Hii Ni Tabia Inayozidi Hata Kipaji.
Ukimuona mtu anayeanza kuponda jiwe kwa nyundo, unaweza kumuonea huruma au kumkatia tamaa. Kwani wataki atakapokuwa anashusha nyundo zile za kwanza, jiwe litaendelea kumwangalia tu bila y ahata kuonyesha dalili kuwa litapasuka.
Lakini kuna kitu cha ajabu sana hutokea pale ambapo mpondaji anapokuwa mvumilivu na mstahimilivu akiendelea kushuka nyundo juu ya jiwe hilo hilo. Zinaweza kufika hata nyundo hamsini ndipo jiwe linaanza kuonyesha ufa wa kupasuka.
Lakini jambo hili hutokea pale mpondaji anapoamua kuchagua jiwe moja na kuendelea kushusha nyundo bila kuhamia jiwe jingine.
Lakini kama akianza kushusha nyundo kwenye jiwe moja kisha kuhamia jingine baada ya kuona la kwanza halipasuki basi anaweza kushusha nyundo kuanzia asubuhi mpaka jioni bila ya hata na kuw akipande kimoja cha jiwe lililosambaratika.
Hapa kuna siri kubwa sana ambayo tunaweza kuitumia kwenye maisha yetu ya kila siku. Umekuwa ukishusha nyundo kadhaa kwenye jiwe moja na baada ya kuona hakuna dalili za jiwe kupasuka, umeliacha jiwe hilo na kuhamia jingine.
Kumbuka kuna vitu vingapi mpaka sasa ulivyovjijaribu na kuviacha? Biashara ngapi umeanza na baada ya kukutana na ugumu ukaacha na kuhamia nyingine?
Kama kwa mponda mawe siri ya jiwe mawe kusambaratika ni kuendelea kushusha nyundo kwenye jiwe moja mpaka lisambaratike kisha kuviponda vipande vile vikubwa kupata vidogo zaidi kabla ya kuhamia jiwe jingine.
Utapata mafanikio makubwa na unayostahili katika maisha yako kwa kuchagua kitu kimoja maishani mwako kisha kukifanya hicho , kukomaa na hicho, kuzama kwenye hicho , kuwekeza kwenye hicho mpaka upate matokeo makubwa unayotarajia.
Kukaa kwenye kitu kimoja imekuwa ni changamoto kwa watu wengi. Watu wamechoka lakini haana matokeo ya maana. Watu wameshakuwa kwenye kazi muda mrefu lakini hawana mafanikio yoyote ya maana.
Kama mponda mawe akiamua kushusha nyundo chache kwenye jiwe moja kisha kukimbilia kwenye jiwe jingine, tambua kuwa itafika jioni akiwa amechoka lakini hana kazi yoyote yenye maana aliyoifnya, ndivyo ilivyo kwako wewe unayegusa kitu kimoja kwa muda mfupi kisha kuhamia kingine. Umekuwa ukichoka bila ya kupata matokeo.
Ili uweze kupata matokeo yatakayokupa mafanikio mkubwa katika maisha yako huna budi kuweka malengo kutoka kwenye ndoto zako kisha kuzama mzima mzima kwenye lengo hilo mpaka upate matokeo. Hii ni muhimu kwa sababu kila kitu huonyesha ukinzani mwanzoni. Gari huhitaji nguvu kubwa kuanza kisha ukinzani huo hupungua baada ya kushika kazi.
Hata ndege huhitaji kutumia nguvu kubwa sana wakati inaanza kupaa ili kukabiliana na ukinzani wa upepo na mwngine. Lakini ukinzani huo hupungua na kuanza kutumia nguvu kubwa ikishafika juu sana.
Calvin Coolidge ambaye alikuwa Rais wa 30 wa Marekani alinukuliwa akisema hakuna kitu kinachoweza kuchukua nafasi ya msimamo, si kipaji, wala si ujiniasi au elimu. Hivyo kupitia msimamo ndipo unapoweza kupata chochote unachokitaka.
Lakini faida hii ya msimamo itakuwa na faida pale utakapochagua kuwekeza nguvu, muda na umakini wako kwenye jambo moja. Nyundo ya kwanza juu ya jiwe inaweza isilete mabadiliko yoyote juu ya jiwe mpaka nyundo ya 50 itakapodondoka juu ya jiwe hilo. Lakini nyundo ya 50 haiwezi kujisifu pekeyake kwani nyundo ya kwanza ilikuwa mchango wa kulilegeza jiwe hilo.
Hata kama utakuwa huoni matokeo mwanzoni, endelea kufanya kitu ulichokichagua, kuendele kutakusaidia kuondoa ukinzani. Endele kutangaza biashara yako kuna muda watu wataifahamu na watakuja kununua. Endelea kuwekeza hicho kiasi kidogo hata kama huyaoni matokeo makubwa baada ya muda mrefu uwekezaji wako utakua na kuwa mkubwa. Unachagua kitu gani leo ambacho utakifanya kwa msimamo?
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz