Ukifanikiwa Kupeleka Mkono Wako Mdomoni Tu, Umemaliza Kazi!
Unakula ili uishi. Lakini ili uweze kukamilisha hilo, mwili wako huwa unasubiri mpaka upeleke tonge mdomoni. Ukitafuna na kumeza, kazi inakuwa imeishia hapo. Wewe hujui kinachoendelea baada ya hapo. Unasubiri njaa iume tena.
Wewe kaa kwenye hewa. Lakini pia ukifanikiwa kukaa kwenye hewa kinachofuata ni wewe kuendelea na shughuli zako. Hewa safa itaingia mwilini na hewa chafu itatolewa nje.
Kumbe kuna vitu automatiki vitatokea baada ya wewe kufanya jambo fulani kwanza.
Hata katika kusaka mafanikio yako, kuna mambo unayotakiwa kuyafanya kwanza na baada ya hapo kuna matokeo yatatokea. Matokeo hayo ni automatiki, yapo nje ya uthibiti wako, Lakini yatatokeo tu.
Wewe weka kazi tu. Sheria ya sababu na athari inasema kwenye kila athari kuna sababu iliyofanya hayo yote yatokee. Kinachotangulia kwenye sheria hii siyo athari au matokeo, bali kisababishi.
Je unataka mafanikio katika maisha yako? Naamini jibu litakuwa ni ndiyo kwako. Basi nakuambia kuwa unahitaji kisababishi na baada ya hapo mafanikio yatakuja automatiki. Kisababishi cha mafanikio ni kazi kwenye mipango yako.
Wewe anza tu. Unapoanza hata kwa kupiga hatua moja tu, safari hako inapungua. Hii inamaanisha kuwa kama ni biashara, unapoianza na kuendelea ndivyo unavyozidi kuisogelea faida na mafanikio ya kiuchumi. Wewe anza tu
Wewe weka akiba tu. Moja ya kitu ya kitu kinachowapa watu utajiri ni akiba. Wanaupata utajiri huo kwa kuweka akiba kutoka kwenye kila kipato wanachoingiza. Nidhamu hii inawafanya baada ya muda kuwa na fedha na kisha kuwekeza sehemu inayozalisha zaidi.
Kuweka akiba ni kisababishi ambacho kinakupatia utajiri automatiki. Wewe wekeza tu.
Wewe toka nje. Kama kuna matokeo unayapata sasa na huyafurahii unahitaji kutoka nje. Toka nje ya vile unavyovifanya sasa. Toka kwenye mazoea unayofanya sasa. Ukitoka kwenye mazoea na kuanza kufanya kwa sababu, basi wewe subiri matokeo, yatakuja automatic.
Wewe jiandae tu. Mwanafalsafa Seneca alisema “Luck is when preperation meets opportunity ” ikiwa na tafsiri kuwa bahati ni pale maandalizi yanapokutana na fursa. Kumbe usimuonee wivu mtu anapopata kitu na kumwambia huyu jamaa ana bahati sana. Kuna kitu kinachotangulia kabla ya bahati hiyo kuonekana, nacho ni maandalizi. Wewe jiandae na mtaji, kuna manunuzi ya bei ndogo sana utakutana nayo.
Ndugu una kazi ya kupeleka kwanza mkono wako mdomoni ili chakula kiingie tumboni baada ya hapo kila kitu ni automatiki.
Nini unakitaka maishani mwako? Kiwekee malengo na mipango kisha nidhamu kali ya kazi, baada ya hapo mafanikio yatakuja automatiki.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz