Kwa Nini Husogei?


Categories :

Kama utamuona mtu sehemu hiyo hiyo barabarani kwa muda mrefu bila ya kwenda mbele au kurudi nyuma, utamshangaa sana. Unaweza kujiuliza maswali mengi ambayo ukakosa majibu ya kwa nini yupo pale akiwa ameganda kwa muda mrefu hivyo?

Na mara nyingine unaweza kwenda mbali zaidi ukiamini atakuwa amechanganyikiwa. Lakini mgando kama huo upo katika maisha ya watu wengi;

[ ] Ni muda mrefu sasa umepita lakini bado una maarifa yaleyale na hivyo kuendelea kutumia mbinu zile zile hata kama hazikupatii majibu mazuri!

[ ] Ni muda mrefu sasa tangu uanzishe biashara yako, lakini ipo vile vile

[ ] Ni muda mrefu sasa kipato chako kipo vile vile licha ya maisha kupanda bei

[ ] Ni muda mrefu sasa tangu uwe na mgogoro kwenye mahusiano, hujatatua mpaka leo.
Ndugu! Ili uweze kwenda mbele unahitaji kupiga hatua. Kupiga hatua ni kukua na mara nyingine bila kujali kasi. Hivyo kama hukui ina maana hupigi hatua.

Baada ya kuwa na malengo unatarajiwa kuanza kupiga hatua kwa kufanyia kazi mipango yako kwa nidhamu kubwa. Kama unaona hupati matokeo yoyote basi tambua umebaki umeganda sehemu moja. Hii ni hatari kubwa!

William Bourroughs alisema “When you stop growing you start dying”, akimaanisha kuwa pale unapoacha kukua unaanza kufa.

Kuna vitu viwili vikuu vitakavyokusaidia kukua. Cha kwanza ni malengo na cha pili nidhamu.

Kuweka malengo ni kuwa na dira ya kitu gani unataka kukifanya. Ili uwe kwenye mwelekeo wa kujua hakikisha malengo yako ya sasa yanakuwa makubwa kuliko yale uliyofanikiwa kutimiza. Huu utakuwa mwanzo mzuri wa kukusukuma kuamsha nguvu kubwa zaidi ndani yako.

Kitu cha pili cha kukufanya ukue ni nidhamu. Haijalishi utaweka malengo mazuri kiasi gani kama hutuweka kazi ni bure. Kufanyia kazi malengo si kitu rahisi, ndiyo maana wanaoweka malengo ni wengi, lakini wanaoyatimiza ni wachache mno.

Ndiyo maana nidhamu inahitajika ili uweze kupiga hatua baada ya kuweka malengo. Nidhamu ni kufanya ulichopanga bila ya kusikiliza sababu yoyote ile. Watu hawapati matokeo na kupiga hatua kwa sababu wanaruhusu sababu pale muda wa kufanya kazi unapofika.

Kupiga hatua kunahitaji kazi na hakuna mbadala wa kazi. Bahati mbaya sana watu wengi hawapendi kazi. Muda wa kazi unapofika kunatokea vishawishi vingi vya kuahirisha kufanya kile unachotakiwa kufanya.

[ ] Muda ukifika utahisi hujisikii kufanya kazi.

[ ] Muda ukifika utahisi mwili na akili vimechoka.

[ ] Muda ukifika vitatokea vitu vingine vizuri ambayo utaona unavipenda kuvifanya kuliko ile kazi.

[ ] Muda ukifika kuna usumbufu mkubwa utajitokeza. Haya yote hutokeo ili mradi tu usifanye kazi.

Umekuwa ukifanya nini baada vipingamizi hivi vinapotokea? Kama umekuwa hupigi hatua, ina maanisha kuwa umekuwa unakubali kuvutwa na vipingamizi hivyo. Watu wengi wamekuwa wakiikimbia kazi kwa kujifariji kuwa watafanya baadaye. Kesho au siku nyingine. Ugonjwa huu unaitwa kuahirisha na ndiyo uliodhoofisha sana maisha ya watu wengi.

Ili uweze kupiga hatua huna budi kujenga nidhamu kali ya kukuwezesha kupiga hatua. Jisukume kuchukua hatua hata pale unapokuwa hujisikii.

Ili uweze kujisukuma tafuta sababu ya kwa nini ujitese. Kama hatuna sababu kubwa ni ngumu kuiishi nidhamu kali. Je sababu kuu yako kuondokana na umasikini, kuboresha afya, kuanzisha na kukuza biashara, kufikia uhuru wa kifedha au nini?

Weka lengo, ainisha sababu ya lengo kisha weka nidhamu kali na ya kudumu. Hakika utapiga hatua kubwa.

Kwa ufahamu zaidi kuhusu kujenga nidhamu usisite kuwasiliana na mimi kupitia mawasiliano hapo chini.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *