Huu Ndiyo Ufunguo Wa Kupata Matokeo Ya Tofauti.


Categories :



Kuna matokeo unayoyapata ambayo yanakuudhi? Kuna matokeo ambayo umeyatamani siku nyingi lakini huyapati? Utaanzia wapi?

Kuna sehemu moja ambayo inabidi uianzie ili uweze kupata matokeo yoyote yale. Kupata matokeo ambayo huyapati sasa, ni lazima ufanye mabadiliko, yaani ufanye kitu tofauti na kile ulichozoea. Kwa kufanya kwa utofauti kunaweza kuwa kufanya kitu kipya au cha zamani kwa utofauti.

Kuanza jambo

Mara nyingi imekuwa ni rahisi mtu kuendelea na kazi anayoifanya kuliko kuanzisha kazi mpya. Kuanzisha jambo kama biashara kumekuwa na kalenda nyingi. Sababu kubwa ya kutokuanza kumekuwa ni kutokuwa tayari. Ndugu kuna jambo unataka kulianzisha wewe anza tu na kile ulichonacho. Ni vigumu sana kufikia maandalizi kamili. Anzisha na endelea kuboresha.


Kuboresha jambo.

Kila wakati kuna nafasi ya kufanya vizuri kiliko jana. Unafanya nini sasa? Huna budi kulikuza jambo unalifanya kama unataka kukua na kupata na mafanikio makubwa. Usiridhike na kile unachokipata sasa. Ongeza wateja wapya, pata maarifa mapya nk.

Kuacha jambo.

Je kuna tabia mbaya ambayo imekuwa inakuudhi na unatamani uiache? Je ni tabia ya kuchelewa kuamka? Je ni tabia ya kutoweka kuweka akiba? Je ni tabia ya kughairisha mambo? Ufunguo wa kupata matokeo ya utofauti katika hali hii ni kuacha kile unachokifanya na kufanya jipya. Acha kuchelewa kuamka na anza kuamka mapema. Acha tabia ya kutumia kipato chote sasa anza kuweka kiasi fulani kama akiba.

Anzia ndani.

Jambo lolote jipya lolote linaanzia ndani. Jambo lolote linaanza kama wazo. Hakuna mavuno unayoweza kupata bila kupanda mbegu. Mawazo ni mbegu ya kila jambo linalotokea. Ili uweze kuwa na mawazo mazuri hakikisha unapata maarifa sahihi kila wakati. Unasoma nini, unasikiliza nini, unaona nini ndivyo vinavyoweza kukusaidia kuwa na mawazo sahihi. Soma vitabu sahihi na kuzungukwa na watu sahihi ili uweze kuwa na mawazo sahihi.

Kuza ndani.

Ufunguo wa kukuza matokeo yako upo ndani yako kwanza. Huwezi kukua nje kama ndani bado umedumaa. Fikiri kwanza ndipo utakuwa na nafasi ya kukua nje. Ongeza wigo wa mafanikio yako kwenye fikra kwanza ndipo utapata nafasi ya kukuza mafanikio yako kwa nje. Toa mipaka kwanza ya kwenye fikra kuwa wewe ni wa kawaida na kuwaza na kuamini kuwa wewe ni wa kipekee. Toa mipaka ya kuwa wewe ni masikini na kuruhusu utaji ndani yako.

Ndugu! Ufunguo wa matokeo yenye mafanikio makubwa upo ndani yako. Ufunguo huo ni fikira. Faida kubwa ya fikra kuwa haina mipaka na hivyo kuruhusu mtu ajipimie mwenyewe. Kama unapata matokeo madogo, utambue kuwa hicho ni kipimo ulichojipimia, ongeza kiwango. Unataka nini maishani mwako, kuanza jambo, kukuza jambo au kuliacha? Tumia ufunguo wa fikra uliopo ndani yako.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *