Dhoruba Inakuja, Simama Hapa Usianguke!


Categories :

Uimara wa nyumba hupimwa wakati wa dhoruba. Sifia nyumba yako kwa uzuri na uimara wake, lakini sifa hizo zitathibitika pale mafuriko na pepo kali vitakapokuja.

Uimara wa nyumba huanzia kwenye msingi wake. Nyumba iliyojengwa kwenye msingi imara, hustahimili mafuriko na pepo kali. Licha ya mafuriko na pepo kali kuifikia nyumba, lakini msingi ule imara huendelea kuishikilia nyumba na kubaki salama.

Ukuaji, ustahimilivu na uimara wa maisha yako katika maeneo mbalimbali vinategemea sana misingi uliyoijenga kwenye kila eneo la maisha yako. Je umejenga msingi imara kiasi cha mafuriko na pepo kali za changamoto za maisha kukuacha salama? Ukiona unaanguka kwenye maeneo fulani ya maisha yako, basi tambua msingi wake pia sio imara.

Ifahamu leo misingi unayotakiwa kuijienga katika maisha yako na hivyo kuendelea kuwa imara maishani.

Msimamo. Je huwa unaamua nini baada ya kuambiwa wewe huwezi kufanya unachofanya sasa au unachowaza kukifanya? Una ndoto yako au wazo lako na kisha ukamshirikisha mtu, lakini akakuambia uache ndoto za mchana, unachukua hatua gani? Wengi wamezima ndoto zao na pia kushindwa kuyaishi mawazo mazuri waliyokuwa nayo kwa sababu ya kukosa msimamo. Kila wakati simama, jiamini na jiambie unaweza kufanya mambo makubwa hata yale ambayo wengine wanasema huwezi.

Uvumilivu. Je matokeo yakichelewa unakata tamaa? Je ukipata matokeo ambayo hukutarajia unakata tamaa? Je umekuwa mhanga wa kupenda njia za makato? Unahitaji kujenga msingi huu wa uvumilivu. Mafanikio makubwa na ya kudumu ni safari ngumu na ndefu, wanaofanikiwa ni wale tu wenye uvumilivu.

Kukua. Njia pekee ya kunufaika na changamoto ni kuigeza changamoto hiyo kuwa fursa. Utafanikiwa kufanya hivyo kama wewe utakuwa mkubwa kuliko changamoto hiyo. Unafanikiwa kuwa mkubwa kuliko changamoto kama utakuwa unakua. Ukuaji wa kwanza kabisa wa kunufaika na changamoto ni ukuaji wa ndani. Jifunze kwa kusoma vitabu, badili mitazamo yako nk. Ukikua ndani utazaiona fursa ndani ya changamoto.

Maandalizi. Wanasema muda mzuri wa kufanya mazoezi ya kivita ni kabla ya vita. Hivyo muda mzuri wa kuimarisha msingi wa nyumba yako ni kabla ya mafuriko. Kwenye kila jambo unalopanga kufanya, ainisha changamoto unazoweza kukutana nazo, kisha jiandae. Hii itakupa uwezekano mkubwa wa kuzishinda.

Hamasa. Safari ya mafanikio ni ngumu sana kwa sababu ya changamoto unazoweza kukutana nazo kila siku. Unahitaji nguvu ya kukufanya usonge mbele hata pale unapoona giza mbele yako. Hii inaitwa hamasa. Hamasa hujengwa kwa kujua kwa thati kabisa nini ni hasa unachotarajia kukipata kwenye mateso unayoyapata. Kwa nini ujitese? Kisha jenga imani ya kuwa utakipata kile unachokitaka.

Ndugu! Dhoruba zipo njiani zinakuja. Ili uendelee kusimama na kupigania kukipata kile unachotamani sana maishani mwako basi huna budi kuanza kujenga misingi hii ya maisha.

Kwa ushauri na mwongozo wa vitabu vya kukusaidia kujenga misingi hii kuwasiliana nami: 0752 206 899.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Mwanasayansi, Mwl & Mwandishi(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *