Furaha Yako Ya Kweli Hailetwi Na Ndege.
“Rangi ya nje ya chupa ya maji haiwezi kubadili rangi ya maji ndani yake”
Kwa kawaida maji masafi hayana rangi. Hivyo mwonekano wa maji yakiwekwa kwenye chupa hutegemea rangi ya chupa hiyo. Yakiwekwa kwenye chupa nyekundu, nayo yataonekana mekundu, yakiwekwa kwenye chupa ya bluu, kadhalika nayo yataonekana ya bluu.
Licha ya rangi ambazo zitabeba maji hayo, lakini maji hayo yataendelea kutokuwa na rangi yoyote. Rangi za chupa hazitaathiri rangi ya maji. Hivyo kama unataka maji yawe na rangi fulani huna budi kuiweka rangi hiyo wewe mwenyewe. Rangi ya chupa ya maji kamwe haiwezi kuyapa maji rangi.
Lakini licha ya rangi ya chupa kutokuwa na uwezo ya kuyapa maji rangi, binadamu wengi ndivyo ambavyo wanafanya katika maisha yao. Utakuwa unajiuliza ni kwa namna gani wamekuwa wakifanya hivyo? Wamekuwa wakifanya hivyo kwa kukaa na kusubiri jambo fulani, mtu fulani, muda fulani ndivyo vitakavyowapa furaha ya kudumu katika maisha yao.
Ni mara ngapi umekaa na kujiambia nikipata mafanikio haya nitafurahi sana, lakini ulipoyapata hukupata furaha na ulipata ikayeyuka ndani ya muda mfupi tu. Ni mara ngapi umeona unastahili kutokufurahia maisha mpaka pale changamoto inayokukabili iishe? Bahati mbaya changamoto hiyo ilipoisha changamoto nyingine ikaibuka, hivyo umekuwa ukiendelea kuisubiria furaha bila mafanikio kwa sababu changamoto za dunia haziishi.
Kuna muda umekosa furaha kwa kujaribu kujilinganisha na watu wengine. Ulipoyaona mafanikio ya watu wengine ukajidhani wao wamebahatika kuliko wewe. Jambo hili limekupa huzuni kwani kila wakati unajiona umepunjwa ingali una uwezo wa pekee ndani yako ambao haupo kwa mtu mwingine yoyote.
Ndugu! Chanzo kikuu cha furaha yako kipo ndani yako. Hakuna mtu mwingine anayeweza kuruhusu furaha yako isipokuwa wewe. Kama ulivyo na uhuru wa kuamua uudhike au usiudhike baada ya baada ya m5u kutokukutendea haki, ndivyo ulivyo na ruhusa ya kuamua uwe na furaha au usiwe nayo. Mazingira ya nje hayawezi kukupa furaha ya kudumu kama ndani mwako hutaamua kuzalisha furaha.
Kama ilivyo kwenye maji, ni rangi yake tu iliyokuwa nayo kabla ya kuwekwa kwenye chupa ndiyo itakayoendelea kuwepo hata kama itawekwa kwenye chupa ya rangi tofauti, ndivyo itakavyokuwa ndani yako kwa furaha yako kukutegemea wewe na sio mazingira.
Unasubiri nini kuwa na furaha maishani mwako? Ahadi gani uliyopewa unasubiri itimizwe ndipo uwe na furaha? Changamoto gani unasubiri iishe ndipo uishi kwa furaha? Kigezo cha kwanza kabisa cha kuwa na furaha ni uhai wako. Kama upo hai una kila sababu ya kuendelea kufurahia maisha. Kisha furahia mchakato unaouchukua kwa ajili ya mafanikio yako.
Furahi kwa sababu unapumua, furahia mchakato wa mafanikio yako na sio matukio; usisubiri mazingira yakuruhusu ufurahi, iishi furaha hiyo ndani yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz