Siku Utakapoanza Kujiuliza Swali Hili, Maisha Yako Yatabadilika Sana.


Categories :

Kuna majibu ya ajabu aliyapata mtafiti huyu ambayo na wewe unaweza kushangaa na kujifunza pia.

Mtafiti huyo aliamua kuwafanyia utafiti nyani. Aliwakusanya nyani kumi kisha kutengeneza kizimba. Ndani ya kizimba hicho aliweka ngazi katikati kisha kuning’iniza chana la ndizi juu kidogo ya ngazi hiyo.

Mtafiti huyo aliwaingiza nyani watano kwenye kizimba hicho kisha akaanza kuwachunguza. Basi kuna nyani wa kwanza akataka kupanda juu ya ngazi ile ili azifikie ndizi, basi yule mtafiti akamwagia maji ile ngazi kisha yule nyani kateleza na kurudi chini bila kuzifikia zile ndizi.

Hata wa pili alipotaka kupanda, basi yule mtafiti aliimwagia maji tena ile ngazi na nyani yule akateleza na kurudi chini. Nyani wa tatu alipotaka kupanda, mtafiti hakumwagia maji na nyani wenzake walipoona anazidi kupanda tu wakamkimbilia na kumvuta chini. Hii ikatokea vivo hivyo kwa nyani wa nne na wa tano.

Ndipo alipomwingiza nyani mmoja kati ya watano waliokuwa nje. Nyani huyo wa kwanza kutoka nje alipojaribu kupanda, wale nyani watano kwanza wakamvuta na kushuka chini. Akamleta wa pili wa nje, naye alipojaribu kupanda wale sita ikiwa pamoja na yule wa kwanza aliyetoka nje wakasaidiana kumvuta na kumshusha chini.

Hata alipoletwa wa tatu wa nje wale saba wakamfanyia vivo hivyo. Matokeo haya yakaenda mpaka kwa nyani wa mwisho.

Hivyo mpaka mwisho, hakuna nyani aliyefanikiwa kupanda juu ya ngazi na kula ndizi zile.

Cha kushangaza ni kila nyani aliyekuwa anaingia kwenye kizimba aliungana na nyani wengine kufanya waliyokuwa wanafanya licha ya muda mfupi waliokuwa wanaingia kizimbani.

Watu wanaokuzunguka wana nguvu kubwa sana ya kukufanya ufanikiwe au ushindwe. Ukizungukwa na watu wenye kiu na waliotayari kupiga hatua zaidi ya waliopo, watakusaidia na wewe kupiga hatua.

Lakini ukizungukwa na watu wanaoona wameshafika na si wahusika wa mafaniko yao, lazima watakukwamisha tu, hata pale utakapotaka kupanda juu yao lazima watakuvuta tu urudi chini ili ufanane nao.

Kamwe usiidharau nguvu ya watu wanaokuzunguka kuwa utawashinda. Ni suala la muda tu, utaungana nao.

Umezungukwa na watu gani? Unashirikiana na nani? Je watakufikisha kwenye ndoto zako za kufika juu? Au watakuvuta ushuke chini walipo pale utakapotaka kupanda?

Tafakari na chukua uamuzi!

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *