Usikose Muda Wa Kunoa Shoka Kabla Hujaanza Kukata Mti.


Categories :

Aliyewahi kuwa Rais wa Marekani Abraham Lincoln aliwahi kunukuliwa akisema “Give me six hours to chop down a tree and I will spend the first four sharpening the axe” ikiwa na tafsiri isiyo rasmi kuwa akipewa masaa sita ya kukata mti basi atatumia masaa manne ya kwanza kunoa shoka.

Unaweza kumshangaa na kujiuliza kwa nini atumie masaa mengi hivyo kukata mti angali ana masaa sita tu? Kwa asitumie muda mwinge kwenye kazi ya msingi ya kuangusha mti badala yake kutumia zaidi ya 60% ya muda wake kunoa shoka? Je haogopi kushindwa?

Kitu alichokisema atakifanya Lincoln kimekuwa kinapuuziwa na kutofuatwa na watu wengi wanaotafuta mafanikio. Baada ya kutambua kuwa mafanikio yao watayapata baada ya kuangusha miti, wamekuwa wakichukua shoka na kuanza kukata mti bila kujali ubutu wa shoka hilo. Na kwa sababu hiyo wengi wameshituka masaa sita yakiisha bila ya kuwa na dalali zozote za mti kuanguka. Hiki ni kitu cha kwanza kufanya ili uweze kupiga hatua; tambua hitaji la msingi la wewe kufanikiwa kwa kufanya maandalizi sahihi ya awali.


Kutambua hitaji la msingi ni kufanya maandalizi kabla ya ya kuchukua hatua. Unahitaji kujiuliza maswali ya msingi ya nini unahitaji kufanya uli uweze kufanikiwa katika mpango wako. Hii itakusaidia kufanya kitu sahihi kwa namna sahihi na wakati sahihi. Ukifanya hivyo utaimaliza siku yako ukiwa umechoka kwa faida baada ya kuwa na ufanisi na matokeo makubwa.

Kutambua kitu gani ukifanye na kwa namna gani ili kilete matokeo makubwa ni kutambua umuhimu wa kunoa shoka lako ili kabla ya kuuvamia mti. Hii itakusaidia kukata mti huo kwa muda mfupi na kwa ufanisi kuliko shoka hilo lingekuwa butu. Hivi ndivyo unavyoweza kunoa shoka katika maisha yako na kufanikiwa kupata mafanikio makubwa;

Wekeza kwenye maarifa. Kwa namna yoyote huwezi kutenganisha mafanikio yako na maarifa. Maarifa ndiyo dira itakayokuwa unakuongoza kipi sahihi cha kufanya na ipi namna bora ya kufanya. Kupitia maarifa utapata nafasi ya kwa kujua watu waliopita njia ambayo wewe unatarajia kupita na vikwazo walivyopitia na jinsi walivyovikabili na hivyo rahisi na wewe kuvikabili kirahisi. Soma vitabu vinavyohusiana na kile unachofanya, hudhuria semina na kupata miongozo sahihi. Hii ni kunoa shoka kabla ya kukata mti.

Ipangilie siku. Kabla hujatoka na kuanza kufanya chochote katika siku husika, hakikisha umeipangilia siku yako, kujua nini unaweza kufanya kwenye muda fulani. Kujua nini ufanye kwenye muda fulani na kukaa kwenye mpangilio huo ni kunoa shoka la muda wako ili kupata mafanikio yanayoeleweka kwenye kila muda unaotoweka. Kutopangilia muda wako ni kufanya muda wako kuwa butu na hivyo kuwa na uzalishaji mdogo licha ya muda mwingi utakaotumia.

Pata muda wa kupumzika. Hakuna kitu chochote unachoweza kufanya bila ya kutumia akili. Ili akili yako iweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa unahitaji kupumzika baada ya kuchoka. Kabla hujaianza siku yako hakikisha umepata muda wa kupumzika. Kupumzisha akili ni kuinoa ili iweze kufikiri kwa umakini na kuchukua vitendo sahihi. Noa akili yako kwa kulala kwa wastani wa masaa 7 kila siku.


Usikimbilie kumuuzia bidhaa mteja bali jenga mahusiano mazuri naye. Ili biashara yako isimame na ikue inahitaji wateja wa kudumu. Ili upate wateja wa kudumu lazima unoe shoka kwa kuhakikisha unaimarisha mahusiano mazuri na mteja wako ili anunue leo la kesho. Usikimbilie kumuuzia mteja bali anza kwa kitu hiki unachokiona ni kidogo cha kuimarisha mahusiano yako mteja ili ajisikie mfalme.

Ndugu ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka huna budi kuhakikisha unanoa shoka lako kabla hujaweka jitihada kwenye malengo yako. Hii itakusaidia kuwa na ufanisi mkubwa katika utendaji wako. Nini unaweza kukiandaa ili siku yako iwe ya mafanikio makubwa.


Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *