Endelea Kumwagilia; Huwezi Kuchuma Matunda Kwenye Mche.
Ili kuweza kupata matunda kutoka kwenye mti, mbegu yake huzikwa ardhini kisha kuota na kutoa mche. Mche wake huendelea kumwagiliwa ili uendelee kukua na kuwa mti kisha kuzaa matunda.
Itakuwa ni ajabu mkulima huyo kuanza kuulaumu mche wa mti huo kwa kutokutoa matunda. Hii ni kwa sababu mkulima hujua ni mti uliokamilika ndiyo unaotakiwa kuzaa matunda na hivyo ana kazi ya kuendelea kuumwagilia mche huo.
Hiyo ni kanuni ya asili ambayo ipo kwenye hiyo mbegu. Lakini kanuni hiyo haijaishia tu kwenye mbegu ya mti wa matunda tu bali hata kwenye mbegu uliyonayo ndani yako.
Ndani yako kuna mbegu ya uwezo wa kipekee. Hii ni nguvu unayotakiwa uiamshe na kukupatia kile unachokitaka maishani mwako.
Lakini uwezo huo ni kama mbegu, ili uweze kukayaona matunda lazima uendelee kuumwagilia kwa muda mrefu. Lazima utambue kipaji chako, ukinoe na kuendelea kutumia kupata matokeo kwenye malengo yako.
Zoezi la kuamsha uwezo wako na kuutumia kuishi ndoto yako si jambo la siku moja. Itachukua muda mrefu sana mpaka kuja kuona matunda yake.
Watu wengi wameshindwa kufaidi matunda ya uwezo kwa sababu ya uharaka wa kutaka matokeo ya haraka katika kuishi ndoto zao.
Licha ya kutambua nini unakitaka maishani mwako, na kutambua mbegu ya uwezo ulionao wa kukuwezesha kupata unachokitaka kuna kitu cha ziada kinahitajika.
Kitu hicho ni ni muda wa kukua na kuzaa matunda.
Licha ya kuwa na uwezo ndani yako wa kuwa tajiri lakini utahitaji muda wa kukua mpaka kufikia utajiri huo. Hivyo unahitaji kusubiri mche ukue, uwe mti, utoe maua na baadaye matunda.
Inawezekana mpaka sasa tayari uwezo wako umeshaota, yaani una ndoto na mipango ambayo unaifanyia kazi. Ukitafakari, unaona upo kwenye njia sahihi lakini kinachokosekana ni matokeo. Nakwambia uskate tamaa, kama mche unavyotakiwa kuendelea kumwagiliwa ili uweze kuzaa matunda, ndivyo unavyotakiwa kuendelea kuweka jitihada kwenye mipango yako ili upate matokeo unayoyatarajia.
Usiwe miongoni mwa wale wanaokimbilia njia za mkato ili kupata mafanikio ya haraka. Hakuna njia ya makato ya kupata mafanikio makubwa na ya kudumu. Unahitaji kuanzisha safari na kuvumilia urefu wa njia mpaka kufika u unakotakiwa.
Jenga tabia ya uvumilivu huku ukiepuka tamaa za kuchepuka. Baki na vumilia kwenye lengo lako.
Jikumbushe ndoto, malengo na mipango yako kila siku. Endelea kuboresha mbinu hizo kila siku ili kuwa bora kila siku. Hakika utavuna mafanikio unayostahili.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz