanakuachaje? Yanakuacha na huzuni, masikitiko au malalamiko? Matukio mengi ndiyo yanayowatesa wengi na kutofurahia maisha. Lakini kwa upande mwingine sio matukio yanayomtesa mtu, bali ni matokeo ya matukio hayo ndiyo yanayoleta utumwa kwa watu. Wengi wamepata shida hii kwa kutokutambua kuwa wana uhuru wa kuamua matokeo ya matukio yoyote yale.
Kwa mfano watu wengi huumia sana baada ya watu wengine kuwaonea. Yaani kupata adhabu kwa kosa ambalo hawakulitenda. Watu wengi huumia sana baada ya kutukanwa wakiamini watu hao wamewadharau. Watu wengi hulalamika kama hawajapewa haki ambayo walistahili. Je wewe ni miongoni mwa watu hao ambao wapo kwenye utumwa huo?
Ngoja nikupe siri leo ya kuwa huru katika eneo hili ambalo ndiyo kiini cha uhuru wa maisha yako. Una uhuru wa kuamua nini kitokee baada ya tukio kutokea. Lakini umekuwa ukikosa uhuru huo kwa sababu ya kutokuchagua matokeo baada ya tukio. Umeacha uchaguliwe ujisikieje baada ya kukutana na maisha magumu badala ya wewe kuchagua ujisikieje hata katika mazingira hayo. Una uhuru huo ambao hakuna mtu anayeweza kuuchukua kutoka kwako ukiamua kuutumia. Hata kama maisha ni magumu unaweza kuchagua kuchukua jukumu la kuyatengeneza maisha hayo badala ya kumlalamikia mtu fulani ukiamini ndiye aliyesababisha.
Njia pekee ya kujipatia na kuulinda uhuru huu ni kuwa wa kwanza kutengeneza majibu ya matukio na si kusubiri kutengenezewa. Kusubiri kutengenezewa ni kukaribisha utumwa. Kuanzia sasa, kwa kila tukio linalotokea, andaa matokeo badala ya kusubiria upewe. Usisubiri uambiwe ujisikieje amua wewe ujisikieje. Usiache hisia zako zikaamua, shirikisha akili yako iamue. Hii ni tabia ambayo itakulazimu kuijenga. Itakupa ugumu mwanzoni lakini jisukume na kufanikiwa kuijenga, ndipo utakapopata uhuru huu muhimu na kuyafurahia maisha yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz