Zingatia Mambo Haya Sita(6) Kuboresha Maisha Yako.
Je ungependa uishi kikamilifu katika uhai wako? Leo jifunze mambo sita ambayo ukiyazingatia maisha yako yataongezeka thamani.
1. Kabla hujaomba amini. Dunia ipo tayari kukupa chochote unachokitaka. Dunia inakuhitaji uombe unachokitaka. Unataka utajiri omba! Unahitaji furaha omba! Unahitaji utoshelevu omba.
Lakini kabla hujaomba, tanguliza imani. Ndani yako lazima kuwe na imani, kuwa unachokiomba utapata. Unakipata unachokiomba kwa njia ya kuweka kazi. Hivyo amini kuwa kazi unayoiweka itakupa unachokitaka. Bila imani hakuna uvumilivu na ustahimilivu.
2. Kabla hujaongea sikiliza. Binadamu ana masikio mawili lakini mdomo mmjoa ili tuwe tunasikiliza zaidi kuliko kuongea. Usipende kujibu haraka kabla hujasikiliza vizuri.
Watu wamekosa fursa nyingi kwa sababu ya kukosa usikuvu. Ili uweze kujibu kwa usahihi sikiliza kwanza.
3. Kabla hujatumia pata. Pesa ni mambo mengi. Wengi hupenda kutumia hata kama wahajapata. Tunapata fedha kwa kutoa thamani kwa watu wengine.
Usitumie fedha zaidi ya kile unachokipata. Kabla hujafikiria kutumia fikiria kupata kwanza.
4. Kabla hujapokea toa. Chochote unachokitaka kukipata kutoka kwa watu wengine kitoe kwanza. Je unataka upendo kutoka kwa watu wengine? Wapende wengine kwanza. Unataka watu wengine wakuheshimu, waheshimu kwanza.
5. Kabla hujaacha jaribu. Vitu vizuri huviji kirahisi. Vinahitaji nguvu kubwa na uvumilivu. Kuna milima na mabonde unahitaji.
Kwa mfano kutengeneza utajiri ni safari ngumu iliyojaa vikwazo vingi. Kuna wakati utapata hasara kwenye biashara unayoijenga ili ikupatie utajiri. Hapo ndipo utataka kukata tamaa. KABLA HUJAACHA ENDELEA KUJARIBU MPAKA UPATE MATOKEO.
6. Kabla hujafa ishi. Ulizaliwa ili uishi. Umepewa uhai ili uishi. Muda ulionao ni wa wewe kuishi.
Je unaishi? Kuishi kwa faida na kwa uaminifu ni kuishi maisha yako. Huku ni kuishi upekee wako. Una kitu cha pekee ndani yako ambao ukikiishi hicho dunia utakuwa umeiishi kwa ukamilifu mkubwa.
Inawezekana umekuwepo hapa duniani kwa muda mrefu lakini bado hujaanza kuishi. Kama huishi upekee wako bado hujaanza kuishi.
Hujui ni lini utakufa ambapo ndiyo itakuwa huna muda tena. KABLA HUJAFA ISHI UPEKEE WAKO.
Ndugu naamini unatamani kuwa na maisha yenye ukamilifu katika maisha yako. Mambo haya sita ni muongozo wa kuwa na maisha bora kabisa. Yatafakari mambo haya kwa kina. Lipi utaanza nalo leo?
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz