Dawa Ya Saba Ya Kutibu Ugonjwa Wako Wa Kushindwa.
Hongera kwa kufanikiwa kupata dawa sita sasa za kutibu ugonjwa wako wa kushindwa. Naamini kama umeendelea kutumia dawa hizi tangu siku ya kwanza mpaka sasa bila ya kuacha , basi utakuwa umeanza kupona. Endelea kunywa dawa hizi kila siku na ziwe sehemu ya maisha yako. Utajiuliza je sitapata madhara nikinywa kila siku? Ni kweli utapata madhara, lakini chanya.
Ili uzidi kukumbuka dawa hizi naenda kukutajia dawa zote sita zilizopendekezwa ili uzidi kuzikumbuka na kuziishi na kupata mafanikio unayostahili. Dawa ya kwanza ni Mtazamo sahihi, ya pili ni malengo bora, ya tatu ni kazi, ya nne ni nidhamu, ya tano ni ustahimilivu na ya sita ni tathmini. Leo utaenda kupata dawa ya saba katika kutokomeza kabisa ugonjwa huu, nayo ni kukua.
Maisha yako yameunganishwa na muda, na sifa kuu ya muda ni kutokusimama bali kuwa kwenye mwendo. Hivyo ili uweze kuufaida muda ulionao ambao una ukomo huna budi kuhakikisha unakua kila siku. Usikubali kuendelea kubali ulivyo siku zote. Kitu ambacho hakikui kinakufa.
Msingi mkuu wa kukua ni kutoridhika na kile ulichokipata sasa. Kikwazo kikubwa cha watu wengi kufanya makubwa zaidi ni mafanikio waliyoyapata. Wateja wengi uliowapata sasa unaona wanakutosha, kiasi cha kuona huhitaji kufanya masoko tena. Elimu uliyoipata unasema inatosha, huhitaji kujifunza zaidi. Ajira uliyonayo unasema inatosha na huhitaji kufanya biashara nk. Hivi ndivyo vinavyosababisha kushindwa kwako. Unahitaji dawa hii ya kukua ili upone.
Utafika kiwango ambacho unastahili kufika kama utarusu ukue kila siku.
Kuza maarifa yako. Hakuna siku itafika utasema unafahamu kila kitu. Na siku utakayosema hivyo, huu ndiyo utakuwa mwanzo wako wa kufa. Kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wengine na maarifa mapya. Kitu unachokifanya kuna watu walishwawahi kukifanya na kupitia changamoto ambazo na wewe unaweza ukawa unazipitia sasa. Hivyo itakuwa rahisi kwako kipita kwenye changamoto hiyo kama utajifunza kwa waliotangulia.
Kuza kipato chako. Kwenye biashara yako unayoifanya, hakikisha inakua kwa kukuza kipato chake. Unakuza kipato kwa kuuza zaidi wakati ukijitahidi kupunguza matumizi pale inapowekezekana. Hivyo usikubali kipato cha mwaka jana kikawa sawa na leo, utaishia kuugua kushindwa.
Kua kimtandao. Mafanikio yako yapo kwenye thamani unayoitoa kwa watu wengine. Huwezi kufikisha thamani unayoitoa kwa watu wengi na kupata utajiri kama huna mtandao mzuri wa watu sahihi. Kila siku kuza mtandao wa wateja wako. Mteja uliyenaye sasa akusaidie kukupa mteja mwingine.
Kuza thamani yako. Thamani ndiyo msingi wa mafanikio yako. Ubora wa thamani yako ndiyo utakaoamua pia ninkiasi gani ulipwe. Chochote unachouza, hakikisha thamani yake inaongezeka kila siku. Kuna nafasi ya kuboresha bidhaa au huduma unayoitoa. Kwa kuboresha thamani, itakuwa rahisi kukuza kipato chako.
Albert Einstein alisema “Insanity is doing the same thing over and over and expecting different results” akimaanisha kuwa uwendawazimu ni kufanya kitu kile kile kwa namna ile ile huku ukitegemea kupata matokeo tofauti. Huwezi kuendelea kufanya vile vile bila kuboresha halafu ukategemea ukuuji.
Jipange kuhakikisha leo yako ni bora kuliko jana na kesho yako kuwa bora kuliko leo. Hivyo ndivyo utakavyofanikiwa kupona ugonjwa wako wako wa kushindwa. Endelea kunywa dawa hizi kila siku. Hakika utakuwa mshindi.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz