Vitendo Vina Kelele Kuliko Maneno.
“Chuma hulia baada ya kupondwa na ngoma baada ya kudundwa. Kadhalika kipaza sauti hukuza sauti na si mawazo “
Miongoni mwa matamanio makubwa ya binadamu ni kutambulika na kuona ana umuhimu kwenye jamii. Kwa sababu ya matamanio haya watu wameweka bidii kuwaelezea watu jinsi ambavyo wangetamani kuwa hata pale ambapo wamepata matokeo kidogo tu ukilinganisha na ukubwa walioufikiria wanao. Ili kufidia upungufu huo wametumia maneno kujaribu kufidia matokeo yanayokosekana.
Nguvu hizi za kujitambulisha kwa maneno hazidumu kwa sababu maneno hupotea kirahisi na hivyo mtu kusahaulika kirahisi. Mara nyingine imewalazimu watu hawa kurudia maneno hayo mara kwa mara kwa sababu maneno yao hupunguka sauti na kupotea baada ya muda mfupi tu.
Kuna njia moja ya uhakika ambayo kila mtu anaweza kuitumia na kelele za thamani yake zikaendelea kusikika kwa muda mrefu. Hii ni njia inamfanya mtu kuendelea kuongea hata kama umelala usingizi. Si hivyo tu njia hii inamfanya mtu thamani yake kuendelea kupiga kelele na wengine kufaidi hata pale yeye atakuwa amekufa. Njia hii ni kwa VITENDO. Ndiyo vitendo hupiga kelele kuliko maneno.
Kati ya kitu ambacho kila mwanadamu ameweza kufanikiwa kukifanya ni kusema maneno. Watu wengi wanaongea nini wanataka maishani mwako. Na si kuongea tu, wanakwenda mbali wakisema ni kwa njia gani wanaweza kutumia kupata hicho wanachokitaka, lakini ni wachache sana wanaoweza kubadilisha maneno yao kuwa matokeo. Hii ndiyo sababu kubwa inawafanya watu wachache tu kufanikiwa katika maisha yao.
Hakuna njia yoyote unayoweza kutumia kubadilisha maneno kuwa matendo ambayo yana kelele kubwa hata kama umenyamaza zaidi ya kuweka kazi. Baada ya kuwa na maneno mazuri, baada ya mipango mizuri, sasa nenda hatua muhimu sana ya kupata thamani kutoka kwenye maneno hayo kwa kufanya vitendo.
Kufanya kazi kuna maumivu kuliko kuongea maneno, kufanya kazi kunahitaji kujitoa zaidi kuliko kuweka mipango. Ili mipango yako iweze kuzaa matokeo ambayo watu wataiona thamani yake na kufaidika, unahitaji kuweka nidhamu kubwa. Kuweka nidhamu ni kujisukuma kufanya kile ulichokipanga hata kama hujisikii.
Kadri unavyotaka kelele kubwa za matokeo yako ndivyo unavyotakiwa kuweka kazi kubwa za vitendo. Kadri kazi kubwa inavyohitajika ndivyo unavyohitaji nidhamu kubwa zaidi.
Kwa mfano kama unahitaji kuwa tajiri, kusema nataka kuwa tajiri kama mtu fulani, nitafanya biashara fulani inayolipa nk, hivyo peke yake haitoshi. Hata kama utaweka mipango mizuri sana kwenye makaratasi, hiyo nayo peke yake haitoshi. Unahitaji kuweka kazi sawasawa na matokeo unayoyataka. Utapata matokeo sambamba na kazi unayoiweka na sio kiasi gani unatamani au kelele za maneno unayoyaongea. Weka kazi.
Vitendo haviondoi umuhimu wa kuweka mipango katika maisha yako. Hakikisha unaweka mipango mizuri ya kile unachotaka kukifanya. Kama ni utajiri kupitia biashara hakikisha una mpango kamili wa namna gani unaenda kufanya ili kuweza kuufikia utajiri huo. Mpango huo utaonyesha ni nini hasa unaenda kukifanya kila siku. Baada ya kuwa na mpango huo weka kazi na matokeo yataonekana na watu watapiga kelele.
Unataka kuwa mwema, usijinasibu kuwa wewe ni mwema, tenda wema na wema wako utapiga kelele machoni na akilini mwa watu. Unataka kuwasaidia watu, acha kuongea bali toa thamani nayo itapiga kelele kwa niaba yako.
Tafakari leo; ni kitu gani umekuwa ukiiambia unacho lakini hujaweka vitendo na jamii ikapata thamani hiyo! Weka mipango ya kukifanya kitu hicho. Nakuhakikishia matokeo yake yataendelea kupiga kelele hata pale wewe utakapokuwa umeondoka.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz