Hizi Ndizo Hasara Ulizozipata Kwa Kuwahukumu Watu Bila Kujua Ukweli


Categories :

Wakanye wanao! Una malezi mabaya! Haya yalikuwa ni maneno ya baadhi ya abiria waliokuwa wamepanda gari moja na baba aliyekuwa pamoja na watoto. Baba mmoja aliingia kwenye usafiri wa uma na watoto wawili na kukaa kwenye kiti. Wakati safari ikiendelea, watoto walikuwa wakipiga kelele huku wakirukaruka kutoka kiti kimoja kwenda kingine. Hii iliwakera abiria wengine waliokuwa karibu nao. Wakati wakitarajia baba yao awakataze wasifanye hivyo, hali ilikuwa tofauti kwani baba huyo aliwaacha waendelee na vurugu hizo huku akiwatazama tu.

Baada ya muda kupita baadhi ya abiria walipandwa na hasira na kuanza kumfokea baba yule wakimshutumu ni kwa nini amewaacha watoto wafanye vurugu kiasi kile huku wakimhukumu ni kwa nini amewalea katika malezi mabovu kama yale. Yule baba kwa dakika kadhaa aliwaangalia tu watu wale huku wakiendelea kumshutumu. Kuna baadhi ya watu walianza kuamini kuwa inawezekana alikuwa hayupo vizuri kiakili. Baada ya abiria kupungua mtu mmoja akaenda na kukaa karibu na yule baba na kwa upole akamuuliza nini maana ya hayo yote yaliyokuwa yanatokea?

Baba yule akamjibu yule mtu huku akitoa machozi kuwa niliacha watoto hao waendelee kucheza kwani niliona tayari kuna kitu kikubwa walikuwa wamekipoteza kwenye maisha yao. Aliendelea kumueleza yule mtu kuwa watoto hawa wamefiwa na mama yao ambaye alikuwa ni mtu wa karibu sana kwao na aliyewaonyesha upendo mkubwa. Najaribu kuwaza ni maisha gani watakayoishi bila mama yao. Nafsi ilikuwa inanisuta kuwakanya kwani najua ni huzuni gani watakayokuwa nayo baada ya kufika nyumbani na kukuta mama yao amefariki.

Ndugu ni mara ngapi umewahukumu watu wa kuzingatia mwonekano wa nje tu wa jambo bila kujua undani wake? Je na wewe ni miongoni mwa abiria wale ambao walimhukumu yule baba na watoto bila kujua kile kilichokuwa kinawasibu? Kuna matukio mengi sana umehitimisha bila kujua ukweli wake. Kwa kufanya hivyo umepata hasara kubwa maishani mwako.

Zifuatazo ni hasara za hukumu bila kujua undani wake;

Umekosa fursa: Kwa kukihukumu kitu au mtu tofauti na uhalisia, umekosa fursa nyingi ambazo zingekuwa msaada wako. Kwa kuhukumu vibaya umekosa msaada ambao ungeupata kwa mtu. Ni mara ngapi umemuona mtu ungali una shida lakini ukamhukumu kuwa hana uwezo wa kukusaidia kwa mtazamo wa nje tu. Kuanzia sasa muone kila mtu ana thamani na anaweza kukupa kitu chenye thamani kwako.

Umejiongezea huzuni. Kuhukumu bila kujua undani wake imekuwa ni chanzo cha wewe kujiongezea masikitiko na huzuni. Ukimuhukumu mtu kwa kutokukujibu baada ya kumsalimia, ni rahisi sana kukaribisha huzuni ndani yako. Anaweza akawa hajasikia, wewe ukajua amenyamaza kwa makusudi, anaweza akawa na msongo wa mawazo tu, wewe ukajua ana dharau. Kabla hujafika kwenye hukumu pata sababu halisi ya jambo hilo vinginevyo lipuuzie.

Kukosa thamani za watu wengine. Kila mtu ana thamani ya pekee katika maisha yake, thamani hiyo ni ngumu kuipata kama utamhukumu mtu tofauti na uhalisia. Huwezi ukajua thamani ya mtu kwa kumhukumu kwa mwonekano wa nje tu au kutokana na vitu vichache alivyovifanya. Kuna thamani kubwa ungeweza kuzipata kwa watu na zikawa msaada kwako kama usingeweka ukuta kati yako na yeye kwa kumhukumu tofauti na uhalisia. Usimdharau mtu kwa mtazamo wa nje tu.

Umepunguza au kukosa mahusiano mazuri na watu wengine.  Unapomhukumu mtu kwa ubaya, inadhoofisha mahusiano na mtu huyo. Baada ya kumhukumu mtu kuwa ana dharau baada ya kutokukusalimia, ni rahisi sana na wewe kupunguza upendo kwake kama hupo makini. Kuimarisha mahusiano bora, usimhukumu mtu bila kuujua ukweli halisi.

Maisha yenye mafanikio makubwa na furaha tele, yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mahusiano uliyonayo na watu wanaokuzunguka. Ili kuwa na mahusiano bora na kuepuka hasara hizo hapo juu epuka hukumu bila kuja undani wake. Kuanzia sasa usikurupuke tu na hukumu bila kujua ukweli, bali jiridhishe kwanza.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *