Hii Ni Siri Ambayo Hujawahi Huifahamu. Kwa Nini Ulizaliwa Ukiwa Umevikunja Vidole?


Categories :



Ulipokuwa unazaliwa ulivikunja vidole vyako vya mkono kutengeneza ngumi. Namna ulivyovikunja ni sawa na pale unapokuwa umeshikilia kitu kwa umakini mkubwa ili kisianguke.

Hivyo ndivyo na wewe ulivyoifanya mikono yako. Lakini swali kubwa ambalo utajiuliza ni kuwa muda huo ndiyo ulikuwa umetoka tu tumboni mwa mama yako, ulikuwa umeshikilia nini mikononi mwako? Kitu gani ulitaka kisidondoke? Tulipojaribu kuvikunjua vidole vyako, hatukuona chochote ukiwa umekishikilia, lakini tulivyoachia vidole uliendelea kuvikunja mpaka baada ya majuma kadhaa.

Unaweza kuielezea kisayansi, lakini mimi nitaenda kukwambia siri kubwa ambayo inawezekana ulikuwa huifahamu maana ya jambo hili ni itakusaidia sana kufungua ufahamu wako na kufanya makubwa kwa kulitambua hili tu.


Licha sisi tulikuwa hatukuoni ulichoshikilia, lakini wewe ulionyesha ishara kuwa kuna kitu ulichokishikilia tangu kuzaliwa kwako. Kwa sababu kila mtoto huzaliwa hivyo hii ina maanisha kuwa kila mtu huzaliwa na hii ishara hii muhimu na hakuna anaye kuja mikono mitupu.

Ndugu! Mikono yako ilishikilia zawadi kwa ajili ya dunia. Ulikuja duniani ukiwa tayari una kitu mikononi mwako kwa ajili ya dunia. Unatarajiwa uitoe zawadi hiyo katika kipindi chako cha uhai wako.

Ng’ombe alikuja na zawadi ya maziwa na nyama. Kuku alikuja na zawadi ya mayai. Nyuki walikuja na zawadi ya asali. Mwembe ulikuja na zawadi ya maembe. Kadhalika na wewe ulikuja na kitu chenye thamani ya kipekee. Ndani yako kuna kitu cha kipee ambacho unaweza ukakifanya na kikatoa thamani ya kipekee duniani na dunia ikastaajabu na kufurahia. Nini ulikishikilia na bado kipo ndani yako?

Kuna mtazamo ambao umeubeba akilini mwako unaokufanya usiipe dunia zawadi hiyo. Mtazamo huo ni hasi wa kuona kuna watu fulani tu wenye uwezo wa kufanya vitu vya thamani hapa duniani. Wakati ukiwapa upekee huo, wewe umejiona ni wa kawaida na unastahili kuwa na maisha ya kawaida. Kwa sababu akili yako imeamini hivyo, kweli umekuwa wa kawaida kama ulivyotaka. Ndiyo maana licha ya kufanikiwa kufanya baadhi ya vitu lakini hakuna cha ajabu kilichokushangaza au kuishangaza dunia.

Leo ni siku maalumu kwako ya kukumbuka ile ishara uliyoitoa wakati unazaliwa. Kuna kitu umekishikilia ndani yako. Hata kama hujakitoa haimaanishi kuwa huna. Kipo ndani yako, kaa chini na tafakari ni kitu gani unaona hakipo sawa na unaweza kukibadilisha? Kitu unaona unaweza kukifanya kwa ubora na urahisi kuliko watu wengine? Huko ndiko zawadi yako ilikojificha. Anza kufanya taratibu huku ukiendelea kukua na kuijaza dunia kwa thamani hiyo.

Wakati wa kuitoa zawadi hiyo ni sasa. Kama bado upo hai, una nafasi ya kuipa dunia zawadi hiyo. Usikubali kufa nayo. Thamani yako itaipa dunia utajiri, usikubali uzikwe na zawadi yako na kuongeza utajiri wa makaburi.

Zawadi yako ni deni ambalo dunia inakudai na hakuna mtu mwingine wa kukulipia kwa niaba. Hivyo usipotia zawadi hii ungali hai dunia itaendelea kukudai. Kama unaishi na kufurahia maisha yako duniani, tambua kuwa kuna watu waliozitoa zawadi zao. Na wewe ni wakati wa kuitoa ya kwako sasa. Kunjua vidole vyako sasa na uiachie zawadi hiyo iwe faida kwa dunia.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *