Macho Yako Yanatazama Nini?
“Simba hakosi amani kwa sababu hajui urefu wa shingo ya twiga, bali jitihada zake huwa kuhakikisha twiga huyo anakuwa kitoweo”
Dunia ina mambo mengi, ina taarifa nyingi na vituko vingi. Kwa kuzingatia wingi wa mambo ya dunia huwezi kumaliza kuyaelewa.
Wingi wa mambo ambayo mtu anaweza kuyafanya umekuwa mwiba kwa watu wengi kutokufanya vitu vya msingi maishani mwao. Kwani ni rahisi sana kwa sasa mtu kukaa na kufikiria na kumjadili mtu mwingine kuliko maisha yake. Ni rahisi mtu kufahamu, uwezo, mafanikio, changamoto na malengo ya mtu mwingine kuliko kile alichonacho yeye na kukitumia.
Muda ni moja ya rasilimali muhimu sana katika kutengeneza mafanikio yako makubwa . Bahati mbaya ya rasilimali hii ni kuwa ukishaipoteza huwezi kuipata tena. Huwezi kuwa na maisha bila muda. Kwa kuzingatia hilo, usitumie muda wako kwa mambo ambayo hayana au yana mchango mdogo kwenye maisha yako.
Ili uweze kutumia muda wako vyema huna budi kujiuliza swali hili muhimu katika maisha yako. Unataka nini? Hili ni swali ambalo majibu yake yatagusa kila eneo la maisha yako; fedha, kazi/biashara, binafsi, mahusiano na afya pia. Ukishajua unataka nini, huko ndiko kwa kukutazama, kuwekeza na kujadili na si vinginevyo.
Unafanikiwa maishani mwako kwa kupata kile unachostahili kama utatumia muda wako, nguvu zako, umakini wako n.k. katika mambo machache yanayogusa maisha yako. Kutaka kupata mambo yote yanayoendelea dunia, ni kuchagua kupoteza yote. Waswahili husema miluzi mingi hupoteza mbwa.
Kama ambavyo simba hahangaiki kujua urefu wa twiga bali kujikita kwenye kuhakikisha kumkamata na kumla, ndivyo na wewe unavyotakiwa kujikita kwenye kuboresha maisha yako kwa kufanya vilivyo sahihi.
Chagua biashara moja kwanza. Moja ya njia ya uhakika ya kuingiza kipato cha kutosha na kufikia utajiri ni kuwa na biashara yenye faida na inayojiendesha. Biashara ya kukufikisha kwenye utajiri haioti kama uyoga, bali inahitaji muda, umakini na juhudi za muda mrefu. Chagua biashara moja ambayo kutoka kwenye vitu unavyovipenda kufanya kisha komaa na hiyo mpaka ikufikishe kwenye utajiri.
Chagua watu wachache lakini sahihi. Mafanikio yako yanategemea sana watu wanaokuzunguka. Je watu wanaokuzunguka wanatumia muda wao mwingi kufanya nini? Mafanikio yako ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka. Kwa sababu watu wengi kwenye jamii wanaridhika kuishi maisha ya kawaida, huna budi kuchagua watu hata wachache ambao watakuwa chachu kwako kuchukua hatua na kufikia kwenye mafanikio makubwa.
Chagua maeneo machache ya kubobea. Ni kitu gani wakikihitaji chaguo la kwanza au jina la kwanza linakuwa lako au taasisi yako? Chagua eneo moja ambalo utakuwa upo vizuri kupindukia ambako utawaacha washindani wako mbali sana. Huko ndiko kutakuwa chimbuko la wewe kupata mafanikio makubwa.
Ndugu! Huwezi kukimbizana na kila kitu kinachoendelea hapa duniani, hutaweza kwa sababu vipo vingi sana na muda wako hautoshi. Ili kuweza kufanya makubwa maishani mwako huna budi kuchagua kimoja au vichache ambavyo utavifanya kwa viwango vya juu sana kuliko watu wengine.
Chukua hatua: Tambua unataka binafsi uweje, uwe na utajiri wa sh?, mahusiano yako je? Wekeza huko kila ulichonacho ndani yako kupata unachokitaka na kustahili.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz