Huyu Ndiye Mwalimu Mzuri Wa Maisha Yako.
“Mtu aliyekanyaga mwiba hutoa mguu wake kwa haraka ili kuweza kuokoka na maumivu yanayomkabili”
Watu wamekuwa hawapendi kusikia au kupata maumivu katika maisha yao. Wamekuwa wakifanya kila namna kuhakikisha wanayakwepa maumivu hayo. Kwa sababu ya maumivu watu wameogopa kutoka nje na kutembea wakitafuta kwa sababu ya kuogopa kukanyaga miiba yenye maumivu.
Kuzuia kupata maumivu imekuwa sababu mojawapo ya kutokutoka nje ya sanduku. Mtu hung’ang’ania kuendelea kubaki kwenye sanduku kwa kuendelea kufanya vitu alivyovizoea ambavyo haviwezi kumpa maumivu ili tu kuepuka maumivu.
Kama mtu anavyoweza kunyanyua mguu ili kuyakabili maumivu baada ya kukanyaga mwiba, ndivyo na wewe unavyoweza kupiga hatua kubwa zaidi kama kutakuwa na maumivu yatakayokuwa yanakukabili. Anza kutumia maumivu yafuatayo kama mwalimu katika maisha yako;
Maumivu ya kipato kidogo. Kipato kidogo kimekuwa changamoto kwa watu wengi. Lakini wengi wameendelea kuizoea hali hiyo kwa kuona wanastahili hali hiyo na kuwa tayari kuvumilia. Ili uweze kutoka katika hali ya umasikini au kipato kidogo lazima jambo hili ulitengenezee maumivu na uwe kutokuwa tayari wa kuvumilia maumivu hayo. Ukiupenda utajiri utauchukia umasikini kiasi cha kutokuwa tayari kuvumilia maumivu yake. Kwa maumivu hayo utakuja na mipango ya kuondoka na hali hiyo.
Maumivu ya malengo madogo. Unapata nini baada ya kuweka nguvu, umakini na muda wako kwa mambo unayoyafanya? Je matokeo yake yanaendana na nguvu unazoziweka? Sababu mojawapo ya kutokupata matokeo makubwa ni kuendelea kuishi malengo madogo na kuridhika nayo. Ili uweze kutengeneza maumivu ambayo hutaweza kuyavumilia, tambua kuwa nguvu, muda na umakini unaoutumia kwenye malengo au ndoto ndogo ndizo unazoziweza kufanya hivyo hivyo kwenye ndoto/malengo makubwa . Tumia maumivu ya habari hii sasa kuanza kupanga kufanya mambo makubwa.
Maumivu ya mauzo madogo. Lengo kuu la kwanza la biashara ni kutengeneza faida. Biashara haiqezi kutengeneza faida kama huuzi na unauza kidogo. Mauzo kidogo lazima kiwe maumivu makali ya mwiba kwenye biashara yako. Maumivu haya yakusukume kutafuta wateja watakaokuja kununua na kuongeza mauzo na faida. Usiridhike na mauzo kidogo, tafuta wateja wapya huku ukiwalinda wale wa zamani.
Maumivu ya mawazo hasi. Matatizo mengi ya kiafya na kihisia yanasabaishwa na hisia hasi. Hisia hasi kimekuwa chanzo cha kushindwa katika mambo mengi. Maumivu ya athari za hisia hasi yawe mwalimu kwako wa kukufundisha kutoka kwenye hisia hasi na kutawaliwa na chanya.
Unapopitia maumivu katika maisha yako, yaruhusu maumivu hayo yawe mwalimu wa kukufundisha na kukukumbusha kubadili hatua unazochukua. Hakuna maumivu yoyote yasiyo na somo la kujifunza na kuwa bora zaidi. Ili uweze kukua na kuchukua na kuwa bora tafakari kila maumivu unayopitia na kutumia kama ngazi kupandia juu.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.