Huu Ndiyo Utabiri Muhimu Sana Unaotakiwa Kuufanya Mwenyewe Maishani Mwako.
Umeshawahi kusikia watu wakisema wanaweza kutabiri maisha ya watu wengine. Umeshawaona waganga wa kienyeji wakisema wanatoa huduma za kutabiri maisha yako kwenye eneo la mahusiano (ndoa) au utajiri wa fedha nk. Umewaona pia viongozi wa dini wakitabiri wapi utakuwa muda fulani ujao. Inawezekana na wewe pia ulienda ukatabiriwa kuhusu maisha yako.
Kutabiri ni hali ya kuonyesha kitu kinachoweza kutokea katika kipindi kijacho cha maisha ya mtu. Kwa muda wa sasa mtabiri anakuwa hana matokeo, lakini hujaribu kuona yale atakayoyapata mtabiriwa wakati ujao. Watabiri hao wamefanya kazi hizo kwa kutumia nyota au nguvu nyingine. Kuna wakati yale yaliyotabiriwa yametokea na mara nyingine hayajatokea. Kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa matokeo, kazi ya utabiri imeonekana kuwa ngumu na mara nyingine haina uhakika.
Lakini licha ya utabiri kuwa mgumu lakini wewe mwenyewe unaweza kuwa mtabiri mzuri tu wa maisha yako. Utabiri wako hautakuwa wa kutumia nyota au alama za wanyama au majira au namna nyingine wanazotumia watabiri. Kitu kimoja ambacho unaweza kutabiri na kikatokea ni MAFANIKIO. Kama kuna mafanikio yoyote uliyonayo basi hayo ni matokeo ya utabiri ulioufanya maishani mwako muda uliopita. Katika kutabiri kwako, unaweza kujua kuwa utayapata au utayakosa mafanikio katika maisha yako.
Utabiri huu unawezekana na unakiwa wa kweli kwa sababu ya kuwepo kwa kanuni zinazoendesha mafanikio. Ili uyapate mafanikio lazima uzifuate kanuni hizo. Hizi ni kanuni za asili, na yoyote anayezifuata zinampa matokeo na yule ambaye hazifuati anayakosa matokeo hayo. Moja ya kanuni hizo ni kanuni ya kisababishi na matokeo.
Kanuni ya kisababishi na matokeo inatuonyesha kuwa hakuna matokeo yanayoweza kutokea bila kuwa na kisababishi. Pia popote utakapoweka kisababishi, kuna uwezekano wa kupata matokeo. Mafanikio ni matokeo ya visababishi mbalimbali katika maisha yako. Hakuna muujiza wa mafanikio unaoweza kutokea bila ya kuwa na visababishi. Hivyo katika maisha yako kama hakuna mafanikio ujue kuwa kuna shida kwenye visababishi.
Hii sheria ya mafanikio inakufanya uwe mtabiri mzuri na mwaminifu wa maisha yako. Kumbe chochote unachokifanya leo unajitabiria matokeo utakayopata muda ujao. Kitu cha ajabu ni hili, kama unavyoweza kuwa mzuri kutabiri mafanikio ndivyo kwenye kushindwa. Kama unakuwa mtabiri mzuri wa mafanikio kwa kuzingatia kanuni vivo hivyo unavyoweza kujihakikishia kushindwa pale unaposhindwa kufuata kanuni za mafanikio.
Nakushauri usijikite kutabiri kushindwa katika maisha yako, badala yake kwenye mafanikio. Unaweza kuanza sasa kutabiri mafanikio unayoweza kupata mwaka mmoja, mitano, kumi hamsini ijayo na maishani mwako kiujumla.
Ufuatao ni utabiri wa uhakika unaweza kuanza kuufanya katika maisha yako na kufanikiwa kuwa mtabiri bora wa maisha yako;
1. Unaweza kutabiri utajiri kama kuna kisababishi thamani unachowapa watu wengine. Pia unaweza kutabiri utajiri kama utakuwa hutumii kipato chote bali kutenga kwa mfano 10% ya kila kipato chako na kukiwekeza sehemu inayozalisha zaidi.
2. Unaweza kutabiri ongezeko la faida kwenye biashara yako kama kuna visababishi vinavyoongeza mauzo kama matangazo (masoko) na kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara yako.
3. Unaweza kutabiri mahusiano yako kudumu kama utaweka mazingira ya kila upande kufaidika na kila mtu kuishi upendo katika mahusiano hayo.
4. Unaweza kutabiri utajiri wa afya kama kutakuwa na visababishi vya afya kama chakula bora, mazoezi ya mwili na muda wa kutosha wa kupumzika.
Anza leo kutabiri mafanikio ya maeneo hayo hapo juu ya maisha yako huku ukiendelea kuweka visababishi vya mafanikio hayo unayoyatabiri. Kwa kufanya hivyo utakuwa mtabiri mzuri ambaye hata watu wengine watapenda uwatabirie maisha yao.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz