Tengeneza Nguvu Hii Kubwa Ya Mnyororo Kwenye Maisha Yako.


Categories :


Mnyororo huundwa na vipande vidogo vidogo vya chuma. Mnyororo una matumizi mbalimbali kama ulinzi (kufungia mbwa na mageti), kuvutia mashine kama vile magari, trekta nk.

Licha ya mnyororo kuhitaji vipande vidogo vidogo ili kukamilika, una sifa ambazo unaweza kuzitumia na kuamsha nguvu kubwa za kukupa mafanikio makubwa maishani mwako. Zifuatazo ni sifa zinazoupa nguvu mnyororo ambazo unaweza kuzitumia kuyapa maisha yako nguvu.

1. Vipande vidogo vidogo ndivyo vinavyotengeneza mnyororo.
Vipande vinavyotengeneza mnyororo ni lazima viungane kimoja baada ya kingine bila kuachana. Ikitokea kipande kikaachie kingine, mnyororo huo hukatika na kutengeneza vipande viwili ambavyo vinategemeana na hivyo kupunguza ukubwa wa mnyororo huo.

Hii ina maana gani maishani mwako? Mafanikio ya maisha yako hayaoti mara moja kama uyoga, bali ni mkusanyiko wa mafanikio madogo madogo kutokana na jitihada ndogondogo za kila siku. Hivyo hakikisha unazalisha mafanikio hayo madogo kila siku bila kudharau.


2. Ukubwa wa mnyororo hutegemea idadi ya vipande vilivyoungana. Kadri vipande vingi vinavyozidi kuungana ndivyo mnyororo unavyozidi kuwa mrefu.

Hata kama unazalisha matokeo mdogo madogo kila siku, lakini hakikisha unazalisha mara nyingi ili uweze kupata mafanikio makubwa zaidi.

3. Uimara wa mnyororo unategemea uimara wa kipande kimoja kimoja
. Kadri vipande vilivyoungana vinavyokuwa vinene na imara ndivyo vinavyozidi kutengeneza mnyororo imara zaidi.

Uimara wa mafanikio yako, utategemea ukubwa wa matokeo ya kila siku. Ili uweze kupata matokeo makubwa na imara huna budi kuhakikisha kuwa unajenga mfumo wa kuwa na mafanikio imara na makubwa yanayojirudia rudia.

4. Mnyororo husafirisha nguvu kutoka kwenye mashine moja kwenda nyingine. Mnyororo unapounganisha mashine moja inayozalisha nguvu kwenye ile nyingine isiyozalisha nguvu, hata ile isiyozalisha nguvu huanza kutembea.

Tumia tabia hii ya mnyororo kuhakikisha mafanikio unayoyapata yanasaidia kuendesha sehemu nyingine ya maisha iliyolala. Kwa mfano kwenye kipato kidogo unachokipata kutoka kwenye ajira hakikisha unaweka akiba ambayo baada ya kuwa kubwa, itumike kufufua au kuanzisha biashara mpya.

5. Mnyororo ni mnyumbulifu. Mnyororo kutengenezwa kwa vipande vingi na kuwa mrefu, lakini unaweza kukunjwa na ukawa mdogo, unaweza kupindishwa kadri unavyotaka ili kutimiza kazi yake.

Hivi ndivyo unavyotakiwa kuwa maishani mwako, utakutana na hali mbalimbali za kukukwamisha usisonge mbele, wewe hakikisha unakabiliana na hali hizo kwa kutakiwa kubadili mtazamo tu mara nyingine na kusonga mbele.

Hizi ni tabia za mnyororo zinazoufanya uwe na nguvu kubwa na kuwa na matumizi muhimu maishani. Unaweza kuzitumia tabia hizi kuamsha nguvu kubwa ya mafanikio katika maisha yako
1. Hakikisha kila siku kuna mafanikio unayozalisha ambayo utayaunganisha na kesho
2. Ukitaka kukua zaidi ongeza ukubwa wa matokeo ya siku
3. Badilika pale inapolazimu, mbinu moja ikigoma badili nyingine, lakini usibadili malengo yako sahihi
4. Tumia mafanikio madogo uliyonayo kuzalisha makubwa zaidi.

Kila la kheri.


Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *