Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuepuka Foleni Ya Umasikini.
Licha ya jamii yetu kuwa na watu wengi sana, ni idadi ndogo sana ya watu ambao ni matajiri. Utajiri ninaoutaja hapa ni ule uhuru wa kifedha. Ni watu wachache sana ambao fedha siyo kikwazo katika maisha yao.
Idadi kubwa ya watu wengi wasio huru kifedha imetengeneza foleni kubwa. Foleni hiyo ni jitihada zinazofanyika na mtu kujinasua kwenye utumwa huo wa kifedha. Foleni hizo mara nyingi zimekuwa hazisogei. hivyo mara nyingine mtu kujikuta akitumia maisha yake yote kwenye foleni bila kufika kule ambako amekuwa akikutamani.
Lengo makala hii ni kukupa taarifa kuwa unaweza kuipita foleni hii na kuiona njia wazi ambayo utaenda kwa uhuru zaidi na kufikia utajiri wako. Ni watu wachache tu wanaoweza kuipitia njia hii, lakini wewe unaweza kuwa miongoni mwao. Njia hiyo ni kwenda maili zaidi kuliko watu wengine.
Chukulia foleni ya magari, hii hutokea kwa magari mengi yanapotembea kuelekea upande mmoja tena kwa kasi ndogo. Athari za foleni hii huwa ni kupoteza muda na kuchelewa kufika kwani utabaki umeganda sehemu moja. Hivi ndivyo inavyotokea pale unaamua kuiga wanachofanya watu wengine bila kujali kama ni chako au la. Ili uukimbie umakini ambao watu wengi wamejipanga kwa kufanya chochote kwa namna yoyote huna muda kufanya yafuatayo;
Fanya kitu tofauti. Badala ya kuendelea kuwa kama watu wengine waliopo kwenye foleni wewe jitofautishe ili uweze kuwa tofauti na kuivuka foleni. Badala ya wewe kuangana na watu ambao wapo kwenye foleni wakilalamika kuwa maisha ni magumu, basi wewe fanya tofauti, chukua wajibu kwenye kila jambo unalotaka ulipate.
Fanya kitu hicho hicho kwa utofauti. Mara nyingine si lazima ufanye kitu tofauti na kile ambacho kila mtu anafanya bali unaweza kitu hicho hicho lakini kwa utofauti. Kuna vitu amba yo kila mtu anaweza kukifanya na wote mkawa kwenye foleni wakifanya kwa namna ile ile na kupata matokeo ya kawaida. Lakini ili uepuke foleni hii na kupata utajiri huna budi kuhakikisha unajitofautisha na kufanya kwa ubora zaidi. Kuna watu wengi wanaofanya biashara na biashara nyingi zimekuwa zikifa au kusuasua basi wewe fanya kwa utofauti ukiijengea biashara mfumo huku ukiweka thamani kubwa na kuikuza.
Fanya kwa msimamo. Kumekuwa na foleni ya watu wengi wakifanya vitu kwa muda mfupi tu. Hawa ni watu wanaojaribisha mambo. Baada ya kuanza jambo, wakikutana na ugumu wanaacha. Wanaanza jambo, wakisika kuna fursa mapya wanaacha wanachokifanya na kuikimbilia fursa hiyo. Bahati mbaya wakifika huko wanaona mambo siyo sawa na vile walivyokuwa wanafikiri.
Wewe huna budi kuiepuka foleni hiyo kwa kuwa na msimamo. Ukianzisha jambo na kuwa na uhakika wa kuwa upo kwenye njia sahihi, wewe endelea kuweka nguvu na jitihada mpake upate matokeo. Utajiri huja kwa kuweka msimamo kwenye jambo moja au machache.
Ongezeka. Hakikisha unakua kila siku. Usikubali kila siku kubaki palepale. Weka mipango ya kujinyoosha zaidi. Kua kimaarifa kwenye eneo unalofanyia kazi. Baada ya kukamilisha lengo la sasa, panga kubwa zaidi. Usiunge foleni ya watu wanaodumaa kwa kufanya vitu kwa mazoea, miaka nenda wapo palepale.
Ndugu foleni ya umasikini inaweza kuepukika kwa kujitofautisha na wale mlionao kwenye foleni. Ili uweze kuiacha foleni hiyo, huna budi kwenda maili za ziada, ambako kuna ukinzani kidogo. Kufika huko, hakikisha unaacha mazoea, unachukua jukumu la maisha yako na kukua kila siku. Chagua jambo moja ambalo utalifanya kwa kujitofautisha na watu wengine. Lifanye hilo kwa viwango vya juu sana huku ukitoa thamani kubwa kwa wengine. Huko kutakuwa ni kwenda maili za ziada kufikia utajiri wako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz