Hivi Ndivyo Majasiri Wanavyoishinda Hofu.


Categories :

Ukiwaona watu majasiri unaweza kuwaonea wivu na kutamani kuwa kama wao. Majasiri huchukua hatua hata zile ambazo watu wengine wanona wasingeweza. Mara nyingine majasiri wanapochukua hatua hizo hofu huanza kuwapata wao wasio na ujasiri.

Majasiri huchukua hatua ambazo zinaogofya. Kwa haraka unaweza kudhani wao wamezaliwa bila hofu, la hasha! Kuna hatua wanazochukua kwa mara ya kwanza au zile ambazo wamezifanya mara chache ambazo bado wanaziogopoa. Majasiri huendelea kuchukua hatua hizi si kwa sababu hawaogopi bali wanazichukua hata kama wanaogopa.

Kuna hatua ambazo wameendelea kuzichukua hata kama wanaogopa na sasa hawaziogopi tena. Kwa mfano watu wengi ambao wanaweza kusimama mbele za watu wakaongea kwa ujasiri mkubwa si kwamba mwanzoni waliokuwa hawaogopi la hasha! Walikuwa wanaogopa lakini mwanzoni waliendelea kulazimisha kuendelea kuchukua hatua hizo hata kwa kutetemeka.

Kumbe kuna njia mbili wanazotumia majasiri kuikabili hofu. Moja kukifanya kile wanachokihofia au kukiogopa. Pia baada ya kuendelea kufanya kitu hicho baadaye hofu ile huwakimbia.

Hivyo si kwamba majasiri hawazaliwi na hofu, bali huweza kuzithibiti hofu zao kwa kuziendea na mwisho wa siku hofu hizo huwakimbia.

Matajiri walikuwa na hofu mwanzoni za kuanzisha biashara lakini walijilazimisha kuanzisha biashara hizo hata kama walikuwa wanaogopa kupata hasara.

Watu wanoziishi ndoto zao si kwamba mwanzoni walikuwa hawana hofu juu ya mambo makubwa waliyotakiwa kuyafanya, bali walijipa ujasiri wa kuanza kuishi ndoto zao hatimaye wameshayapata matokeo makubwa

Wauzaji maarufu si kwamba mwanzoni walikuwa hawawaogopi wateja waliokuwa wanaonekana wana mapingamizi makali, la hasha bali waliwafikia wateja hao licha ya kuwa na hofu nao. Sasa ndiyo wamekuwa wateja wao wakubwa kwenye biashara zao.

Kuna msemo unasema woga sawa na umasikini. Huu msemo una ukweli ndani yake kwani kwani ili upate matokeo yatakayokupa utajiri maishani mwako huna budi kuchukua hatua. Kuna kitu huwa kinasimama katikati ya hatua na matokeo, kitu hicho ni hofu/woga.

Hofu ndiyo iliyokwamisha watu wengi sana kutopata wanavyovitaka. Wanaweka malengo na hatua za kuchukua ili kupata wanavyovitaka, lakini muda wa kuweka kazi unapofika wanahofia hatua hizo. Hofu hizo huwa juu ya kutokuwa na uhakika wa kupata matokeo hasa kwenye kitu unachokifanya kwa mara ya kwanza, au kuchekwa na watu wengine.

Huwezi kupata matokeo yoyote usipochukua hatua. Umekuwa ukipanga vizuri, hongera lakini utapata matokeo ya mipango yako kama utafanikiwa  kuacha woga kisha kuanza kuchukua hatua.

Basi leo jifunze kwa majasiri, fanya kile unachokihofia. Wazo la kukimbia kufanya kwa sababu ya hofu likatae kafanye tu hakuna njia nyingine.

Jihamasishe kwa kukumbuka kuwa hata majasiri nao huwa wanahofia lakini huchukua hatua zaidi ya kufanya kile wanachokiogopa. Na wewe anza sasa kuchukua hatua zile ambazo umeziogopa kuchukua kwa siku nyingi kisha kukusababishia kukosa majibu uliyoyatamani kwa muda mrefu.

Chukua hatua;

  1. Kaa chini sasa kisha tafakari na kuorodhesha vitu vyote ulivyopanga kuvifanya lakini hukuvifanya kwa kuhofia hatua za kuchukua. Pia ainisha ni matokeoa gani umeyakosa kwa kutochukua hatua hizo.
  2. Anza sasa kuchukua hatua moja baada ya nyingine kwa kujifunza kwa majasiri na walifanikiwa kwa kujisukuma kufanya vile unavyovihofia na kuendelea kufanya mpaka hofu zote zinayeyeuka.

Anza Leo Anza Sasa Anza na Ulichonacho.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *