Hiki Ndiyo Kitu Cha Kwanza Unachotakiwa Ukifanye Ili Kuishi Maisha Yako Halisi.


Categories :



Kila mtu ana kitu cha thamani ndani yake, kitu hicho ni uwezo wa kipekee alionao ndani yake. Uwezo huo ndiyo utakaomwezesha mtu kuishi maisha yake halisi.

Ni kupitia uwezo huo mtu anaweza kuishi maisha yake ya thamani. Kwa kutumia uwezo mtu anaweza kuishi kusudi la maisha yake kikamilifu. Ni kupitia uwezo huu mtu anaweza kutengeneza ndoto kubwa na kuitimiza. Ni kupitia uwezo huu mtu anaweka malengo na kuyatimiza. Ni uwezo unaomfanya mtu kutoa thamani kwa watu. Kumbe uwezo ndiyo unaompa mtu utajiri.

Lakini jiulize, kama kila mtu ana uwezo ndani yake na ndiyo unaompa mtu utajiri, kwa nini watu wengi bado ni masikini? Kwa nini watu wengi bado hawaishi makusudi, ndoto au malengo yao? Kwa watu wengi bado hawana utajiri wa furaha? Unaweza kusema sababu nyingi kuhusu hili, lakini miongoni mwa sababu kuu ni kutojiamini.


Kutojiamini ni kikiwazo kikubwa sana kinachowafanya watu wengi kutoishi maisha yao halisi. Kuishi maisha yako halisi kunaanzia ndani mwako kwa kujiona una kitu cha thamani kubwa kinachoweza kukusaidia kutoa thamani kubwa kwa watu wengine. Huku ni kujiamini. Mtu anaposhindwa kujiamini anabaki kuishi maisha yoyote yale. Huona kuwa hana kitu kikubwa ambacho anaweza kukisimamia kama yeye na kuionyesha dunia thamani yake.

Kwa kushindwa kujiamini mtu ameshindwa kutambua thamani kubwa iliyopo ndani yao na kuipa dunia. Kwa kushindwa kujiamini mtu ameamini kuwa hawezi kupata mafanikio bila ya kuangalia na kuiga wanavyofanya watu wengine. Kwa kutojiamini mtu ameishia kujidharau na kuona maisha ya ndoto na mafanikio makubwa ni ya watu wa aina fulani na siyo yeye. Hii ndiyo ilisababisha watu wengi kuishi maisha ya kuiga, kama ni biashara wameacha kubuni za kwao na kusubiri kuona ni biashara gani inayolipa muda huo na wao kuanzisha hizo.

Zifuatazo ni hatua unaweza kuchukua ili kuanza kujiamini na kuishi maisha yako halisi,

Jione wewe ni wa pekee. Licha ya dunia kuwa na watu zaidi ya bilioni nane lakini kuna wewe mmoja tu. Yaani hakuna hata mtu mmoja anayefanana na wewe kwa kila kitu. Una kitu ndani yako ambacho kinakosekana kwa watu wengine, huu ni uwezo wako wa kipekee ambao ni wewe pekee uliyeushikilia. Jiamini na kuona una kitu cha pekee ndani yako na hivyo unaweza kuipa dunia thamani ya kipekee na kuishi maisha yako halisi.

Tambua na ishi kusudi lako. Una sababu maalumu ya kuwepo hapa duniani. Una kazi maalumu ya kuifanya hapa duniani ambayo haiwezi kufanywa na mtu mwingine. Ukifanikiwa kuliishi kusudi hilo kikamilifu unaipa dunia thamani na kuziba pengo lililokuwepo. Ukifanikiwa kulitambua hili, utajiamini na kuona thamani kubwa uliyonayo hapa duniani kisha kuishi maisha yako halisi.

Usiige maisha ya watu wengine. Kuiga kwa asilimia mia moja vitu wanavyovifanya watu wengine kunapunguza uwezekano wa kuishi maisha yako halisi. Kila wakati jiulize ndani yako, ni kitu gani unapenda kukifanya? Ni kitu gani unaweza kukifanya kwa ubora zaidi kuliko wengine. Huko ndiko kwenye upekee wako na kunakokuwezesha kuishi uhalisia wako.

Ndugu! Mafanikio yako yapo kwenye kuishi maisha yako halisi na sio bora maisha. Huwezi kuishi maisha yako halisi kama hutachukua hatua ya kujiamini kwa kuona una kitu kikubwa na chenye thamani kubwa ndani yako kinacho kukusaidia kutoa thamani kubwa kwa watu wengine. Kuanzia sasa jiamini; ona wewe ni wa pekee, tambua kusudi lako na kuliishi kikamilifu na acha kuiga kila kitu bali fanya cha pekee kilichopo ndani yako.

Kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI kimeelezea kiundani zaidi kuhusu kusudi lako na upekee ulionao ambao utakupa kujiamini na kupata maisha halisi yenye mafanikio makubwa. Pata nakala yako leo kwa kupiga simu 075220688 ili ujifunze zaidi na kuishi maisha yako halisi.


Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *