Utajiri Unaanza na Hicho Kidogo.


Categories :

Moja ya kitu ambacho kingechaguliwa na wengi kutoka kwenye vitu ambavyo binadamu angapenda awe navyo ni UTAJIRI.

Utajiri ninaotaka kuzungumuzia hapa ni utajiri wa fedha. Utajiri wa fedha ni kuwa na kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinakupa uhuru. Uhuru wa kifedha ni hatua ambayo mtu hufikia ambapo fedha inakuwa sio kikwazo kwako kuishi maisha anayoyataka. Hivyo hula chakula anachokitaka, hununua gari analolitaka, hustarehe anavyotaka, hutembelea sehemu anayotaka nk.

Hili limekuwa ni tamanio la watu wengi lakini ni tamanio ambalo halitimii kirahisi na hivyo wengi kufa bila kuupata utajiri huo.

Moja ya njia ya kufikia utajiri ni kuweka akiba. Hiki ni kitendo cha kutoa na kuweka pembeni kiasi cha kipato chako.

Fedha hiyo huweza kutumika baadaye kwa ajili kuongeza thamani zaidi. Kwa mfano kiasi kikubwa kukikusanya huweza kutumika kama mtaji wa kuanzisha au kukuza biashara biashara au kuwekeza.

Moja ya sababu ambayo inawafanya watu wengi wasiwekeze ni kuamini kuwa wataanza kuwekeza wakiwa na kipato kikubwa.
[ ] Kwa sasa mshahara wangu ni mdogo, ukiongezeka na kuwa mkubwa ndipo nitaanza kuweka akiba
[ ] Biashara yangu ni ndogo inatoa faida ndogo, kwa sasa siwezi kuweka akiba mpaka biashara hii itakapokua
[ ] Kipato changa ni kidogo na cha kuungaunga nitakapokuwa na kipato kikubwa nitaanza kuweka akiba.
Ndugu, ni muda gani umepita tangu uliposema kipato chako hakitoshi kuanza kuweka akiba? Je ungekuwa umeanza sasa ungekuwa na sh?

Kuweka akiba ni tabia na utafanikiwa kujenga tabia hii na kukipeleka kwenye utajiri kama utaanza kuwekeza sasa kwa kipato hicho unachokiona kidogo.

Jack Beny alisema “Try to save something while your salary is small; it’s impossible to save after you begin to earn more” Ikiwa na tafsiri kuwa jisukume kuweka akiba angali mshahara wako ni mdogo, haiwezekani kuanza kuweka akiba pale utakapoanza kupata kipato kikubwa.

Kauli ya Jack ni sahihi kabisa. Kama unaona shida kuweka sh. elfu moja angali kipato chako ni sh elfu kumi itakuwa ni vigumu sana kuanza kuweka sh laki moja ambapo kipato chako kitakapokuwa milioni moja.

Kupata fedha na kutumia yote ni njia ya kujihakikishia utumwa wa kifedha. Unahitaji kuanza na kuendelea kuweka akiba na kuikuza ili kuweza kufikia utajiri na uhuru wa kifedha siku zijazo.

Muda sahihi wa kuanza kuwekeza ni sasa hata kama unaona una kipato kidogo sasa. Ili kuwezesha jambo hili unahitaji kuwa na nidhamu kali ya kutenga fedha hiyo kutoka kwenye kipato chako, kuitunza na kutotumia kama ulivyopanga.

Ili uweze kufanikiwa kujenga nidhamu hii muhimu ya kufikia unahitaji;

  1. Kuwa na kwa NINI KUBWA. Hii ni sababu ya kwa nini ujisukume kuweka akiba, je ili kupata utajiri na kuukimbiza umasikini unaokukabili sasa?
  2. Anza sasa ungali una kipato hicho kidogo. Ukifanikiwa sasa ambapo una kipato kidogo itakuwa rahisi kuweka akiba hata kipato chako kikiongezeka.
  3. Jisukume mwanzoni kwani utakutana na upinzani mkubwa. Lakini usipokata tamaa, baadaye itageuka kuwa tabia yako. Kumbuka kuweka akiba ni tabia ya kimafanikio.
  4. Tafuta gereza la kuweka akiba yako. Si rahisi kuitunza akiba yako sehemu unapoweza kuichukua kirahisi muda wowote ule. Ili uweze kufanikiwa kuitunza fedha hiyo weka sehemu ambapo huwezi kuchukua hata kama utakuwa na uhitaji mkubwa kiasi gani. Gereza linaweza kuwa akaunti ya benki ambayo huwezi kuchukua fedha hiyo mpaka baada ya muda maalumu. Kwa mfano akaunti ya CRDB inayoitwa DHAHABU.
  5. Andaa mpango wa matumizi wa akiba hiyo. Je unaweka akiba ili kupata mtaji wa biashara? Au kwa ajili ya kuwekeza na kuzalisha zaidi?

Ndugu wakati wa kuanza kuweka akiba ni sasa. Anza sasa anza na ulichonacho.

Asante.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *