Unaweza Kuwa Na Siku Nzuri Kila Siku .


Categories :

Leo sina “mood” ya kufanya kazi. Leo sijisikii kuongea au kuongoleshwa. Leo nina siku mbaya kazini. Siku za jumatatu siyo nzuri kazini.

Haya ni baadhi ya maneno ambayo yamekuwa yakisikiwa kwenye akili na midomo ya watu, inawezekana na wewe mwenyewe. Ni meneno yanayoashiria unaweza kuwa na siku nzuri au mbaya.

Kila mtu angetamani kuwa na siku nzuri ambayo ingemfanya kuwa mtu wa furaha, shauku na nguvu za kufanya kazi. Lakini haya hayatokei kwa sababu ya kuruhusu kuwa na siku nzuri au mbaya.

Mafanikio au kushindwa katika maisha yako hunategemea sana kama unakuwa na siku nzuri au mbaya. Wanaofanikiwa ni wale wanahakikisha kuwa kila siku ni njema kwako bila kujali changamoto zinavyoweza kujitokeza.

Kuna kitu kimoja kinachoamua siku yako iwe vipi. Ukikithibiti hicho utafanikiwa kuwa na siku njema na nzuri na kuwa na siku zenye mafanikio . Kitu hicho ni MTAZAMO.

Mtazamo wako ndio unaoamua uvionaje vitu. Kama akili yako imebeba mtazamo hasi utaona udhaifu kwenye kila jambo linalotokea mbele yako.

Kwa mfano kama una mtazamo kuwa siku za jumatatu huwa ni mbaya kazini utajiandaa mapema kabisa kutafuta ubaya au udhaifu wa siku hiyo. Kwa sababu hamu yako ni kuupata ubaya.

Inawezekana umemtafuta mchawi wa kushindwa kwako kwa muda mrefu, lakini mchawi mkuu wa siku yako kuwa mbaya ni mtazamo wako. Kumbe ukitengeneza mtazamo wako vizuri utakuwa na siku nzuri sana.

Zifuatazo ni njia unazoweza kutumia ili kuwa na mtazamo sahihi utakaokusaidia kuwa na siku njema. Siku njema itakuwa ni chachu ya kuwa na ufanisi mkubwa na mafanikio makubwa.

Ianze siku kwa mtazamo chanya. Kila uanapoamka jiambie leo utakuwa na siku nzuri, utakutana na mambo mazuri licha ya changamoto zinavyoweza kujitokeza. Jiambie huku ukiamini hivyo. Hii itakuwa kama antena kwako ya kuvuta mambo mazuri kwako huku ikisukuma mabaya mbali na wewe.

Usiambiwe ukaamini. Usiamini kirahisi chochote unachoambiwa. Imani hiyo ndiyo itakujengea mtazamo huo hasi. Kwa mfano mara ngapi umeambiwa mtu fulani ni mbaya, ana roho mbaya na ghafla ukaanza kumchukia hata kama hajamuona akitenda ubaya wowote?

Jiandae kutokwazika. Marcus Aurelius alitushauri nini cha kufanya ili tuwe na siku nzuri kupitia sehemu hii ya nukuu yake. “Today I shall be meeting with interference, ingratitude, insolence, disloyalty, ill-will, and selfishness – all of them due to the offenders’ ignorance of what is good or evil”
Kwa tafsiri isiyo lasmi alisema “Leo nitakutana na watu wasumbufu, wenye kukosa shukurani, dhulma, wasio na uaminifu, wenye nia mbaya, na ubinafsi – watafanya yote haya kwa sababu ya kutojua mema au mabaya”
Ukiianza siku kwa mtazamo huu itakuwa rahisi sana kwako kukabiliana na changamoto zozote zitakakukuta. Hata kama mtu akikutendea ubaya siyo rahisi kuharibu siku yako kwa sababu utajua kuwa amefanya hivyo kwa sababu ya kutojua mema na mabaya.

Usitafute ubaya ulipo. Epuka kuianza siku yako kwa kufikia vyanzo ambavyo vinavyoweza kukupa habari hasi. Chagua sana mitandao ya jamii ya kutembelea, usiingie na kusoma chochote. Kuna taarifa za kusikitisha na nyingi sio za kweli.
Epuka kuchangamana na watu ambao muda wote wanaongelea vitu hasi tu.

Ndugu! Naamini unatamani kuwa na siku njema yenye furaha na mafanikio. Dhamana hii ipo kwenye akili yako kwa kuwa na mtazamo sahihi wa mambo yanatokea kwenye siku.

Una uwezo wa kuthibiti mtazamo wako, hii ni nguvu ambayo hakuna mtu anaweza kukunyang’anya. Usikubali kuwa na siku mbaya tena.

[ ] Unapoamka jiambie utakuwa na siku nzuri
[ ] Usiruhusu vyanzo vyovyote vya habari hasi

[ ] Ukitendewa ubaya, jiambie hao watu hawajuai wema na ubaya

[ ] Usiambiwe mtu ni mbaya ua kitu ni kibaya na ukakiamini kirahisi.
Natarajia siku njema kutoka kwako kuanzia sasa.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *