Tatizo La Kutopata Matokeo Limeanzia Hapa.


Categories :

Licha ya kuwa na tamaa ya mafaniko lakini watu wengi wameshindwa kuyapata mafanikio hayo. Licha ya watu kuwa vizuri kwenye kuweka malengo na mipango lakini hawajafanikiwa kupata matokeo. Hii ndiyo sababu ya watu wengi kuwa palepale miaka nenda miaka rudi.

Tatizo liko wapi? Hata wewe yamkini unaweza ukawa unajishuhudia kuwa ni miongoni mwa watu hao. Kwa sababu kama mipango umeipanga kila mwaka, lakini hujapata matokeo hayo. Watu umewaambia unataka nini, lakini bado hawajashuhudia matokeo ya kile ulichowaambia.

Licha ya sababu nyingi, mojawapo kuu ni ‘baadaye kugeuka kamwe’ . Ni kweli umekuwa ukiweka mipango mizuri ya kupata matokeo unayoyataka. Lakini waswahili wanasema mipango si matumizi. Baada ya kuweka mipango huchukui hatua nyingine muhimu ya kuweka kazi. Muda wa kufanyia kazi mipango yako ukifika, nasema nitafanya baadaye au kesho. Baadaye au kesho ikifika unaahirisha tena. Baadaye imekuwa kamwe, kwa sababu hujapata ulichopanga kukifanya.

Ndugu! Hakuna mbadala wa kazi, sehemu ambayo inabidi uweke kazi, huwezi kuweka maneno. Maneno matupu hayavunji mfupa. Ukiahirisha kazi umeahirisha matokeo.

Wengi wamekufa na kamwe; walipanga lakini muda ulipofika wakasema baadaye au kesho. Miongoni mwa vitu ambavyo watu hujutia wanapoondoka hapa duniani ni kutokuwa wamefanya vitu walivyokuwa na uwezo wa kuvifanya. Walipanga kuwa watu fulani lakini kila siku wakufanyia kazi yale ambayo yangewasaidia kuwa walivyotaka. Inawezekana walitakiwa kusoma na kupata maarifa lakini hawakufanya hivyo, kila siku walisema nitaanza kusoma vitabu kesho.

Kuchukua jukumu la maisha yako. Kutochukua jukumu la maisha yako ni sababu mojawapoa ya kutopata matokeo. Umeendelea kuahirisha ukiamini labda muda fulani ukifika nitalibeba hilo. Kwa sasa umeona jukumu hilo ni la wazazi wako, au serikali yako, au la watu fulani. Umeendelea kuahirisha na muda umezidi kwenda kisha umeshindwa kuwa mtu unayetakiwa kuwa.

Kutambua kusudi lako. Ukijitafakari unaona kama sababu fulani ya wewe kuwepo hapa duniani. Sauti ya kwa nini upo hapa duniani imeendelea kukuita lakini, lakini umeipuuzia na kuona kama muda bado. Lakini ni muda gani umepita tangu umeanza kuisikia sauti hiyo? Huwezi kupata matokeo ya kusudi lako kama utaendelea kuahirisha kulitambua kusudi lako. Kama huliishi kusudi lako, tambua kuwa unamsaidia mtu mwingine kuishi kusudi lake.

Kutengeneza ndoto yako kubwa. Umeendelea kuahirisha kutengeneza ndoto kubwa kwa sababu ya ndoto ndogo unayoiishi sasa. Kila wakati umeona muda wa kuwa na ndoto kubwa haujafika. Kadri unavyoendelea kufikiri muda bado unatengeneza mazingira ya kamwe kutoiishi ndoto yako kubwa.

Kuweka akiba. Ni muda gani umepita tangu ulipoona una kipato kidogo na huwezi kuweka akiba? Mbona sasa kipato chako kimeongezeka lakini bado huweki akiba? Je unasubiri ‘baadaye’ iwe ‘kamwe’? Usiahirishe kuweka akiba kwa kigezo cha kuwa una kipato kidogo bali anza kujenga tabia ya kuweka akiba tangu unapoona una kipato kidogo.

Kuanzisha biashara. Unafahamu umuhimu wa kuwa na biashara katika kutafuta uhuru wa kifedha. Lakini kila siku umesema nitaanzisha baadaye. Umetumia sababu ya kutokuwa tayari kuahirisha zoezi hili muhimu. Umeahirisha kwa kusingizia kuwa huna mtaji wa kutosha, huna maarifa ya kutosha au wewe siyo mtu wa biashara. Unajichelewesha kupata matokeo, anza leo kwa kutumia chochote ulichonacho.

Kuna vitu vingi ulivyoviahirisha kwa muda mrefu sasa ambavyo ukianza kuvifanya maisha yako yataboreka sana. Acha tabia ya kuahirisha mambo kisha weka nidhamu kubwa kufanya kile unachokuwa umepanga. Hakuna kitakachotokea bila kukifanya. Toa kuahirisha, ingiza kazi.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *