Huu Ndiyo Msingi Imara Wa Nyumba Ya Utajiri Wako.


Categories :



Nyumba imara hujengwa juu ya msingi imara. Wengi hupendezwa na rangi za kuta za nyumba zinazoonekana baadaye, lakini uimara wa hizo kuta zitategemea ni kwa uimara gani msingi huo ulijengwa. Hivyo uimara au ubovu wa nyumba hutegemea msingi wa nyumba hiyo.

Mara nyingi msingi wa nyumba huwa hauonekani na hivyo watu kutotilia maanani kuhusu msingi badala yake kuangalia tu vitu vinavyoonekana juu ya msingi.

Licha ya umuhimu wake msingi huo hufukiwa chini. Lakini licha ya kutotiliwa maanani, ukubwa au urefu wa jengo hutegemea ni ubora wa msingi uliojiwekea. Hivyo ili jengo liweze kupanda juu sana, msingi wake lazima ushuke chini zaidi. Utajiri ni kitu kinachotafutwa karibu na kila mtu duniani. Jitihada nyingi zinazofanyika ni kwa ajili ya kupata utajiri kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yake. Lakini changamoto kubwa inayokumba watu wengi ni kutokutambua msingi ambao utajiri imara utajengwa kwa huo. Msingi wa kujenga nyumba imara ya utajiri wako ni THAMANI.



Thamani ni kile unachotoa kwa wengine na kikasaidia kutatua changamoto zinazowakabili. Hivyo thamani ni kutatua matatizo ya watu wengine. Unaweza kuwapa thamani wengine kwa kuwapa njia ya kuwapa bidhaa au huduma. Utajiri unaouona kwa watu wengine wameupata kwa kupitia msingi huu wa kutoa thamani kwa watu wengine.

Kumbe kama wewe bado ni masikini katika eneo lolote lile maishani swali la kwanza muhimu unalotakiwa kujiuliza ni thamani gani unatoa kwa watu wengine? Hakuna namna nyingine ya kupata utajiri zaidi ya kuwapa watu wengine thamani. Kumbe kabla hujakimbilia kutaka kupokea fedha ya mtu huna budi kujiuliza ni thamani gani unampa.

Utajiri unaenda sambamba na thamani. Kama unataka kuongeza mali au fedha basi huna budi kuongeza thamani unayoitoa kwa watu wengine.

Haya ni maeneo unayoweza kuanza kuongeza thamani na kujenga utajiri;

Biashara: Biashara yako lazima iwe inatatua tatizo fulani linalowakabili watu. Biashara yako inaweza kutoa bidhaa, huduma au vyote. Biashara yako lazima ijengwe kwenye kukua kithamani kila wakati ili uweze kufikia utajiri. Kila wakati fikiria ni kwa namna gani unaujenga na kuimarisha msingi huu kwenye biashara yako. Je ni kwa kuongeza huduma kwa wateja wazidi kujiona wao ni wafalme? Je ni kwa kuongeza idadi ya bidhaa ili wapate kwa wingi? Je au ni kwa kuongeza ubora wa bidhaa? Ongeza thamani ya biashara yako nayo itakupa utajiri.

Binafsi. Utajiri wako binafsi upo kwenye kuishi kusudi lako kikamilifu. Pale unapotambua na kuliishi kusudi hilo kikamilifu ndipo utakapofanikiwa kutoa thamani kubwa kwa watu wengine na kupata utajiri na utoshelevu. Kitu gani unawiwa ukifanya kuwasaidia watu wengine. Anza kuishi kusudi lako na utajiri utakuja mikononi mwako.

Mahusiano. Moja eneo ambalo watu wengi wanaukosa utajiri ni eneo la mahusiano. Unawapa thamani gani watu wa karibu yako ili mzidi kushikamana na kupendana. Toa thamani kwao hata kabla ya kufikiria kupokea. Wape muda maalumu na wasaidie katika shida za. Huu ni msingi wa utajiri katika mahusiano.

Naamini unapenda kuwa tajiri katika maeneo mbalimbali ya maisha yako. Kwenye kila eneo angalia ni thamani gani unaweza kuitoa ili upate utajiri. Anza na maeneo matatu hapo juu.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *