Unaweza Kushinda Mashindano Hata Kwa Kutanguliza Pua Tu!
Farasi wengi wanapokuwa kwenye mashindano, mshindi hupatikana kwa kuangalia nani anayezidi wenzake baada ya umbali wa kukimbia mashindano kukamilika. Mara nyingine hutokea mmoja kuwazidi wenzake kwa pua yake kutangulia kuliko wenzake na hivyo yeye kutunikiwa ushindi.
Hili ni funzo kubwa sana katika maisha yetu ya ushindi, huwa tunafikiria kuwa ili uwe mshindi lazima uwe tofauti sana na watu wengine tena katika mambo makubwa. Hii sio kweli kwani ni tofauti ndogo tu ambazo unaweza kufanya tofauti na watu wengine au juu yako mwenyewe ndizo zinazoweza kukupa ushindi mkubwa sana katika maisha yako.
Unahitaji kuangalia ni vitu gani unaweza kufanya vizuri zaidi ya watu wengine. Pale watu wengine wanapoendelea kufanya kimazoea ndipo unapotakiwa kuona ni kitu gani hata kidogo ambacho unaweza kukifanya zaidi ya wengine. Kutabasamu tu unapowahudumia wateja unaweza ukaona jambo dogo sana. Lakini ukiamua kufanya hilo kwenye biashara na ukijitofautisha na watu wengine, utashangaa jinsi itakavyoweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye matokeo.
Kama umezoea kuamka saa kumi na mbili asubuhi, na ukaamua kujitofautisha mwenyewe kwa kuanza kuamka saa kumi na moja na ukatumia saa moja hiyo kupanga ratiba ya siku, kutafakari malengo yako, kufanya mazoezi, kusoma kitabu nk utashangaa jinsi mabadiliko madogo yatakavyokuletea mapinduzi makubwa kwenye matokeo ya maisha yako.
Kujitofautisha kunaweza kukawa juu yako na sio watu wengine tu. Angalia ni kwa namna gani unaweza kuitofautisha jana yako na leo. Angalia matokeo yako jana yaliishia wapi kisha angalia jinsi unavyoweza kupata matokeo makubwa au bora zaidi ya jana, hata kama ni kidogo sana. Ukiweza kujitofautisha hivyo kila siku, utaona mabadiliko makubwa sana kadri muda unavyoendelea.
Usipende ufanano kwani ni zao la mazoea. Ukiwa unafanya vitu kwa mazoea utakaribisha ufanano kwa kuona unafanya vile vile na hivyo kutotegemea matokeo ya utoafuti wowote.
Angalia mambo yoyote katika maisha yako ambayo unaona kuna fursa ya kufanya tofauti na ulivyozoea. Ainisha ni nini unachoweza kufanya kwa utofauti na kila siku fanya utofauti huo huku ukiendelea kukua.
Biashara. Panga kuongeza hata mteja mmoja kwenye biashara yako kila siku. Unaweza kuona ni kidogo sana lakini tofauti hii italeta mabadiliko makubwa sana mwisho wa siku. Ukifanya mabadiliko hata hayo madogo kwa mwezi mmoja tu, utakuwa na wateja thelathini mwisho wa mwezi, je vipi kama utafanya hivyo kwa mwaka mzima?
Akiba. Hakuna utajiri unaoweza kuupata bila kuweka akiba. kujenga tabia ya kuweka imekuwa changamoto kwa watu wengi, ili kuijenga tabia hii unaweza kutokeza pua na kushindwa kwa kuanza kuweka hata 5% tu ya kila kipato na utashangaa kiasi kikubwa utakachoweza kukikusanya baada ya muda mfupi tu.
Nidhamu. Kufanya vile ulivyopanga ni msingi mkuu sana wa kupata kile unachokitaka. hii huitwa nidhamu. kuishi nidhamu pia imekuwa changamoto kwa watu wengi kwani mara nyingine huwalazimu watu kutoka nje ya mazoea. Utaanza kupata matokeo ya utofauti kama utafanikiwa kuanza kujenga nidhamu hata kwa kutokezea pua kwa kujilazimisha kufanya jambo moja ambalo ni muhimu sana kwanya orodha yako ya vitu vya kufanya.
Ushindi katika maisha yako unapatikana hata kwa kufanya vitu kwa utofauti mdogo tu kutoka kwenye vile unavyofanya sasa. Kabla ya kufikiria mambo makubwa unayoweza kufanya, angalia ni vitu gani unavyoweza kuanza kufanya hata kwa utofauti mdogo katika maeneo yaliyoainishwa hapo juu.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
Nimekupata mkuu mafunzo Yako very fantastic broo congratulations
Karibu sana Paschal, yatumie yatakupa matokeo