Njia imefungwa. Pita huku!


Categories :

Njia imefungwa! Pita kulia! Pita kushoto! Haya ni maandishi unayoweza kukutana nayo kwenye barabara ambayo umezoea kuipita.

Kukiwa na matengenezo kwenye barabara uliyozoea kupita, barabara hiyo hufungwa ili kupisha ukarabati huo. Lakini mamalaka huwa haziachi watumiaji wateseke, badala yake hutafuta namna ya kuwawezesha kuendelea na safari. Huandaa njia nyingine na kuwaelekeza watu wapite huko. Hakuna kuahirisha safari.

Safari ya mafanikio yako haiahirishwi, njia ya kwanza haijakupi majibu, usiahirishe jitihada bali hamia mbinu nyingine.

Kwa nini umekuwa ukirudi nyumbani pale unapokutana na changamoto kwa kusema kama mambo yenyewe ni magumu kiasi basi Bwana! Hujafika unakotakiwa uende, usirudi nyumbani.

Usiache lengo, badili mbinu. Kama hupati matokeo ya lengo ulilonalo basi mbinu zake zinawezakuwa hazifai. Usiseme hili lengo halifai na kuliacha, badala yake badili mbinu unazozitumia kwenye lengo hilo. Lengo ni zehemu unayotaka ufike njia hii imefungwa pita njia nyingine ya kukufikisha unakoenda.

Leo ukishindwa endelea kesho. Unapofanya jambo na hasa kwa mara ya kwanza, kuna nafasi ya kushindwa. Lakini kushindwa siyo kukosa. Ukishindwa leo kuna nafasi ya kupata kesho. Leo njia imefungwa, pita kesho kwa kurudia jambo hilo huku ukisahihisha makosa.

Asiponunua leo mkumbushe kesho. Mteja kununua kwenye biashara yako ni jambo la mchakato. Asiponunua leo si kwamba hana nafasi ya kununua leo. Mpe nafasi; endelea kuwasiliana naye na kumuelimisha kuhusu biashsra yako. Kuna siku atanunua tu. Njia ya mauzo ikifungwa leo, pita kesho.

Ukiteleza inuka . Kila mtu anaweza kuteleza na kuanguka wakati anatembea. Mtu akiteleza anatarajiwa atainuka. Mshangao huwa unakuja pale mtu anapoanguka kisha kuendelea kulala palepale. Ukishindwa jambo usikate tamaa, badala yake nenda ujipange upya na rudi kwa umakini na nguvu kubwa zaidi.

Jana hujafanya, fanya leo. Kuna mipango ulitakiwa uikamilishe mwaka jana, mwezi uliopita au jana na huweza kufanya hivyo. Jana ilishindimana lakini kuna nafasi nyingine tena leo. Hakikisha leo huachi tena kabla hujafanya kile ulichoshindwa jana. Njia ya jana imefungwa, pita leo.

Ndugu! Kuna mbadala kwenye kila changamoto unayokutana nayo. Usikubali kukata tamaa. Njia moja ikifungwa, mara nyingi kuna kuwa na njia mbadala, pita huko ufike unakokutaka.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *