Usikubali Kutumbukia Kwenye Shimo Hili Kwa Hiari…..


Categories :

Matamanio ya mafanikio na mafanikio yenyewe havipo pamoja. Kuna safari ya kuiendea ili kuweza kuyafikia mafanikio hayo.

Lakini watu wengi wamekuwa hawaifiki safari hiyo kwa sababu ya kuishia njiani. Katika ya matamanio hayo na mafanikio hayo kuna mashimo mengi ambapo mtu hutakiwa kuyakwepa ili kuweza kuyafikia mafanikio makubwa maishani mwake.

Moja ya mashimo hayo ni BADO SIJAWA TAYARI. Hili ni shimo liliowameza wengi. Umekuwa na nia ya kufanya na kupata mafanikio fulani. Lakini ni muda mrefu sana tangu umeweka nia hiyo. Sababu kubwa ya kutoanza ua kuendeleza mipango yako ni kwa sababu unaona bado hujawa tayari.

Umeendelea kufanya maaandalizi ili kuwa tayari, lakini bado hujaweza kufikia hatua ya kuona kuwa upo tayari.

Umekosa fursa nyingi za kuyapata mafanikio unayoyatamani kwa sababu ya kutumbukia kwenye shimo hili refu la kuona hupo tayari na unahitaji kuendelea kujiandaa.

Umepoteza muda. Muda ni rasilimali ambayo ukiipoteza huipati tena. Ungekuwa umeanza hata kwa kuona bado hujawa tayari ungekuwa umepiga hatua fulani.

Umepoteza fursa. Kwa kipindi ambacho umekuwa ukijiandaa kuwa tayari, kuna mtu amekuwa tayari kufanya ulichopanga. Kumbuka ulikuwa na wazo fulani la kuanzisha biashara fulani mpya. Kwa muda uliondelea kusubiria kuna mtu ameanzisha biashara hiyo na kukutangulia.

Umeamua kuahirisha. Baada ya kuendelea kujiambia hupo tayari sasa umeamua kuahirisha kabisa. Maandalizi ya muda mrefu sana ni mwanzo mzuri sana kuahirisha kabisa. Kumbuka hata mtaji ulikuwa nao mwanzo umeshapunguza au kula kabisa.

Sasa imekuwa ni gharama zaidi. Kwa sababu ya kuendelea kusubiria kuwa tayari, kile ulichotaka kuanzisha sasa ni gharama zaidi. Hivyo kadri unavyoendelea kujipanga ndivyo na gharama zake zinaongeza.

Ndugu haitafika siku na kuona upo tayari kwa kila kitu. Vitu vingine vinaweza kuwepo lakini akili yako ikawa haipo tayari. Hivyo muda mzuri wa kufanya au kuendeleza ni sasa.

Umekuwa ukitafuta muda au kiasi kizuri cha kuwa tayari, napenda kukukuambia kuwa kama kweli una nia ya kukifanya kitu hicho basi muda wake ni sasa.

Chukua hatua;
Anza na kile ulichonacho. Kama ni biashara basi anza na mtaji ulionao. Anza na watu ulionao.

Lakini pia muda mzuri na uhakika wa kuanza ni leo tena sasa. Hakuna muda mwingine. Kwa kile ulichonachoa ,anza nacho sasa.

  1. Uwe tayari kuanza kuchukua jukumu la maisha yako.
  2. Uwe tayari kuweka malengo makubwa sasa.
  3. Uwe tayari kuanzisha biashara yako sasa.
  4. Uwe tayari kutafuta wateja wengi zaidi kisha kuikuza biashara sasa.
  5. Uwe tayari kuanza kusoma na kujifunza zaidi sasa.
  6. Uwe tayari kuanza kuandika kitabu cha maisha yako.

Anza Leo, Anza Sasa, Anza na Ulichonacho.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *