Fanya Kazi Ya Masaa 8 Kwa Saa 1.


Categories :

Kama ufanisi wa kazi ungekuwa unapimwa kwa kiasi ambacho upo ‘busy’ basi leo u ungekuwa umefanikiwa sana. Bahati mbaya ufanisi wako unapimwa kwa matokeo unayoyazalisha.

Umekuwa ukiamka ukiwa na nguvu lakini unarudi jioni ukiwa umechoka sana. Ukilinganisha nguvu na muda uliowekeza kisha matokeo uliyoyapata ni vitu viwili tofauti. Mara nyingi matokeo yamekuwa kidogo kuliko nguvu na muda uliotumia.

Kikwazo kikubwa kinachosababisha ufanisi na matokeo ya kazi tunazozifanya kuwa madogo ni kukosa kuzingatia(Focus). Kuzingatia ni kukaa kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu bila kutoroka.

Kuna dhana ambayo imejengeka kuwa ukiwa unafanya kazi nyingi kwa wakati mmoja ndipo unaonekana unafanya kazi sana. Lakini ukweli ni tofauti na hicho kilichodhaniwa na watu wengi.

Chris Bailey anasema “One hour of hyperfocus can generate more results than an eight hour workday filled with distractions, interruptions and sidetracks” ikiwa na tafsiri kuwa saa moja lenye kuzingatia kwa kiwango kikubwa linatoa matokeo makubwa zaidi kuliko masaa nane ya kazi yenye usumbufu mkubwa.

Kumbe si kiasi cha muda ulichokaa kwenye kazi pekee kinachoamua upate matokeo kiasi gani bali nini umekizalisha kwa muda huo.

Usumbufu umekuwa kikwazo kikubwa cha ufanisi na mafanikio kwa watu wengi. Watu wanagusagusa tu kazi badala ya kuzifanya kazi.

[ ] Mtu anapanga kufanya kazi hii, kwa dakika chache anahamia kufanya kazi nyingine kabla hata hajafika mbali kwenye ile ya kwanza.

[ ] Unaanza kufanya kazi tu, simu inaita unaiangalia kisha kuipokea. Ukirudi kuifanya kazi ile ya kwanza inakuchukia muda mrefu sana kurudi kwenye utulivu ule wa awali.

[ ] Umeanza kufanya kazi mtu anakuja na kuanza kukuongelesha, unaacha ulichokuwa unafanya, unahamishia umakini kwake

[ ] Una kazi nyingi za kufanya, unaona kufanya moja ni kuchelewa hivyo kuamua kufanya nyingi kwa wakati mmoja. Unagawa umakini wako kwenye kazi nyingi, unafanya makosa mengi na kupata matokeo madogo. Unachoka sana lakini matokeo kidogo.

Haya na mengine yanayofanana ndivyo umekuwa ukifanya. Hii ni sababu mojawapo kubwa iliyokunyima matokeo makubwa. Pia imekunyima upekee wako umeishia kuwa mtu wa kawaida tu.

Lakini unaweza kufanya marekebisho sasa. Amua kuanza kuzingatia kwa kiwango kikubwa unapoamua kufanya kazi. Hii ni kuweka umakini wako kwenye jambo moja lenye thamani kubwa mpaka upate matokeo kabla hujahamia jambo jingine.

Hivi ndivyo unavyoweza kuzingatia(Kufokasi) kwa kiwango cha juu sana kisha kupata matokeo makubwa kisha kufanikiwa kutimiza malengo yako;

  1. Chagua kazi moja kutoka kwenye orodha yako. Chagua ya muhimu zaidi kuliko zote
  2. Ondoa usumbufu wote. Zima simu, jitenge na watu, ondoa vitu usivyotumia mahali unapofanyia kazi
  3. Ielekeze akili yako kwenye kile unachokifanya.
  4. Irudishe akili yako kila inapohamia kwenye jambo lile
  5. Endelea na hatua ya 4 mpaka ukamilishe jukumu moja kisha uendelee na jukumu jingine.

Ukifanya hivi ndipo utakapoanza kukamikisha kazi ulizokuwa unafanya kwa saa nane sasa kwa saa moja.

ANZA LEO ANZA SASA ANZA ULICHONACHO

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *