Huu Ndiyo Ufunguo Wa Kupata Siri Za Dunia Hii.


Categories :

Moja kati ya sababu kubwa ya watu wa dunia hii kuhangaika na kukosa furaha ni kutoielewa dunia, yaani watu wake na vitu vingi vilivyomo. Imekuwa ngumu kumuelewa mtu alivyo na kuwa ana nini ndani yake chenye thamani.

Ni mara ngapi umeishi na mtu kwa muda mrefu bila kugundua  kuwa alikuwa anaweza kufanya kitu fulani, ana kitu fulani ambacho ulikuwa unauhitaji nacho? Mara ngapi umehangaika ni biashara gani unaweza kuifanya na ukaona kama mawazo yote ya biashara yalishachukuliwa na watu wengine lakini baada ya muda mfupi mtu anaanzisha biashara ambayo itakushangaza ni kwa nini wewe hukufiria hivyo awali?

Licha ya dunia kuwa na kila kitu katika utele lakini imekuwa ni vigumu kupata utele huo, unajiuliza ni kwa nini. Kuna siri ambayo itakuwa inajificha ambayo itakusaidia kuwafahamu watu zaidi na vitu vingi vizuri vya dunia hii. Siri hiyo ni kutaka kuelewa kwanza kabla ya kueleweka.

Ukikutana na mtu nini kinakuwa kipaumbele chako? Je ni yeye akufahamu wewe ni nani au wewe kumfahamu yeye ni nani na ana nini ndani yake? Mara nyingi mtu amekuwa mstari wa mbele kujitambulisha yeye kuliko kuwafahamu watu wengine.

Siri hii ya kutaka kuelewa kwanza kabla ya kueleweka ni ufunguo wa kufahamu ni biashara gani unaweza kuifanya na ikapata wateja kirahisi. Watu wengi wanapoanzisha biashara wamekuwa wakijitanguliza wao kwanza kabla ya watu wengine ambao watakuwa wateja wake. Watu wengi huanzisha biashara kwa kujifikiria wao kwanza kiundani kabla ya watu ambao wanataka kuwauzia huduma au bidhaa. Hii ndiyo iliyochangia biashara nyingi kuwa na changamoto kubwa . Kumbe kabla ya kujifikiria wewe kwanza kuhusu faida yako, huna budi kumfikiria mteja wako ni tatizo gani analo na ni kwa kiasi gani biashara yako itatatua tatizo alilonalo.

Kwa ajili ya kutaka kueleweka kwanza kabla ya kuelewa umekuwa ukiongea sana kuliko kusikiliza. Kwa kutaka kuongea sana kuliko kusikiliza huwapi nafasi watu unaokutana nao waongee na uelewe nini walichonacho. Kila mtu ana kitu cha thamani ndani yake unachoweza kukipata baada ya kumsikiliza kwa makini na kumuelewa. Wape watu nafasi waongee utashangaa utakavyopata thamani kubwa ambayo hukutarajia.

Kwa kutotaka kuelewa kabla ya kueleweka hujaweza kutambua thamani ya mtu wa karibu yako kwenye mahusiano. Wapo watu walioachana na wenza wao kwa kujua hawana thamani kwa sababu tu ya kutanguliza kueleweka badala ya kuelewa. Weka kipaumbele cha kutaka kumuelewa mtu wako wa karibu kuliko kutumia muda mwingi kueleweka. Ukifanya hivyo utaepuka hasara ya kuiona thamani ya mtu baada ya kuachana naye.

Ndugu! Dunia ina thamani kubwa sana ambayo ingeweza kukupa kitu chochote unachokitoka kutoka kwa watu na mazingira yanayokuzunguka. Lakini umeshindwa kupata kwa sababu ya kutoweka kipaumbele cha kuelewa na badala yake umeweka nguvu kubwa ya dunia ikuelewe wewe ni nani. Kuanzia sasa kazi yako kubwa iwe kuelewa kiundani kitu chochote au mtu yoyote ili kupata thamani yake halisi. Kazi ya kueleweka sio yako bali ya wale wanaokuzunguka, watu watakuelewa tu wewe tumia muda mwingi kuelewa mambo.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *