Toa Matokeo Sio Sababu
Kuna kila sababu ya kwa nini usifanye kitu. Lakini kunahitaji kazi tu ili utoe matokeo. Sababu za kutokufanya kitu ni nyingi sana na hiki ndicho kilichopelekea watu wengi kukosa matokeo huku wakibakia na uthibitisho kwa nini hawana matokeo.
Kutafuta sababu za kwa nini usifanye kile ulichopanga kufanya ni kutafuta raha za muda mfupi. Lakini kufanya kitu ili kupata matokeo huhitaji kujitoa na matokeo yake huchukua muda mrefu japo mara nyingi huwa ya kudumu.
Ili uweze kutimiza malengo yako na kufikia mafanikio makubwa huna budi kujenga nidhamu itakayokusaidia kujisukuma kuchukua hatua ili kupata matokeo na sio kukimbia kazi huku ukitafuta sababu za kwa nini usifanye.
Watu wengi huanza vizuri mchakato wa kupata mafanikio. Huweka malengo na mipango vizuri kabisa. Lakini ikifika muda wa kuchukua hatua, ndipo sababu au udhuru wa kwa nini asifanye kazi huanza kuota kama uyoga.
Watu waliofanikiwa ni watu wa matokeo na sio udhuru. Wakipanga kufanya kitu, hawana mbadala wa kazi hiyo zaidi ya matokeo. Hivyo hawatafuti sababu bali mbinu za kuleta matokeo. Hakuna mafanikio yoyote yanayopambwa na udhuru.
TOA MATOKEO SIO SABABU.
Hii ni nidhamu ya hali ya juu sana. Lakini ukifanikiwa kuijenga nidhamu hii lazima ufanikiwe. Kwani kazi na matokeo ndivyo vinavyokupa mafanikio.
Sababu zipo nyingi: Kinachowafanya watu kuwa washindi kwenye kutoa sababu na sio matokeo na kwa kuwa sababu zipo nyingi na zinapatikana kirahisi. Lakini unahitaji kutoa jasho ili kutoa matokeo
Sababu huonekana ni za kweli: Kitu kingine kinachowafanya watu kutoa sababu na sio matokeo ni sababu hizo kuwa na sura ya ukweli. Kama kuna sehemu unatakiwa kwenda lakini ukiangalia angani unaona wingu zito limetanda, ni rahisi sana kuahirisha safari kwani sababu hiyo itakuwa na sura ya ukweli hata kama mvua haitanyesha.
Kutokutoa sababu ni kujiffunga mwenyewe kuwa kwa hali yoyote ile wewe utatoa matokeo bila kujali ugumu ambao unaweza kukutana nao. Hivi ndivyo unavyoweza kufanikiwa kujenga nidhamu hii kali na kujihakikishia matokeo na mafanikio;
[ ] Hakikisha umeweka wazi kabisa nini unatakiwa ufanye na namna utakayotumia kufanya hivyo. Hii itakusaidia kupunguza sababu zinazoweza kutengenezwa kwa nini usifanye kitu hicho. Kama kazi ni kuwafikia wateja basi ainisha wapi wateja tarajiwa walipo, wangapi wanatakiwa wafikiwe na mbinu gani zitatumika.
[ ] Weka mbadala. Kwenye kila njia unayopanga kufanya jambo, weka mbadala wake. Binadamu hupanga lakini asili hutimiza mambo yake ambayo huweza kuwa tofauti na ulivyopanga, ukiweka mbadala kwenye kila mpango utashindwa kujitetetea kutokufanya kwa sababu kama moja itafunga, nyingine bado ipo wazi
[ ] Jilipishe zawadi au adhabu. Mtu hufanya tofauti pale anapojua kuna zawadi au adhabu atakayopata. Vyote viwili vinamsaidia sana mtu kutoa matokeo na siyo sababu. Pale anapotaka atoe udhuru kwa kutofanya, akikumbuka kuna adhabu tu atachukua hatua mara moja.
[ ] Wajibika kwa mtu. Watu hufanya tofauti pale wanapotambua kuwa kuna mtu anawatazama. Kuwa na Kocha au mtu mwingine ambaye atakuuliza kwa nini hujafanya ulichopanga kufanya itakusaidia wewe kijisukuma kuchukua hatua na kutoa matokeo
[ ] Jikumbushe KWA NINI kubwa. Pale unapotaka kutoa udhuru wa kutofanya jikumbushe faida kubwa utakayopata kwa kujisukuma kuchukua hatua.
Mafanikio ni kupata matokeo na sio kujifariji na sababu. Kauli hii ikae ndani yako na iishi; TOA MATOKEO NA SIO SABABU. Panga cha kufanya kisha ona kuwa una chaguo moja tu, matokeo siyo sababu.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz