Ni Mpaka Uanze Ndipo Utamaliza.
Natamani niwe wa pekee, natamani niwe maarufu, natamani niwe tajiri, natamani niwasaidie wengine, natamani niishi kusudi langu, natamani niwe na ridhiko moyoni mwangu. Unaweza ukawa unatamani vitu vingi.
Umekuwa mzuri sana kwenye kutamani na mara nyingine kuweka malengo. Inawezekana ni muda mrefu sana tangu umeanza kutamani na kupanga lakini huna matokeo yoyote mpaka sasa. Tatizo liko wapi?
Kuna hatua moja ambayo imekuwa ni changamoto kwa watu wengi kutokupata matokeo licha ya kutamani na kuweka malengo. Kitu hicho ni kutokuanza.
Mipango yako imekuwa mizuri sana lakini huanzi. Huna matokeo kwa sababu huanzi. Hatua ya kuanza ina ukinzani mkubwa sana.
Hapa tunaenda kujifunza sababu zinazochangia kwenye kutokuanza na sluu unazoweza kuchukua ili uanze kupata matokeo kwenye yale uliyoyatamani siku nyingi.
Anzia ulipo. Mara nyingi umeahirisha kuanza kwa kujiona bado hujawa tayari. Ndugu, maandalizi huwa hayaishi. Kila wakati utaona bado kuna kitu hakijakamilika ili wewe kuanza. Kushinda ukinzani huu wewe anza tu. Anzia ulipo kwa kutumia ulichonacho.
Weka nguvu kubwa. Ni wakati wa kuanza ndipo unapokutana na ukinzani mkubwa. Gari hutumia nguvu kubwa kuanza kabla halijashika kasi. Ndege hutumia nguvu kubwa kukabiliana na ukinzani wa kimo cha chini kabla ya kufika juu zaidi. Hivyo jitoe kukabiliana na vikwanzo vingi mwanzoni. Utakutana na ukinzani mkubwa unapoianza biashara yako.
Weka wazi sababu ya kukifanya kitu hicho. Kama kile utakachokikosa kwa kutokuanza kile kitu hakipo wazi ni vigumu kuanza kwa sababu hutakuwa na hofu ya kutokipata. Ona mapema matokeo ya kitu unachotaka kukifanya. Hii itakuwa msukumo kwako kwa nini ukikose?
Ondoa laana. Weka hii kwenye akili yako kuwa kutokuanza ni kuendelea kuikumbatia laana. Huwezi kupata kitu bila kuanza. Hivyo fungua kili yako na jiambie kuwa nataka kutoa laana ya kutopata kile ninachokipata. Nafanya hivyo kwa kuanza.
Ndugu hutafanikiwa kupata chochote mpaka umeanza. Muda umefika sasa wa kuanza. Anzia hapo ulipo. Ondoa laana ya kutokupata unachokitaka.
Anza kuweka akiba sasa. Anza biashara ya ndoto yako sasa. Anza kuandika sasa. Anza kusoma vitabu sasa. Anza kuboresha mahusiano yako. Anza kuishi ndoto yako.
Anzia ulipo, anza leo.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz