Huu Ndiyo Ukuta Sahihi Wa Kuegesha Ngazi Yako Na Kufanikiwa Kufika Kileleni.


Categories :

Imekuwa ni kawaida ya watu kutumia ngazi pale wanapotaka kufikia sehemu ambayo mikono yao haiwezi kufika miguu yao ikiwa ardhini. Kwa kutumia ngazi hizo watu wamefanikiwa kufikia hata kimo ambacho kingekuwa ni vigumu kwa hali ya kawaida kufikika. Licha ya kuwepo uwezekano wa kufika juu sana, lakini mtu hulazimika kupanda ngazi moja badala ya nyingine ili asianguke.

Maisha yako ya mafanikio ni kupanda kutoka ngazi moja kwenda nyingine. Huwezi kukua na kufika kileleni kama utakuwa hutembei kutoka ngazi moja kwenda nyingine. Ni kwa kupitia ngazi hizo ndipo unapoweza kupiga hatua kubwa na kufika sehemu ya juu sana ambapo ingekuwa ngumu kufika kwa hali ya kawaida. Kufika juu kwa kutumia ngazi kunakulazimu kuweka ngazi kwenye ukuta sahihi. Ukiweka kwenye ukuta usio sahihi, kuna nafasi kubwa ya kufikishwa sehemu ambayo sio sahihi, kisha ukawa umepoteza nguvu na muda.

Kuegesha ngazi kwenye ukuta usio sahihi imekuwa miongoni mwa sababu ya watu wengi kukosa  mafanikio makubwa licha ya kuendelea kuweka nguvu kubwa na muda mwingi kwenye vitu wanavyovifanya.  Umeshuhudia watu wakiendelea kuwa ‘busy’ kila siku lakini wakiambulia mafanikio kiduchu, hii ni kwa sababu ya kuegesha ngazi kwenye ukuta usio sahihi ambao unawapeleka haraka eneo lisilo sahihi.  Kuna ukuta sahihi ambao ukifanikiwa kuegesha ngazi yako utaweza kupiga hatua kubwa na kufika kileleni, ukuta huo ni Anza Na Mwisho Kwenye Akili Yako.

Kuanza na mwisho kwenye akili yako ni kuwa na picha ya nini muhimu katika maisha yako kisha kuilinda picha hiyo muda wote ili chochote unachokifanya kiendane na ile picha ya kitu unachokitaka. Maana nyingine ya kuanza na mwisho kwenye akili yako ni kuwa na picha ya mwisho wa safari yako tangu mwanzo, hivyo kila siku unapoamuka unaona mwishao wa safari yako ya mafanikio yako. Kila unapowaza nini ukifanye cha kwanza unachokiona akilini mwako ni ile picha uliyoitengeneza.

Hiki ni kitu muhimu sana ambacho kitakusaidia kupiga hatua. Kuweka ngazi ni kuweka jitihada ili kupata mafanikio makubwa unayostahili. Kuweka ngazi ni jitihada, maarifa na nguvu zinazowekwa kila siku katika mambo unayoyafanya. Ili hivi vyote vikusaidie kupiga hatua ambazo zitakusaidia kufika kileleni, ni lazima ziwekezwe eneo sahihi. Namna pekee ya kuwekeza kwenye eneo sahihi ni kuwa na picha ya wazi kabisa ya wapi unakotaka kufika. Hii ni dhana ya kuanza na mwisho kwenye akili yako. Usipokuwa na mwisho akilini mwako kuna hatari ya kufika kokote hata upotevuni.

Kama ukiegesha ngazi kwenye ukuta sahihi, kila jitihada unayoifanya itakupeleka kwenye ngazi nyingine na ya juu ya mafanikio yako. Pia kila ongezeko lolote la mwendo litakufanya ufike unakotaka kwa uharaka zaidi. Hii ni sawa na gari ambalo lipo kwenye njia sahihi, kila ongezo la mwendokasi litapelekea gari hilo kuwahi kufika safari. Lakini kama gari hilohilo litakuwa kwenye uelekeo usio sahihi, ongezeko la mwendo wowote ule litapelekea gari hilo kuendelea kupotea.

Chukua hatua: Pata picha ya kile unachokitaka kwenye kila eneo la maisha yako; binafsi, kazi/biashara, fedha, afya na mahusiano. Unaweza kuijenga picha hii kwa kukaa chini na kutafakari kwa utulivu na kina, huku ukiona kama tayari una kitu hicho mkononi. Pia ili picha hiyo ikae vizuri andika mara kwa mara kile unachotarajia kukipata mwisho wa safari yako. Huu ndiyo utakuwa ukuta sahihi wa kuegesha ngazi yako. Kisha kila jitihada utakazokuwa unaweka, elekeza kwenye picha kamili iliyopo kwenye akili yako. Kamwe usiwekeze nguvu eneo jingine lolote.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *