Hii Ndiyo Sumu Ya Kutopata Matokeo Unayotaka.


Categories :



Siku hizi nipo busy! sana kila wakati kuna kitu nafanya. Kazi zimekuwa nyingi sana naanza asubuhi sana na kumaliza usiku sana! Hizi ni baadhi ya kauli ambazo huwa zinatumiwa na watu wengi kuwasilisha ujumbe ni kwa namna gani wapo busy na maisha.

Wewe unaweza ukawa miongoni ukiyafanya haya au umekuwa shahidi wa watu wengi ambao wapo busy sana. Ni muda mrefu sana tangu umeanza kuwa busy ukiamini umefanya mengi. Nikupongeze kwa kuamua kuwa busy. Lakini nina swali moja kwako, una nini mkononi mwako kwa ajili ya jitihada ambazo umekuwa unazifanya? Je muda ulioutumia unalingana na kile ulichokipata? Je nguvu na muda uliouweka unalingana na kile ulichokipata?

Kwa watu wengi ambao wamekuwa wapo busy nguvu zao wanazowekeza zimekuwa tofauti na matokeo wanayoyapata. Matokeo yamekuwa kiduchu ukilinganisha na nguvu zinazotumika. Matokeo yamekuwa kidogo sana ukilinganisha na muda walioutumia. Sababu mojawapo ya matokeo haya ni kufanya chochote. Ukiamua kufanya chochote tegemea kupata matokeo yoyote na hasa kidogo.

Kufanya chochote ni kutokuwa na mpango wowote unaofanyia kazi. Na kwa sababu hiyo mtu huamua kufanya chochote kinachokuja mbele yake. Maana nyingine ya kufanya chochote ni kuwa na mpango wa kufanyia kazi lakini unashindwa kuufuata kama inavyotakiwa. Hii ni kukosa nidhamu kwenye yale uliyoyapanga. Kuwa tayari kufanya chochote kinachokuja mbele yako ndiko kulikofanya upate matokeo kigogo kwenye nguvu kubwa uliyoiweka.



Kanuni ya Pareto(80/20) inasema 80% ya matokeo unayoyapata yanatokana 20% ya kazi unazozifanya. Au 80% ya mali ulizonazo zimetokana na 20% ya tu ya vitu vyote ulivyovifanya au inamaanisha kuwa 80% ya utajiri wako umetokana na 20% tu ya biashara zako. Kumbe kanuni hii inatuonyesha kuwa hatustahili kufanya chochote bali vile ambavyo vina mchango mkubwa katika malengo uliyoyaweka.

Kuamua kufanya chochote kunatoa nafasi kubwa sana ya kufanya yale mambo yanayokamata 80% huku yakiwa na mchango wa 20% kwenye mafanikio yako. Badala ya kufanya chochote, sasa fanya kazi zilizopo kwenye 20% lakini zinazochangia 80% ya matokeo ya mafanikio unayoyapata. Hivi ndivyo unavyoweza kuachana na kufanya chochote kisha kuanza kufanya yale muhimu yatakayokupa matokeo yanayoendana na u’busy’ wako;

Tambua unataka nini. Unataka nini maishani mwako. Kwa nini uhangaike? Ili upate nini? Usikubali kuhangaika kwa chochote bali kwa kitu maalumu katika maisha yako. Nini unataka kipo ndani yako. Ndani yako kuna sauti yenye kiu ya kitu unachotaka kukipata. Kupitia sauti hiyo ndipo utatambua ni kitu gani unatakiwa kukifanya. Utatambua ni biashara gani unatakiwa kuifanya badala ya kuhangaika na biashara yoyote. Usihangaike na chochote bali kile unachokitaka toka ndani mwako.

Pangilia siku yako kwa kuweka vipaumbele.
Kazi zote zinafanyika kwenye siku. Hivyo mafanikio yako yanategemea kile anachokifanya kwenye siku. Ni yale matokeo madogo madogo unayoyapata kila siku. Hivyo hakikisha hufanyi kitu chochote bali vile vya muhimu kwenye siku yako. Weka vipaumbele wa vitu gani utavifanya kwanza kabla asubuhi ukiwa bado una nguvu.

Vumilia kupata matokeo. Watu wengine huanza kufanya chochote baada ya kukosa matokeo yale waliyoyategemea. Huona huko kunawachelewesha. Kama ni biashara haitoi faida aliyotarajia huona hii haifai na kuenda kuanzisha nyingine. Akianzisha mpya na kupata matokeo yaleyale ya biashara ya kwanza huacha tena kuanzisha nyingine. Ndugu huwezi kupata mafanikio makubwa kwa kutokaa kwenye jambo moja kwa muda mrefu na kubobea.

Tumia neno HAPANA. Moja ya sababu ya kubwa inayowafanya watu kufanya chochote ni kutokuwa na matumizi kabisa au kuwa na matumizi madogo ya neno hapana. Ukiwa tayari kufanya jambo lolote linalokuja mbele yako si rahisi kufanya mambo machache ambayo ni muhimu sana kwako yanayo. Anza kutumia neno hapana kwa yale ambayo hayakuwa kwenye ratiba yako na ambayo hayana mchango mkubwa kwako. Kwa kutumia neno hapana ataanza kupata muda mwingi wa kufanya yale muhimu kwa ajili ya mafanikio yako makubwa.

Ndugu! Huwezi kufikia mafanikio makubwa kwa kuamua kufanya chochote. Unahitaji kufanya yale yaliyo muhimu kwenye muda mwingi. Amka asubuhi na pangilia vizuri siku yako huku ukiweka vipaumbele vyako. Sema hapana kwa yale yasiyo muhimu katika mikakati yako.


Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *