Kama Unataka Kufanikiwa, Usiige Alichokifanya Huyu Bwana Misosi.
Leo kuna harusi tatu! Watanikoma! Haya ni maneno ambayo jamaa mmoja maarufu kijijini alijisemea moyoni baada ya kuambiwa kuna harusi tatu kijijini hapo.
Umaarufu wa huyu jamaa ulikuwa ni kwenye kupenda kula sana. Alipenda kula kuliko kitu kingine chochote. Wanakijiji walioamua kumbatiza jina jamaa huyo na kumuita bwana misosi.
Ilikuwa jumamosi moja ambapo kijijini hapo palikuwa na harusi tatu. Kwa sababu ya hali ngumu ya uchumi, siku za sherehe kama harusi ndipo kulikuwa na fursa ya kukutana na chakula adimu kama ubwabwa, pilau, nyama nk. Hiki ndicho kilichomfanya bwana misosi aseme watanikoma.
Ili kuifaidi siku hiyo,bwana misosi aliazimia kuhudhuria kila harusi ambazo zilikuwa zipo vitongoji vitatu tofauti vya kijijini hicho. Vitongoji hivyo vilikuwa vimetengwa kwa umbali kidogo kiasi cha bwana misosi kuchukua hata saa moja kutembea kutoka kitongoji kimoja kwenda kingine.
Ili kuhakikisha anapata nafasi ya kula kwenye harusi zote, bwana misosi akaanza kutembelea maeneo ya matukio mapema. Alipoenda kitongoji cha kwanza aliona kwanza ndio wameanza kukoleza moto akasema hawa hawafai akaamua kwenda kitongoji cha pili.
Alipofika kitongoji cha pili akakuta ndiyo wanapika. Akaona hao nao wanamchelewesha akaamua kwenda kitongoji cha tatu. Huko akaona wameshamaliza kupika lakini wanasubiri muda wa kula ili chakuka kianze kugawiwa.
Ndipo bwana misosi alipoona bado wanamchelewesha akaamua kurudi kitongoji cha kwanza na kukuta sasa hao ndiyo wanasubiri kiive vizuri. Akaamua kwenda kitongoji kile cha pili na kukuta chakula kimeiva lakini wanasubiri watu na muda ili kianze kupakuliwa. Bwana misosi akapatwa na hasira kubwa kwa nini chakula hakiwi tayari kwa kula?
Aliamua kutimua mbiyo sasa kwenda kijiji kile cha tatu alikoacha chakula kikiwa tayari wakisubiri watu ili waanze kule. Alipofika pale akakuta watu wameshakula, chakula kimeisha na wananawa mikono. Hasira ikaongezeka na akaanza kupata hasira baada ya kuona dalili ya kutoonja chakula hata kama kulikuwa na fursa kubwa siku hiyo.
Ndipo alipoamua kurudi tena kitongoji cha kwanza sasa akiwa hana kasi ya kukimbia baada ya kuchoka kwa kuzunguka kwa muda mrefu. Alipofika akakuta ndiyo wananawa mikono na chakula kimeisha. Huku akiwa amejikatia tamaa akaamua ajikongoje kijiji cha pili kujaribu tu bahati, lakini huko ndio alikuta watu wamekula na kutawanyika kabisa.
Ndugu! Unaweza ukawa umemcheka na kumdharau bwana misosi, lakini unavyoendesha maisha yako huna utofauti na bwana misosi.
Ni kweli una hamasa kubwa sana ya kupata mafanikio kama bwana misosi alivyopania kula kwenye sherehe zote tatu. Lakini kama utaendelea kutaka kudaka kila fursa, muda wako utazidi kuisha huku ukiwa hauambulii chochote.
Uhakika wa bwana misosi kula ilikuwa kubaki kwenye harusi moja mpaka chakula kigawiwe ale na baada ya hapo angeweza kwenda kijiji kingine akala tena na kwenda kingine. Tamaa ya kutaka apate vyote kwa wakati mmoja vikamponza kisha kukosa kabisa.
Chagua kitu kimoja unachokipenda, kiwekee mipango sahihi. Kisha jiapie kuhakikisha unaweka muda,nguvu na umakini wako mpaka kisimame na kukupa matokeo unayoyataka. Kisha unaweza kuhamia kingine.
Ni biashara gani unaichagua kuhakikisha unaikuza mpaka ikupe mafanikio makubwa bila ya kujali changamoto utakazokutana nazo. Usihangaike na kila fursa ya biashara unayoambiwa. Baki kwanza kwenye kitongoji kimoja mpaka ule kabla hujaanzia kitongoji kingine.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz