Vikwazo Vitakaposimama Mbele Ya Safari Yako Ya Mafanikio, Fanya Hivi…..
Licha ya mipango na ndoto kubwa ulizonazo, malengo na mipango mizuri uliyonayo hayo yote hayatazuia wewe usikutwe na changamoto. Katika safari ya kusaka mafanikio makubwa unayostahili changamoto ni lazima zikukumbe.
Changamoto nyingine huja na maumivu makali kiasi cha mtu kufikiria kukata tamaa, au kuacha kile anachokifanya. Hiki pia ni kitu kikubwa kinachowatofautisha waliofanikiwa na walioshindwa; nini unafanya ukilutana na magumu tena maumivu. Hali hizi zinaweza kukutokea kadri unavyoendelea kuishi ndoto yako;
[ ] Baada ya kutengeneza ndoto yako kubwa na kuona ni nzuri sana kisha kumshirikisha mtu wako wa karibu sana, mtu huyo anakuambia anahisi umechanganyikiwa kwa kitu hicho hakiwezekani. Je utaendelea kuiamini ndoto yako?
[ ] Umekusanya mtaji kwa miaka mingi, muda umefika unasema ngoja nianzishe biashara, lakini unaibiwa fedha zote. Je utaanza vipya?
[ ] Umeanzisha biashara ya ndoto yako kabla hujafika mbali, duka hilo linaungua moto au wezi wanaiba vitu vyote? Je utaanza vipya?
[ ] Umekopa fedha na kuanzisha biashara baada ya kuambiwa biashara hiyo inalipa sana. Lakini baada ya kuanzisha, mauzo ni shida, hata waliokuambia biashara inalipa na watakuwa wateja wako wa kwanza, lakini sasa hawanunui kwako. Benki inahitaji fedha zake, utafanya nini?
[ ] Baada ya biashara kuanza kuchanua na kukupa faida, mara hali ya utulivu wa nchi inatokea, biashara inaanza kuyumba. Uatafanya nini?
[ ] Mmeweka mipango mizuri kama familia, baada ya kuanza kutekeleza na kuwa na mwelekeo mzuri, ugomvi kwenye mahusiano unaanza kiasi cha kutaka kuharibu utulivu. Utafanya nini?
Mambo hayo na mengine mengi yana nafasi ya kukutokea katika maisha yako. Je yakikutokea unafanya nini?
Wapo watu wanaokuwa na ndoto kubwa maishani mwao lakini zikayeyuka pale wanapokutana na upinzani, kushindwa au kukatishwa tamaa.
Lakini wapo wanaojaribu kitu mara nyingi sana bila kupata matokeo na hivyo kuamini hawawezi kupata matokeo wanayoyatafuta. Wanataka tamaa anagali walikuwa wanakaribia kupata matokeo.
Kuna kitu kimoja kinachoweza kukusaidia katika mazingira kama haya na ukafanikiwa kuvuka na kupata mafanikio. Unahitaji nidhamu ambayo itakusaidia kuendelea mbele licha ya vikwazo vitakavyokuwa vinasimama mbele yako, licha ya maumivu na kukatishwa tamaa kuelekezwa kwako. Kitu hicho ni NIDHAMU.
Kumbuka kuwa nidhamu ni kufanya ulichopanga bila kuruhusu sababu yoyote ile ikurudishe nyuma. Watu wengi wanakosa nidhamu kali ya kuendelea kufanya baada ya kukutana na vikwazo. Kwa sababu ya kukosa msukumo wa kuwalazimisha kuendelea baada ya kukatishwa tamaa.
Ili kuweza kujenga nidhamu kali ya kukabiliana na mambo yanapoenda kinyume na matarajio, fanya yafuatayo;
[ ] Jikumbushe KWA NINI yako kataka kipindi hiki. Hakikisha sababu ya kukifanya kitu hicho kuwa kubwa kuliko nguvu ya kukukatisha. Je kwa nini yako ni kupata uhuru wa kifedha hivyo kukatishwa tamaa hakuwezi kukuyumbisha?
[ ] Vumilia. Hakuna kitu kikubwa na kizuri kinachokuja kirahisi. Uwe mvumilivu. Matokeo yakichelewa usiache kuendelea
[ ] Weka malengo na ainisha vikwazo vinavyoweza kujitokeza mbele. Kikwazo hicho kikitokea itakuwa rahisi kujisukuma kuendelea kwani tayari ulitegemea.
[ ] Endelea kujaribu. Kama unafanya majaribio, kuna uwezekano wa kutopata matokeo mapema. Kwa mfano unaweza ukawa umeshajaribu biashara nyingi na usipate matokeo mazuri. Usiache kuendelea kujaribu, jaribu mpaka upate matokeo. Thomas Edison alifanya majaribio takriban mara elfu kumi kabla ya kufanikiwa kuitengeneza taa ya kwanza ya umeme. Wewe umejaribu mara ngapi?
[ ] Jiamini muda wote. Kuna kitu unacho ndani yako ambacho watu wengine hawakioni. Inaweza kuwa ndoto au uwezo wako. Kama bado havijatokea si rahisi watu wengine kuviona na kukuamini. Ndoto yako au lengo lako kubwa linaweza kupigwa mawe sana. Kujiamini kwako kwa kuona picha ya manufaa makubwa unayoyapata kukujengea nidhamu ya kusonga mbele licha ya kupingwa vikali.
Jiandae kwa hali yoyote inayoweza kujitokeza katika safari yako. Maandalizi haya ni ya kujenga nidhamu itakayokufanya usisikilize sababu yoyote bali ukaendelea kung’ang’ana na kile unachofanya.
Chukua hatua leo.
[ ] Tafakari leo kama kuna jambo uliliacha kulifanya baada ya kukutana na ugumu. Kumbuka matokeo mazuri utakayoyapata kisha liamshe tena leo. Utapata matokeo tu.
[ ] Je hamasa imeshuka kwenye jambo unalolifanya? Jipe moyo, ona ushindi mbele yako na jiambie kwamba hakuna kitu cha kukuzuia kupata ushindi kama wewe binafai utajiamini na kujiambia lazima ufike mwisho.
Nakutakia kila la kheri.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz