Kwa Nini Hutumii Mtaji Huu Wa Utajiri Uliokuzunguka Kwa Siku Nyingi?


Categories :



Katika maneno yanayopendwa kusikiwa na masikio ya watu wengi ni utajiri. Utajiri ni utele katika maisha ya mtu. Huu ni utele wa kila eneo la maisha yake. Katika hali ya utajiri mtu hana kikwazo chochote cha kupata anachokitaka, kujisikia anavyopenda, kwenda anakokutaka nk. Ndiyo maana hata wale waliodanganywa kuwa utajiri ni mbaya hupenda kusikia neno hili na kulishika mara baada ya kuutambua ukweli.


Lakini licha ya watu wengi kupenda kusikia neno hili, bado kuna idadi kubwa ya watu walioukosa utajiri huo. Kinyume cha utajiri ni umasikini, hivyo bado kuna idadi kubwa ya watu ambao ni masikini kwenye maeneo yote ya maisha yao.

Kuna mtaji mkuu wa utajiri ambao kila mtu hupewa mradi bado yu hai. Kila mtu ana nafasi sawa ya kutumia mtaji huo na kupata utajiri katika maisha yake. Mtaji huo ni muda. Ndiyo ni muda ambao ndiyo uliokuweka hapa dunia na ambao unamruhusu kila mtu kuwa tajiri. Hakuna mtu anayeweza kufanya jambo lolote bila muda. Ni kupitia muda ndipo unapoweza kutengeneza mazingira ya kuwa na utele kwenye kila eneo la maisha yako.

Muda ni maisha ya mtu na kupitia maisha ndipo unapoweza kutengeneza utajiri wako. Kuupata au kuukosa utajiri kunategemea namna ulivyoweza kuutumia muda uliokuwa nao. Maisha yako ya sasa ni taswira ya matumizi ya muda wako uliopita. Kama umepiga hatua kubwa katika maisha yako, tambua hayo ni matunda ya matumizi ya muda wako. Kwa lugha rahisi. Ulivyo leo ni matokeo ya namna ulivyoutumia muda uliokwisha pita.

Kama watu wawili walizaliwa siku moja na wote bado wapo hai, wote wawili wamekuwa na mtaji sawa na kuwa na utajiri unaolingana. Lakini ni rahisi kuwaona watu hao wakitofautiana kwa mbali sana kutokana na matumizi tofauti ya mtaji muda.

Ulikuwa na mtaji wa muda kwa kipindi kilichopita. Kama hukuweza kutumia mtaji huu vyema kupata utajiri, una nafasi nyingine ya kutengeneza utajiri wa maisha yako katika kila siku;

Tambua vipaumbele vyako. Umefika hapo kwa sababu ya namna ambayo umekuwa ukitumia muda wako. Kwa kutokutambua wapi utaelekeza muda wako, umeendelea kutumia muda wako popote hata kule ambako kumekuwa hakuna manufaa na hivyo kukosa kutengeneza utajiri wako. Nini unataka maishani mwako? Vitu gani vina thamani kubwa katika maisha yako? Vitu gani ukivipata utakuwa umefikia utele katika maisha yako? Huko ndiko kwa kuelekeza muda wako mwingi ili uweze kufikia utajiri. Je vipaumbele vyako ni biashara ambayo baada ya kukikuza itakupa uhuru wa fedha? Je kipauambele chako ni kutengeneza mahusiano bora ili yagubikwe na upendo na umoja?

Thamani. Chanzo cha utajiri wowote ule ni thamani unayowapa watu wengine. Kwa kutumia mtaji huu wa muda ambao tayari unao hakikisha unatatua changamoto zinazowakabili watu wengine. Kama fedha unazozalisha sasa ni kidogo, tambua kuwa thamani unayoitoa sasa ni kidogo. Ili uweze kujenga utajiri, kuhakikisha unaelekeza mtaji wa muda wako kwenye kutengeneza na kuongeza thamani kwa watu.

Ipangilie siku yako. Siku ni muda ambao ndiyo unaoweza kuupangilia vizuri na kisha ukautumia vizuri kukupa utajiri wako. Mafanikio makubwa unayoyatamani yatatokana na jinsi utakavyoweza kutengeneza mafanikio madogo kila siku. Mafanikio mdogo ya kila siku yatakusanyika na kutengeneza mafanikio makubwa. Ili uweze kuzalisha matokeo kila siku za kutengeneza utajiri huna budi kuipangilia siku yako vyema. Kabla hujaianza siku yako hakikisha unatambua nini utaenda kukifanya kwenye siku hiyo husika.

Tathmini. Ili uweze kuutumia mtaji wa muda vizuri, huna budi kufanya tathmini ya namna gani unautumia muda huo. Tathmini itakuonyesha wapi inakupasa ufanye marekebisho. Ukishaupoteza muda hutaupata tena. Tambua mapema kama kuna matumizi ya muda yasiyo na tija.

Ndugu huu ndiyo mtaji ambao umekuwa nao tangu uzaliwe. Ungeutumia vizuri tangu mwanzo, sasa ungekuwa tayari tajiri. Nafasi nyingine ya kupata utajiri huo ni kutumia muda ulionao sasa. Kuanzia leo hakikisha unatambua vipaumbele vyako ambako utautumia muda wako mwingi. Kisha anza kutumia vizuri kila muda wako utakaobahatika kuupata ili kutoa thamani kubwa kwa watu wengine.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *