Dawa Ya Pili Ya Kutibu Ugonjwa Wako Wa Kushindwa.
Hongera kwa kutambua dawa ya kwanza ya kutibu ugonjwa wako wa kushindwa. Kumbuka dawa hiyo ya kwanza ilikuwa ni kubadili mtazamo. Tuliona kuwa hakuna unachoweza kukibadilisha maishani mwako bila kubadili mtazamo kwanza. Hivyo huwezi kubadilika kutoka kwenye kushindwa na kwenda kwenye kushinda kama hutabadili mtazamo wako. Kama hukupata bahati ya kusoma somo hili unaweza kulipa kwa kubonyeza kiunganishi hapa chini; https://www.amshauwezo.co.tz/2022/11/04/dawa-ya-kwanza-kabisa-ya-kutibu-ugonjwa-wako-wa-kushindwa
Baada ya kupata dawa ya kwanza, dawa inayofuata ni kuelekeza mtazamo wako sahihi ili uweze kuzaa matokeo. Dawa hii ni kuweka malengo bora.
Baada ya kuwa na mtazamo chanya kuwa unaweza, huna budi kuwa na uelekeo wa wapi kwa kuelekeza nguvu zako. Baada ya kuwa na mtazamo sahihi kuwa mafaniko yako ni jukumu lako, huna budi kujua ni majukumu gani unapaswa kuchukua na kwa namna gani? Baada ya sasa kuwa na mtazamo sahihi kuwa utajiri ni mzuri huna budi kuweka mipango ya kuupata utajiri huo. Ndiyo maana unahitaji dawa hii ya pili ambayo ni malengo bora.
Malengo ni kitu kinachokutambulisha nini unachotaka kufanya na ukifanyeje ili kiweze kukupa matokeo. Lakini malengo huenda mbali zaidi kutoa muda wa kukamilisha kile ulichokipanga. Hivyo malengo ni dira yako ya nguvu, muda, umakini na mali zako unazozitoa.
Kutokuwa na malengo sahihi imekuwa ni sababu kubwa ya watu wengi kushindwa. Kwani wengi wamekuwa wakirusha jiwe gizani, kuna nafasi ya kutopiga kitu au hata ukipiga utapiga chochote. Ukitaka upige ndege wengi waliopo mtini, huna budi kumchagua mmoja na na kumlenga. Ukirusha jiwe bila kujua ni ndege gani unamlenga, ni rahisi sana kutokumuua ndege yoyote.
Kuweka malengo kunaokoa muda. Kwa kutokuwa na malengo imekuwa sababu ya watu wengi kupoteza muda wao mzuri. Kufikiri nini cha kufanya kila wakati kunapoteza muda kuliko kungekuwa tayari kuna kitu ulichopanga kufanya kwa wakati husika. Hivyo ukifanikiwa kuweka malengo, kila muda ulionao utajua ni kwa ajili ya kufanya kitu fulani.
Kuweka malengo kunaongeza ufanisi. Kuweka malengo kunakusaidia kuweka umakini wako kwenye jambo moja au machache kwenye muda husika. Kwa akili na nguvu zako kuelekezwa kwenye jambo moja unaongeza uwezo wa kulifanya kwa umakini mkubwa.
Watu wengi wamekuwa wakiweka malengo, lakini ni wachache sana wamekuwa wakipata matokeo kwenye malengo wanayoweka. Sababu mojawapo kuu ni kutoweka malengo bora. Nitakushirikisha sifa za malengo bora ili wewe sasa uweze kuweka malengo hayo bora kisha kupata matokeo. Malengo bora yana sifa tano ambazo zinafupishwa kwa neno SMART; likisimama badala ya Specifici, Measurable, Attainable, Realistic na Time.
1. Specific (Malengo yawe maalumu): Lengo lolote unalolipanga lazima liwe wazi kabisa likielezea ni nini hasa unataka kukikamilisha. Usiliweke lengo kwa ujumla wake. Badala ya kusema mwaka huu nataka kuongeza kipato, taja kabisa kiasi, mwaka huu mataka kuongeza kipato kwa 20%.
2. Measurable (Malengo yapimike): Kwenye kila lengo unaloliweka hakikisha kunakuwa na kitu unachoweza kukipima.
3. Attainable (Malengo yafikike): Je unachokipanga unaweza kukifikia. Weka lengo ambalo wewe mwenyewe unaamini unaweza kulifikia.
4. Realistic (Malengo yawe halisi): Je unachokipanga kukipata kipo? Je asili ina kitu kama hicho? Lengo lako liwe na kitu ambacho kinaakisi uhalisia na sio kinachoenda kinyume na asili.
5. Time (Malengo yawe na muda maalumu): Lengo lenye sifa bora hupewa muda maalumu kufikiwa. Usiweke lengo ambalo halina ukomo kwani itakuwa ngumu sana kulifikia.
Ndugu, kama kweli unataka kupona ugonjwa wa kushindwa hun budi kunywa hii dawa ya pili. Kila wakati unpotaka kuweka malengo yako, tumia sifa hizo hapo juu kuweka malengo ambayo unaweza kuyatimiza.
Unapanga kutimiza nini miaka mitano ijayo, mwaka ujao au mwezi ujao. Weka malengo sasa kisha anza kuyafanyia kazi.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz