Utofauti Wa Waliofanikiwa Na Walioshindwa Unaanzia Hapa.


Categories :

Watu wengi wamekuwa wakiamini kuwa waliofanikiwa wana vitu vya ziada kuliko walioshindwa. Wanaamini kuwa waliofanikiwa wana uwezo wa ziada ukilinganisha na walioshindwa. Hivyo masikini wanaoamini kuwa matajiri wana vitu vya upendeleo ndani yao ukilinganisha na wao.

Kama ni kwenye mashindano ya mbio basi waliofanikiwa na walioshindwa wote walianzia Kwenye mstari mmoja na wakiwa na fursa sawa ya kila mmoja kushinda. Lakini baada ya mashindano kuanza, ndipo tofauti zilipoanza. Kuamini hilo, unaweza ukakumbuka watu kadhaa ambao walizaliwa wakati mmoja, wakasoma na kuhitimu pamoja, wakaajiriwa kwa wakati sawa. Lakini baada ya muda mrefu sasa kuna utofauti mkubwa sana kimafanikio baina yao.

Utofauti wa waliofanikiwa haupo kwenye bahati wala kwenye uwezo walionao. Kila binadamu ana uwezo ndani yake wa kumwenzesha kupata mafanikio. Lakini tofauti kubwa ipo kwenye hatua ambazo kila kundi linachukua ili kupata matokeo;

Waliofanikiwa wanachukua jukumu la mafanikio yako bali walioshindwa wanaliacha jukumu hilo kwa watu wengine. Waliofanikiwa wanatambua wazi kabisa kuwa hakuna mtu mwingine wa kuwawezesha kufanikiwa isipokuwa wao wenyewe. Kwa hiyo hawategei watu wengine, badala yake wanajitoa kwa kila hali kuhakikisha wanapata mafanikio hayo. Walioshindwa hukaa wakifikiri kuna watu wengine watawasaidia kufikia mafanikio yao. Hata kama wao hawachukui hatua yoyote au wanafanya kiuvivu, wanafikiri serikali inawajibika kwa mafanikio yao binafasi. Wameyakosa, na hivyo kuishia kulaumu.

Waliofanikiwa wanatumia upekee wao kufanya makubwa bali walioshindwa wanafanya chochote. Waliofanikiwa wanatambua kuwa ndani yao kuna nguvu ya kipekee ya kuwawezesha kufanya vitu vikubwa vya kipekee ambavyo watu wengine wanashindwa kuviiga na hivyo kupata mafanikio makubwa. Walioshindwa hawautambui upekee wao na hivyo kuishi maisha maisha kwa kuiga wanachofanya waliofanikiwa, hii imeshindwa kuamsha uwezo wao wa kipekee na kuishi kuwa watu wa kawaida.

Waliofanikiwa wana ndoto kubwa bali walioshindwa wana ndoto ndogo au hawana kabisa. Waliofanikiwa wametengeneza ndoto kubwa na za wazi ambazo zimetawala fikra zao usiku na mchana, na wamewekeza nguvu, muda na umakini wote kuhakikisha wanazitimiza. Walioshindwa wanahofia kuwa na ndoto kubwa, badala yake wanaishia kupanga kufanya vitu vidogo tu ambavyo kila mtu anafanya. Hii imewafanya kuwa watu wa kawaida.

Waliofanikiwa wanazikabili changamoto bali walioshindwa wanazikimbia changamoto. Safari ya mafanikio haijawahi kuwa rahisi na ndiyo maana waliofanikiwa ni wachache sana ukilinganisha na wale walioshindwa. Waliofanikiwa huwa tayari kuzikabili changamoto zozote zinazosimama mbele ya mafanikio wakiamini bila kuzitatua changamoto hizo hawataweza kupata wanachokitaka. Walioshindwa hukimbia baada ya kukutana na ugumu kwenye waliyopanga. Kila wakati wanatafuta urahisi uko wapi hiyo wamebaki kuwa watu wa kuikamata kila fursa.

Waliofanikiwa hujenga hamasa ya kudumu bali walioshindwa huwa na hamasa za muda mfupi tu. Waliofanikiwa wana kwa nini kubwa ndani yao inayowafanya wawe na shauku kubwa ya kupata wanavyovitafuta licha ya changamoto wanazokutana nazo. Walioshindwa wana sababu ndogo tu za kuyapata mafanikio hayo ndiyo maana huanza kwa shauku kubwa kufanya jambo lakini kadri muda unavyoenda na kuanza kukutana na magumu hamasa hiyo huzidi kupungua na baadaye kupotea kabisa.

Ndugu! Wewe upo kundi gani? La waliofanikiwa au walioshindwa? Lakini kwa sababu bado upo hai, unaweza kuhamia kwa waliofanikiwa. Anza kuchukua jukumu la miasha yako sasa. Tambua upekee wako, tengeneza ndoto kubwa kutokana na upekee wako na kisha tafuta kwa nini kubwa ili kuwa na hamasa ya kudumu wakati unajenga mafanikio yako.

Nakutakia kila la kheri katika kuhama mtaa wa walioshindwa kwenda mtaa wa waliofanikiwa.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *