Msimamo Unaojenga Mafanikio Ya Kudumu.
“Jani la mti lililoanguka kwenye mto, hutembezwa kwa kadri ya uelekeo wa maji. Linaweza kubamizwa kushoto, kulia na kusimamishwa popote”
Dunia ina mipango mingi na hutafuta watu ambao hawana mipango na kuwapa. Bahati mbaya haikupatii mpango mmoja na kusubiri uimalize, bali huendelea kumpa mipango kila siku hata pale ambapo mpango wa kwanza hujautimiza na hata kukupa faida. Ndiyo maana ukijaribu kufikiri vitu ambavyo umeshavifanyia kazi mpaka sasa ni vingi sana. Vingi ulivianza na hukuvimaliza ila kuishi njiani.
Ukijaribu kulinganisha , hakuna uwiano wa vitu ambavyo umeshavifanya na matokeo uliyoyapata. Umefanya vitu vingi lakini umepata kiduchu. Umetembea sana lakini hujaenda mbali sana na safari yako. Umechoka sana lakini ukiangalia ulichokifanya hakikufariji ukilinganisha nguvu ulizoziweka.
Umekuwa ukikutana na fursa kila siku, na kuona fursa mpya inaweza kukulipa kuliko kile unachokifanya sasa. Ulipoacha na kwenda kwenye fursa nyingine , ikajitokeza hivyo ukiacha ya pili na kuiendea mpya. Hayo ndiyo yamekuwa maisha yako ya kugusa gusa kila wakati. Hii imetokea kwa sababu hakuna kitu cha kusimamia. Kitu gani umeamua kukisimamia maishani mwako?
Kumekuwa na utitiri wa biashara, kila siku kuna fursa mpya za biashara ambapo maelezo yake huonekana ni nzuri kuliko zile ambazo unazifanya. Fursa mpya huonekana inaweza kukupa utajiri kirahisi na kwa haraka zaidi kuliko biashara unayofanya sasa. Kwa sababu biashara yako ya sasa ipo kwenye changamoto, umekuwa ukiamini kuwa ni kweli biashara hizo zitakupa utajiri wa haraka. Lakini ukiingia kwenye biashara hiyo utaona kuwa mambo siyo sawa na vile ulivyokuwa unaambiwa au unadhani, unashangaa imekuwaje! Lakini wakati unaendelea kushangaa fursa nyingine mpya inatokea ambayo kwa hiyo unaona utafuta machungu uliyoyapata, lakini inakuwa tofauti. Unasimamia biashara gani?
Unaamuka asubuhi ukiwa na shauku kubwa ya kwenda kufanya mambo yako muhimu ya kukupa mafanikio. Unafika kazini unakutana na mambo mengine tofauti na yale uliyoyapanga, kwa mfano unakutana na mtu anataka muanze kuzungumzia mtu fulani, au unafungua kompyuta unakutana na habari inayokuvutia kuisoma, je unavifanya hivyo vitu au la? Je umetengeneza nidhamu gani ya kusema hapana kwenye mambo mengi yaliyo kinyume na mipango yako? Nidhamu gani unaisimamia?
Ili kuepukana na kelele nyingi za dunia huna budi kutafuta kitu kimoja ambacho unafikiri ukikifanya hicho na kufanikiwa, maisha yako yatastawi sana na kufikia mafanikio makubwa sana maishani mwako. Je ni biashara gani ambayo unaipenda kuifanya ukikaa humu na kuikiza itakupa matokeo mazuri? Hiyo ndiyo biashara ya kukomaa nayo.
Umekuwa unahangaika na ndoto ndiyo kila siku ambazo hazijakupatia matokeo makubwa ya kuridhisha. Kwa sababu unapoteza muda na nguvu zako. Mahitaji ya ndoto kubwa na ndoto ndogo hayatofautiani. Huoni sasa ni wakati wa kutengeneza ndoto kubwa na kuisimamia mpaka itimie.
Baada ya kuchagua ni unakitaka, tarajia kukutana na fursa nyingine ambazo zitakutamanisha uziendee, usikubali wewe komaa na kile ulichokichagua. Bobea kwenye eneo hilo. Kubobea ni kutawala kiasi kwamba kama ni muuzaji wa bidhaa fulani na mtu akifikiri bidhaa hiyo, basi jina lako liwe la kwanza. Umeamua kubobea kwenye nini?
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz