Hii Ni Dalili Ya Utajiri Kukukaribia
‘’Hata kama nta zitapatikana kwa shida, lakini nyuki wataendelea kuzitafuta kwa udi na uvumba ili watengeneze asali ambayo inahitajika na binadamu. Nyuki hufurahi sana akishakamisha jambo hilo’’
Licha ya utajiri kuwa ndoto ya watu wengi, lakini watu wengi bado ni masikini. Watu wamekuwa wakikinga mikono kusubiria utajiri huo, wakiamini kuna siku watapata utajiri huo. Kuna dalili ambayo unaweza kuiona ikiashiria kuwa utakuwa tajiri hata kabla ya kuupata utajiri huo. Dalili hiyo ni kiasi cha thamani unachotoa kwa watu wengine. Kigezo kikuu cha kupata utajiri wako ni kutoa na baadaye kupokea.
Hivyo kama unataka kuwa tajiri kwenye eneo lolote la maisha yako, swali la kwanza unalotakiwa kujiuliza ni kitu gani unakitoa kwa watu wengine. Ukitaka utajiri w amali jiulize, ni thamani gani nitatoa kwa watu wengine? ukitaka furaha na amani tele, jiulize ni thamani gani nitaitoa kwa watu wengine ili wafurahi? Tumeumbwa ili tutoe tulivyo navyo na viwe msaada kwa watu wengine. Furaha na kuridhika kwa mwanadamu kupo kwenye kutoa na sio kupokea.
Maandiko matakatifu yanatukumbusha kheri wa kutoa kuliko kupokea. Matendo ya mitume 20:35 “Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea” Kutoa huambatana na kutumia uwezo wako kuliko kupokea. Thamani kubwa unayowapitia kwa watu ndiyo inayovuta vitu kuja kwako.
Kila kumbe ambacho kipo duniani kilikusudiwa kuleta thamani duniani. Na ni kwa kupitia njia ya kutoa tu mtu anajiika kuridhika. Kadri unavyozidi kutoa ndivyo unavyozidi kutumia uwezo wako. Na ili uendelee kutumia uwezo wako wa ndani huna budi kuongeza kiwango cha kutoa.
Kupokea hakujitaji nguvu, kwani utakaa na vitakuja tu. Huku kunakufanya ulale. Kulala kunakufanya usitumie uwezo wako na hivyo kuna nafasi ya kufa wakati uwezo wako hujautumia. Uliumbwa na uwezo na vipaji ndani yako. Vyote hivyo vina thamani kubwa sana kama vitatolewa hapa duniani. Lengo la hazina hiyo kubwa haikuwa kukaa nayo ndani yako. Bali kutoa ili watu wengine wafaidike.
Dunia inakuwa mahali pazuri pakuishi kwa watu kutumia uwezo wao mkubwa ulio ndani yao. Ukitoka duniani bila kutoa hazina hiyo, unakuwa umeipunja dunia. Pia itakuwa hasara kubwa kwani utazikwa na hazina hiyo na hakuna mtu mwingine anayeweza kutumia zaidi yako.
Unaweza kufikiri kutoa ni hasara. Hapana! Unapoitolea dunia kwa kutumia uwezo wako, unatengeneza thamani kwa watu. Rafiki yangu ni kupitia kutoa thamani kwa watu wengine kwa kutumia uwezo wako, ndipo unapoweza kupata chochote kutoka kwa wengine.
Kadri unavyotoa ndivyo unavyopokea. Ukitoa vikubwa unapokuwa vikubwa. Yaani kadri unavyotoa thamani kubwa kwa watu wengine ndivyo unavyo pata zaidi.
Kama bado upo hai, hakuna siku utasema uwezo wako umeisha. Kila siku una nafasi ya kufanya ambacho hujawahi kukifanya. Au kufika eneo ambalo hujawahi kufika. Au kufika hatua ambayo hujawahi kuifikia. Au kutumia kipaji ambacho bado hujakitumia.
Chukua hatua: Fikiri leo ni kitu gani ambacho unaweza kuipa dunia kwa kiwango kikubwa kiasi cha dunia kukurejeshea utajiri? Kitu hicho lazima kiendane na uwezo wako wa kipekee uliopo ndani yako. Hiki ni kitu ambacho unakipenda kukifanya na kwa urahisi kuliko watu wengine.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa Uwezo Wako Halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz