Haya Ndiyo Maamuzi Yenye Hatima Njema Kwenye Maisha Yako.
Nini kinachoamua maisha yako ya kesho? Utakuwa wapi miaka kumi ijayo? Nini utakuwa umeshafanya muda wako wa kuishi hapa duniani utakapokuwa umeisha? Nani anaamua hatima ya maisha yako?
Haya ni maswali ambayo unaweza kuwa unajiuliza sasa. Sababu ya maswali hayo hapo juu inaweza kuwa ndiyo sababu iliyokusababisha kuwa hapo ulipo.
Matokeo unayoyapata yanatokana na maamuzi unayofanya wakati uliopita. Matokeo yanatokana na kile unachokifanya, na kile unachokifanya kinatokana na maamuzi unayofanya. Kumbe hatima ya maisha yako ipo kwenye kile unachoamua.
Matokeo uliyokwisha kuyapata ni kwa sababu ya maamuzi fulani uliyofanya kwenye maisha yako. Kama huridhiki na matokeo ya sasa, si kwa sababu yametokea tu bali ni zao la maamuzi uliyoyafanya. Kama huna akiba sasa ni kwa sababu ya kuamua kutokuweka akiba muda uliopita kwa kusingizia kuwa kipato chako ni kidogo.
Kadhalika kama una mipango mingi iliyotakiwa kuwa imekamilika na haijakamilika, basi tambua ni kwa sababu ya maamuzi uliyofanya muda uliopita ya kusema nitafanya kesho na kesho haijafika mpaka leo. Pia kama kuna makosa unarudia kila siku kwenye kitu unachokifanya na hivyo kukufanya uendelee kubaki palepale, basi ni kwa sababu ya maamuzi uliuofikia ya kusema kujiona wewe unajua kila siku na huhitaji kujifunza zaidi.
Lakini kwa sababu bado upo hai una nafasi bado ya kutengeneza hatima nzuri ya maisha yako. Yale utakayoamua kufanya leo na kisha kuendelea kuyafanya, ndiyo yatakayoamua ubora au ubovu, kufanikiwa au kushindwa kwako kutategemea maauzi yako ya leo. Yafuatayo maamuzi muhimu sana yatakayoamua mwisho wako mwema;
Shika hatamu ya maisha yako. Hatima ya maisha yako ipo mikononi mwako na kwame ulsimuachie mtu mwingine. Wewe ndiye wa kuamua ushinde au ushindee. Kama umeweka malengo basi tambua mtu wa kwanza wa kuhakikisha malengo hayo yanatimia ni wewe mwenyewe.
Weka vipaombele. Dunia ina vitu vingi sana vya kufanya kiasi cha kujikuta ukifanya chochota kama hutakuwa na vipaombele. Kipaombele chako nini? Kitu gani chenye mchango mkubwa kwenye mafanikio yako utakachoamua kukifanya kila siku? Je ni kutafuta mteja mmoja mpya wa baishara yako kila siku? Je ni kujifunza kitu kipya kila siku na kukitumia?
Amini. Sababu mojawapo kubwa inayowafanya watu wasiwe na maamuzi mazuri ni imani. Imani ni kuwa na uhakika wa kitu hata kabla hujakiona. Ukiwa na ndoto yako ambayo itaamua hatima ya maisha yako, basi amini kuwa utapata matokeo hata kama hujayaona mikononi. Hii itakupa hata nguvu ya kuendelea kuweka jitihada pale utakapopata changamoto.
Usiahirishe. Licha ya kuwa na vipaombele vizuri kwenye maisha yako ambavyo vitakupa mwisho wenye mafanikio lakini hutapata mafanikio hayo kamu utakuwa unaahirisha mambo. Fanya maamuzi haya muhimu leo ya kuhakikisha huahirishi yale mambo muhimu uliyopanga kufanya.
Ndugu! Natambua unatamani sana kuwa na hatima njema ya maisha yako yaliyojaa mafanikio. Lakini haya yote yatatimia kama hutakuwa na maamuzi bora leo. Nakusihi leo ufanye maamuzi hayo manne muhimu na naamini utakuwa na mwisho mwema ulijaa ushindi.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz