Lazima Fundi Akatekate Kitambaa Kwanza!
Kama hujawahi kumuona fundi cherehani akikatakata kitambaa wakati anashona nguo yako, unaweza kugombana naye. Utagombana naye baada ya kuona kitambaa kilichokuwa kizima na kupendeza sasa kinakatwakatwa kwenye sura isiyoeleweka.
Lakini kama utapana nafasi ya kusubiri pale atakapoanza kuviuganisha vipande hivyo, utaannza kupata faraja kuwa kuna kitu cha maana kwenye kile kitambaa ulichogharamikia.
Mvurugano huo ndiyo unaotakiwa utokee maishani mwako ili uweze kupata kitu cha thamani zaidi na kupiga hatua zaidi. Una vitu unavyo au unavifanya sahihi, vinapendeza sana lakini thamani yake ni ndogo sana
Ili uweze kutoka kwenye hali ngumu uliyonayo sasa huna budi kuvuruga baadhi ya vitu ulivyovishikiria visivyo na faida kwako.
Vuruga mtazamo wako. Kuna mitazamo hasi uliyoikumbatia siku nyingi, imekupa hasara, imekuchelewesha. Hii inahitaji kukatwakatwa na maarifa sahihi ili kuweza kuwa na mtazamo sahihi na kuwa na thamani kubwa kwenye mawazo na maamuzi yako. Vuruga mtazamo wa kuona huwezi kisha shona mtazamo wa unaweza.
Katakata kubaki eneo lenye uhuru kisha ingia viwango unavyostahili. Kuna maeneo mengi ya maisha uliyoyazoea kuyaishi. Haya ni maeneo unayojisikia vizuri kuwepo hata kama hayakupai matokeo mazuri. Unapenda sana kulala na kuchelewa kuamka. Unajisikia raha kutumia kipato chote. Unapenda sana kuiga. Unahitaji sasa kuuvuruga uhuru huu ili uweze kupiga hatua kubwa nje ya uhuru huo.
Vuruga marafiki ulionao na tengeneza wazuri. Watu wanaokuzunguka wana mchango mkubwa sana kwenye mafaniko yako. Kama marafiki wa sasa hawakusaidii kufika safari yako unahitaji kuvuruga na kupata watakaokuwa msaada kufikia malengo yako.
Vuruga matumizi yaliyokukosesha uhuru wa kifedha. Je utatumia fedha kama ulivyopanga? Je matumizi yako hayazidi kipato chako? Je huwa hununui vitu ambavyo hujapanga kununua? Unahitaji kukatakata hizi tabia za matumizi mabovu.
Ndugu, kuna vitu au tabia ulizonazo sasa, zinapendeza kweli unaona shida kuziharibu kwa sababu zinakupa raha ya muda. Lakini kama kuna matatizo uliyonayo sasa ni kwa sababu ya tabia hizo.
Kama unahangaika mtaji wa kuanzishia biashara basi tambua ni kwa sababu unajisikia raha kutumia kipato chote. Kama siku yako inakosa ufanisi, basi tambua ni kwa sababu unachelewa kuamka. Kama una mtazamo hasi unaokukwamisha kupiga hatua, basi tambua ni kwa sababu ya watu waliokuzunguka wenye mitazamo hiyo.
Unahitaji kukatakata chochote kinachokupa raha ya muda ingali kikiharibu njia ya kufikia makuu. Huwezi kupata cha thamani zaidi bila kuvuruga mambo yako ya sasa.
Tabia gani unaipenda lakini unaona inakufifisha kwenye safari yako kuu? Anza kuikatakata leo.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz