Njia Ya Uhakika Ya Kuvikabili vizuizi Vya Safari Ya Mafanikio Yako


Categories :



Katikati ya mafanikio wanayoyatamani watu wengi umesimama ukuta ambao unawazuia wengi kupata vile wanavyovitaka. Huu ni ukuta ambao umefanya watu wachache tu waweze kupata mafanikio makubwa katika maisha yao.

Ukuta unaosimama katikati ya malengo na matokeo ya mafanikio ni vizuizi au changamoto mbalimbali zinazokabili mipango ya watu kupata matokeo wanayokusudia. Watu wengi wamekata tamaa baada ya kuviona vizuizi hivi. Watu wengi wameishia kuwa watu wa kawaida baada ya kukutana na vizuizi hivi.

Lakini kwa sababu watu wengine hata kama wachache wameweza kufanikiwa kuvikabili vizuizi vikubwa vya mafanikio makubwa, hii ina maana kuwa hata wewe unaweza kupata mafanikio hayo licha ya changamoto hizo. Njia mojawapo ya uhakika ya kupata mafanikio makubwa licha ya changamoto unazozikabili ni kuchukulia vizuizi hivyo kama sehemu ya njia ya kupata mafanikio na si kuvitenga.


Hakuna mafanikio ambayo yamepatikana kama mteremko, bali ni kwa kupanda milima na kuingia kwenye makorongo pia. Barabara ya kufikia mafanikio yako haijawahi kuwa tambarare hata siku moja. Kosa mojawapo ambalo watu wengi wamelifanya na limewagharimu kutopata matokeo wanayoyataka ni kuona kuwa vizuizi au changamoto zinastahili kuwa kwenye njia yake na sio kwenye njia ya mipango yao ya kupata mafanikio.

Kwa kufikiri kuwa vizuizi vilitakiwa viwe kwenye njia nyingine na sio kwenye njia ya kufikia mafanikio yao, wameshindwa kuvikabili vizuizi hivyo na kuvishinda pale ambapo wamekuwa wakikutana navyo. Hii ndiyo imekuwa sababu moja wapo ya kukata tamaa. Hii imekuwa ndiyo sababu ya kutojiandaa. Hii ndiyo imesababisha maanguko makubwa.

Umuhimu wa kuchukulia vizuizi kama sehemu ha njia ya mafanikio;


Vizuizi vitatabiriwa kwenye mipango. Ukitambua kuwa vizuizi ni sehemu ya njia ya kufikia mafanikio, lazima utavifikiria wakati wa mipango yako. Kuna usemi unasema kumjua adui ni sehemu kubwa sana ya kumshinda. Kama ukifahamu kizuizi unachoweza kukutana nacho wakati wa safari yako, utakiwekea jawabu la kukikabili na inakuwa rahisi kukishinda na kuendelea na safari.

Kukusaidia usikate tamaa. Kama ukitambua au kutabiri na kisha kujiandaa kwa kizuizi utakachokutana kwenye njia ya mafanikio yako hutashituka pale utakapokutana nacho. Hii inakupa nafasi ya kuendelea na safari na si kukata tamaa.

Utajifunza kutokana. Moja ya faida kubwa ya changamoto au vizuizi vya mafanikio ni kuwa darasa ambalo unaweza kujifunza. Kwa mfano kama kizuizi ulichokutana nacho ni kushindwa, kama umefanikiwa kuchukulia kushindwa kama sehemu ya safari ya kufikia mafanikio yako, utaangalia upande mwingine wa shilingi wa nini unaweza ukajifunza kutoka kwenye kushindwa kwako. Kwa kufanya hivyo utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya kitu hicho kwa ubora pale utakapokuwa unakirudia.

Ndugu! Kwenye safari ya mafanikio yako tambua kuwa utakutana na vizuizi ambavyo vimewarudisha nyuma watu wengi, lakini naomba uwe sehemu ya watu wale wachache waliofanikiwa kupata mafanikio makubwa licha ya changamoto hizo. Kwenye kila mpango wako wa kufikia malengo yako amini kuwa kuna vizuizi vinavyoweza kusimama katikati ya safari yako. Lakini kwa namna yoyote ile usikubali kuzuiwa na hivyo bali ona kama sehemu ya njia ya safari yako na safari navyo mpaka mwisho wa safari yako.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *