*Hivi Ndivyo Umekuwa Ukiukuza Mbuyu Kwenye Chungu.*


Categories :

Mbuyu ni miongoni mwa miti mikubwa duniani. Huheshimika kwa unene wake kwani hata kama upo mbali utaonekana kwa sababu ya unene huo.

Kwa sababu ya ukubwa wa mti wenyewe, mizizi yake hulazimika kuwa mikubwa na hivyo kusambaa na kujishikiza kwa uimara mkubwa kwenye ardhi ili kuhakikisha unaendelea kuusimamisha mti huo.

Hivyo unaweza kumshangaa mtu akisema anataka kuuotesha mbuyu huo na kuukuzia kwenye chungu cha maua. Unaweza kumcheka na kumdharau kwamba mbona hafikirii.

Ungemshangaa kwa sababu unatambua kuwa mbuyu ukikua huwa mti mkubwa sana na hivyo hauwezi kukuzwa kwenye chungu. Kwani ukishaongezeka mizizi yake itashindwa kwenda mbali. Hata hivyo chungu kitapasuka, udongo utasambaratika kisha mti kunyauka.

Lakini ndivyo ambavyo umekuwa ukifanya kwenye maisha yako. Uwezo ulioko ndani yako ni kama mbegu ya mbuyu. Unatarajiwa uioteshe na kuikuza katika kipindi cha maisha yako kuwa mbuyu mkubwa ambao kila mtu atauona.

Mbegu hiyo ya uwezo wako inafananishwa na mbegu ya mbuyu kwa sababu inatarajiwa ionwe kama matokeo makubwa ambayo ni miujiza mbele za watu wengine. Unatarajiwa uuamshe uwezo wako na kufanya miujiza; mambo ambayo wengine watasema wewe una nguvu za ziada.

Mbegu ya uwezo wako ndiyo inayokusaidia kufanya vitu vya ubunifu mkubwa na kupata matokeo makubwa na ya kipekee. Kama hujaanza kuyaona matokeo hayo, tambua kuwa wewe unaotesha mbegu ya mbuyu kwenye chungu cha maua, na kamwe hutapata matokeo ya mbuyu wa mafanikio katika maisha yako.

Licha ya uwezo wa mbegu ya mbuyu kuwa mbuyu, mazingira ambapo mbegu ilipandwa inaweza kuzima ndoto ya mbegu hiyo kuwa mbuyu uliokamilika.

*Mtazamo wako ni chungu.* Je unaamini kuwa una nguvu kubwa ndani yako ya kufanya mambo makubwa na muujiza katika maisha yako? Kama jibu ni hapana, basi tambua kuwa umepanda mbegu ya uwezo wako kwenye chungu.

*Ndoto ndogo ni chungu.* Moja ya kitu chenye uwezo mkubwa wa kuamsha uwezo wako na kupata mafanikio makubwa ni kuwa na ndoto kubwa, ndoto ambayo si rahisi watu wengi kukuelewa na mara nyingine ukibakia pekee yako. Kwa kuwa unajijengea ndoto ndogo ambayo kila mtu anaamini, basi umeweka mbegu yako kwenye chungu.

*Kukosa maarifa ni chungu.* Maarifa sahihi huleta mawazo sahihi. Mawazo sahihi huamua vitendo sahihi. Kadri unavyoongeza maarifa na kuyatumia ndivyo unavyozidi kuamsha uwezo wako. Je unasoma vitabu? Je unahudhuria semina mbalimbali za kupata maarifa? Kama jibu ni hapana tambua kuwa unapanda ya mbuyu kwenye chungu.

*Watu wanaokuzunguka wanaweza kuwa chungu.* Watu unaoshirikiana nao kwa ukaribu wana mchango mkubwa wa kuamsha uwezo wako au kuendelea kuubembeleza uendelee kulala. Kama unaoshirikiana nao hawaamnini kama unaweza kutimiza ndoto yako, wanaweza kuihamishia mbegu yako kwenye chungu!

Ndugu! Licha ya kuwa na uwezo mkubwa sana ndani yako, unahitaji mazingira mazuri ya kuuamsha kisha kuweza kukupa mafanikio makubwa. Anza kujiona una nguvu kubwa ndani yako unayoweza kuitumia kupata mafanikio zaidi, tengeneza ndoto kubwa na jisukume kuitimiza huku ukiimarika katika maarifa.

Una mbegu ya mbuyu ndani yako, usiipande kwenye chungu.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *