Hii Ndiyo Njia Pekee Ya Kuanza Kupata Matokeo…
Ni muda gani umepita tangu useme unataka kuanzisha biashara ili kuongeza kipato chako? Ni muda gani umepita tangu useme unataka kuacha tabia mbaya ambayo hata wewe mwenyewe inakuudhi? Ni muda gani umepita tangu uanze kusema utaanza kuthibiti vyakula unavyokula na kufanya mazoezi ili kupunguza uzito hatari?
Naamini una majibu ya maswali hayo hapo juu na mengine mengi ambayo umekuwa ukiongea mara kwa mara na kwa muda mrefu. Lakini licha ya kuyaongea kwa muda mrefu, licha ya kutamani upate matokeo hayo lakini ni moyo tu umeendelea kutamani bila matokeo. Nikihakikishie kuwa upo kwenye kundi la lenye watu wengi sana hapa duniani. Hili ni kundi maarufu wa kuongea na sio kutenda.
Njia pekee ya kuanza kupata matokeo ni kuacha kuongea kisha kuanza kutenda. Maneno peke yake hayawezi kukupa matokeo mpaka ufanye vitendo. Ndiyo maana licha ya kuongea sana kile unachokitaka, hujapata matokeo kwa sababu baada ya kuongea hukuchukua hatua inayofuata ya kutenda. Ni wakati sasa wa kunyamaza na kufanya kuacha vitendo viongee matokeo.
Nyamaza na tenda sasa. Kuongea ni rahisi, kutenda ni kazi ngumu, ndiyo maana watu wengi wanaishia kuongea tu huku wachache tu wakifanikiwa kutenda na kupata matokeo. Ni wakati sasa wa kufanya mabadiliko ya kweli. Nyamaza na acha vitendo viongee.
Toka kwa wengi hamia kwa wachache. Kundi la wasemaji tu lina watu wengi sana. Hili ni kundi linaloamini kuwa mambo yanaweza kutokea yenyewe. Watu hawa wanaamini kuwa kuna siku mambo yatakuwa mazuri yenyewe. Lakini wakashangaa miaka inaenda lakini hakuna matokeo. Licha ya nguvu kubwa jamii ambayo itakung’ang’ania uendelee kuwa kwenye kundi hili la waongeaji kuliko kutenda, huna budi kuweka nguvu kubwa kutoka na kwenda kwenye kundi la watu tofauti wanaongea kidogo na kutenda zaidi.
Weka mpango wako kwenye maandishi. Wazo lolote ambalo halijaandikwa ni sawa na matamanio tu. Una mambo mengi sana unayoyasikia na kuyawaza, ni rahisi sana kupunguza uhalisia wa wazo hilo kadri unavyokaa muda mrefu bila kulifanyia kazi. Kuonyesha kuwa upo makini na hicho unachokisema, fanya hatua hii muhimu ya kuandika yale unayoyataka kufanyia kazi. Andika unachotaka kukifanya.
Anza leo. Unaweza ukapanga kuwa utaanza kufanya, je ni lini? Muda mzuri wa kuanza ni leo. Hakuna muda mwingine ambao una uhakika wa kuanza zaidi ya leo tena sasa. Kamwe usianze wala kuendelea kuahirisha mambo, anza kufanya leo.
Je unahitaji matokeo ambayo yatakupa mafanikio katika maisha yako? Huhitaji kwenda kwa mganga, ni jambo moja tu linahitajika; acha kuongea kisha weka vitendo kwenye vile unavyoviongea. Kuanza kupata matokeo ni mwanzo wa kuyapata mafanikio yako; anza leo.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz